Zaidi ya 500 kufanyiwa upasuaji wa macho

14Mar 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Zaidi ya 500 kufanyiwa upasuaji wa macho

MADAKTARI bingwa wa macho kutoka Marekani wamepiga kambi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Chuo Kikuu cha Dodoma kutoa huduma ya matibabu ya macho kwa wakazi wa mkoa huo na mikoa jirani huku watu zaidi ya 500 wakitarajiwa kufanyiwa upasuaji.

Uchunguzi huo unatokana na wakazi wengi wa mkoa huo kusumbuliwa na matatizo hayo kutokana na kuugua mara kwa mara, sababu kubwa ikielezwa ni uhaba wa majisafi na salama.

Kufuatia changamoto hizo zinazowakumba wakazi wa mkoa huo, madaktari bingwa tisa kutoka Marekani wamejitolea kwa lengo la kutoa matibabu kwa wagonjwa wa macho pamoja na kubadilishana ujuzi na madaktari wa nchini.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, amewataka wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kwenye upimaji na matibabu katika hospitali hiyo.

Dk. Mahenge alisema, huduma hiyo imekuja wakati muafaka kutokana na serikali kuwa katika harakati za kuelekea uchumi wa viwanda ambao hauwezi kufikiwa kama wananchi watakuwa na afya zenye mashaka.

“Viwanda vyetu vinahitaji malighafi hivyo basi kama wananchi wako hawana afya zilizo bora huwezi kupata mazao ambayo ndiyo malighafi katika huu uchumi wa viwanda tunaoutaka sisi Watanzania,”alisema Dk. Mahenge.

Alisema wananchi wanatakiwa kuichangamkia fursa hiyo kutokana na kujumisha wataalamu bingwa wa macho pamoja na vifaa vya kisasa vinavyotumika katika siku tano za huduma hiyo ambavyo hawatavipata katika maeneo mengine.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk. Alphonce Chandika, alisema changamoto kubwa inayochangia magonjwa ya macho ni ukosefu wa huduma za majisafi na salama katika maeneo mengi. 

Habari Kubwa