Zaidi ya milioni 161 zimekopeshwa kwa vikundi 43 Siha

19Dec 2021
Anjela Mhando
Siha
Nipashe Jumapili
Zaidi ya milioni 161 zimekopeshwa kwa vikundi 43 Siha

KATIBU wa Umoja wa Wanawake wa CCM, (UWT) wilayani Siha mkoani Kilimanjaro, Mwanaidi Kaleghela, amesema katika kipindi cha Mwaka 2020/2021 vikundi mbalimbali vya wanawake, vijana na walemavu vimewezeshwa kupata mkopo kwa ajili ya kuendeleza vipato na kukuza Uchumi.

Kaleghela amesema hayo wakati akisoma taarifa ya kazi za UWT jana katika Baraza la UWT lililofanyika katika Ukumbi wa CCM kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia January hadi Desemba 2021 ambayo imezingatia mambo mbalimbali yaliyofanyika kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Amesema katika utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Mwaka 2020/2021 wanawake vikundi 43 walikoposhwa jumla ya shilingi 161 ,028, 367.31 ambapo wanawake wengi waliopatiwa fedha hizo lengo lilikuwa ni la kuendeleza biashara zao na kupambana na hali ya maisha na kupiga hatua zaidi kimaendeleo lakini pia kuweza kuendeleza miradi mbalimbali waliyonayo ili kuepukana na utegemezi katika familia.

Hata hivyo amesema katika 10% inayotolewa na Halmashauri Mapato yake ya ndani ilitoa kiasi cha shilingi milioni 255 ambapo zilikopeshwa kwa wanawake vijana na wenye ulemavu, ambapo wanawake waliopatiwa kiasi cha shilingi milioni 161 na hiyo ikiwa ni Utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Amesema vijana vikundi 23 vimekopeshwa zaidi ya shilingi milioni 78 huku vikundi sita vya wenye ulemavu vilikopeshwa shilingi milioni 15 huku akieleza katika Jumuiya hiyo makundi yaliyotajwa ikiwa ni pamoja na wanawake wamethaminiwa na kupewa kipaumbele kwani wanawake wakiwezeshwa kiuchumi wanaweza.

Habari Kubwa