WMA yaanza kutekeleza agizo la Waziri Mkuu 

18Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
MTWARA
Nipashe
WMA yaanza kutekeleza agizo la Waziri Mkuu 

WAKALA wa Vipimo (WMA) umeanza kutekeleza agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, la kuitaka kuhakiki na kusimamia mizani yote itakayotumika kupima mazao ya pamba na ufuta nchini.

Katika utekelezaji huo, WMA pia tayari imetekeleza kwa vitendo kwa kukagua na kutoa elimu kwa mikoa ya Kanda ya Kusini inayolima ufuta ambayo ni Lindi, Mtwara na Ruvuma.

Mkurugenzi wa Ufundi wa WMA, Stella Kawa, alisema jana kuwa timu ya maofisa wake wanapita kwenye vyama vyote vya msingi kufanya ukaguzi wa kushtukiza, ili kujiridhisha kama ile mizani waliyoihakiki kabla ya msimu kuanza imeendelea kupima kwa usahihi, ili mkulima apate faida inayostahili kwenye mazao yake.

Stella alisema lengo la ukaguzi huo ni kuchochea wakulima kuongeza uzalishaji kwenye kilimo kwa kuwa na uhakika wa kupimiwa mazao yao kwenye mizani iliyo sahihi na kuchochea nia ya serikali ya kuwa na uchumi wa kati wa viwanda.

“Ili kufikia lengo mahsusi la serikali la kuwa na Tanzania ya viwanda kupitia malighafi za kilimo na matokeo yake ajira kwa Watanzania na pato la taifa vitaongezeka na uchumi wa mtu mmoja mmoja kukua na kufikia ule uchumi wa kati.

“Pamoja na mikoa inayolima pamba na ufuta, maofisa wetu wanapita kwenye AMCOS zote (vyama vya msingi) kufanya kaguzi mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha mizani yote inayotumika kupima mazao hayo ni sahihi na mkulima anapata kipato kulingana na jasho lake na si vinginevyo.

“Aidha, nitumie nafasi hii kutoa wito kwa wasimamizi wa vituo vya kuuzia ufuta na pamba kuhakikisha mizani haiharibiwi na wajanja wachache kwa maslahi yao binafsi na atakayekamatwa anadhulumu wakulima kupitia mizani atachukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema Stella.

Kwa mujibu wa Stella, katika baadhi ya AMCOS ambazo zimekaguliwa katika mikoa ya Lindi na Mtwara, mizani 50 kati ya 52 haikuwa na tatizo, huku mmoja ukikutwa ni mbovu na mwingine ulikuwa na kasoro ndogondogo ambazo zilirekebishwa mara moja.

Habari Kubwa