Zaidi ya watoto 900 wamefanyiwa ukatili Mbeya

17Jun 2021
Grace Mwakalinga
KYELA
Nipashe
Zaidi ya watoto 900 wamefanyiwa ukatili Mbeya

ZAIDI ya watoto 900 katika kipindi cha mwaka 2019/2020 mkoani Mbeya wamefanyiwa ukatili wa aina mbalimbali ikiwamo wa kingono, kutelekezwa na kunyimwa haki ya kupata elimu.

Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Dk. Angelina Lutambi.

Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Dk. Angelina Lutambi ameyasema hayo mkoani humo kwenye maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika ambayo yalifanyika kimkoa katika kijiji cha Ipinda wilayani Kyela.

Amesema watoto waliofanyiwa ukatili huo ni kuanzia miaka sifuri hadi 14 na kwamba  idadi ya watoto 196  walifanyiwa ukatili wa kingono, wa kimwili 222, kihisia 296 wa kutelekezwa 84.

“Takwimu hizi ndugu zangu ni mbaya, zinaonyesha ni jinsi gani jamii haiwajibiki na haizingatia sheria katika kuwajibika  kumlinda mtoto na vitendo vya unyanyasaji wa watoto huanzia ngazi ya familia, yatupasa kubadilika na kuongeza umakini katika malezi ya watoto  muhimu wanandoa kudumisha amani na upendo ili kuepusha madhara kwa watoto,” amesema Dk. Lutambi.

Ameongeza kuwa madhara yanayoweza kujitokeza endapo wazazi hawatakuwa na malezi bora kwa watoto  ni kuwa na idadi kubwa ya watoto yatima, wanaoishi katika mazingira magumu  ambao wengi wao huishia kuwa ombaomba mitaani na kujiingiza kwenye vitendo vya uhalifu, pamoja na kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Habari Kubwa