Zaidi ya marais 10 kumuaga Magufuli kesho

21Mar 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Zaidi ya marais 10 kumuaga Magufuli kesho

MARAIS zaidi ya 10 kutoka katika mataifa mbalimbali, wamethibitisha kuhudhuria shughuli ya kumuaga aleyekuwa Rais wa Tanzania Dk. John Magufuli, itakayofanyika kesho Machi 22, Jijini Dodoma.

Taarifa hiyo imetolewa Leo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abasi, kwa kuwa hadi kufikia sasa ana orodha ya zaidi ya maraisi 10 walioahidi na kuweka majina yao wazi na nchi wanazotoka.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, amesema mwili huo utawasili Jijini humo Leo jioni Machi 21, 2021 katika uwanja wa ndege Dodoma majira ya saa 10:00 jioni na utalala Ikulu ya Chamwino  na Kesho Machi 22, 2021 utaagwa na Wananchi wa Mkoa huo wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi katika uwanja wa Jamhuri.

Mahenge amesema msafara wa gari litakalobeba mwili huo utapita katika barabara za Chako Chako, Nyerere, Bunge, Morena, Buigiri hadi Ikulu.

“Wananchi wote wa maeneo hayo mnaombwa kujipanga kwenye barabara hizo nilizozitaja ili kutoa heshima zetu za mwisho kwa mpendwa wetu,” amesema Mahenge.

Amesema Jumatatu ambayo itakuwa ni siku ya mapumziko, saa 12.00 asubuhi mwili huo utapelekwa uwanjani kupitia barabara mpya ya Mfugale, Buigiri, Morena, Bunge, mzunguko wa mkuu wa Mkoa na Nyerere, hivyo wananchi wameombwa kujitokeza kwa wingi zaidi katika shughuli hiyo.

Habari Kubwa