Zanzibar ilivyopaa miaka  54 ya Karume hadi Shein

13Jan 2018
Rahma Suleiman
Nipashe
Zanzibar ilivyopaa miaka  54 ya Karume hadi Shein

ATIMAYE Zanzibar ilitimiza miaka 54 ya Mapinduzi na kusherehekewa kwa kishindo kwenye Uwanja wa Amaan visiwani humo jana, huku mafanikio mbalimbali yakiwekwa wazi kwa kipindi chote hicho kuanzia awamu ya kwanza ya mwasisi wake, Abeid Amaan Karume hadi awamu ya sasa ya Dk. Ali Mohamed Shein.    

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein akikagua gwaride la Heshima katika sherehe hizo. PICHA:OWM

Katika sherehe hizo jana, tofauti na ilivyozoeleka katika miaka ya hivi karibuni, hakukuwa na burudani za ngoma na halaiki na pia hazikuchukua muda mrefu.

Sherehe hizo zilianza saa 1:00 na kumalizika saa 5:00 asubuhi kwa maandamano na gwaride maalumu la vikosi vya ulinzi na usalama, kisha baadaye ndipo Rais, Dk. Shein alipowahutubia wananchi. 

Ilielezwa kuwa sababu za kuchukua muda mfupi ni kutoa fursa kwa waumini wa dini ya Kiislamu kwenda kufanya ibada ya swala ya Ijumaa ambayo huanza kwa hotuba maalumu saa 6:00 mchana.

Licha ya sherehe hizo kuchukua muda mfupi, lakini zilionekana kufana kwa kiasi kikubwa huku wananchi pia wakijitokeza kwa wingi.

Aidha, mbali na Dk. Shein, viongozi wengine waliohudhuria ni Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na marais wastaafu wakiwamo Jakaya Kikwete, Benjamin  Mkapa, Ali Hassan Mwinyi, Dk. Amani Abeid Karume na Makamu wa Rais mstaafu, Dk. Mohamed Gharib Bilali.

MAFANIKIO TANGU KARUME Akihutubia katika sherehe hizo, Dk. Shein, alisema katika miaka 54 ya Mapinduzi, anajivunia kuimarika kwa huduma za elimu ambazo kabla, zilikuwa chache na zikitolewa kwa ubaguzi na kulipiwa.

Alisema hivi sasa shule za msingi zimeongezeka mara saba, za sekondari mara 53 na idadi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari imeongezeka mara 14 kutoka wanafunzi 25,372 mwaka 1963 hadi  378,211, mwaka 2017.

“Tatizo walilotutengenezea wakoloni kwamba watoto wa wafanyakazi na wakulima tusiingie sekondari na kupata elimu ya juu, leo halipo tena, haya ni mafanikio makubwa ya kuigwa,” alisema.

Alisema katika jitihada ya kuongeza madarasa, mwaka 2017 serikali ilianza ujenzi wa shule tisa za ghorofa za sekondari kwa Unguja na Pemba.

Alisema pamoja na hatua hizo, serikali inaendelea kushughulikia ununuzi wa madawati kwa ajili ya shule zote za Zanzibar ili kumaliza tatizo hilo.

Aidha, alisema kuanzia mwezi Julai mwaka huu, serikali yake itaanza kutekeleza azma ya kurudisha utaratibu wa kutoa elimu bure kwa shule zote za sekondari ili kutekeleza lengo la Mapinduzi.

“Kwa hivyo elimu ya msingi hadi sekondari itatolewa bure bila ya malipo,  kwa elimu ya msingi tayari ni bure,” alisema Dk. Shein.

Alisema pia serikali yake imepata mafanikio katika sekta ya afya kwa kuimarisha huduma za afya mjini na vijijini.

Alisema, kutokana na kuimarika kwa huduma hizo, vifo vya kinamama wanaojifungua vimepungua kutoka 237, mwaka 2016 hadi 195 mwaka 2017.

Alisema vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka 54 mwaka 2010 hadi 43 mwaka 2017.

Hata hivyo alisisitiza kuwa maendeleo yanategemea amani na usalama wa nchi na kuwataka wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kulinda nchi na kudumisha amani iliyopo.