Zanzibar kuongeza vivutio vya utalii visivyojulikana

25Jan 2021
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Zanzibar kuongeza vivutio vya utalii visivyojulikana

WAZIRI wa Utalii na Mambo ya Kale wa Zanzibar, Leila Mohamed Mussa, ameelezea mikakati inayofanywa na serikali kuboresha sekta ya utalii visiwani humo kwa kuongeza vivutio visivyojulikana ili kuongeza idadi ya watalii nchini. Fuatilia mahojiano haya:

WAZIRI wa Utalii na Mambo ya Kale wa Zanzibar, Leila Mohamed Mussa.

Swali: Uchumi wa Zanzibar unategemea sana sekta ya utalii, mlipuko wa virusi vya Corona umeathiri kwa kiasi gani sekta hii.

Jibu: Ni kweli Zanzibar kwa asilimia kubwa tunategemea sekta ya utalii, tunasema ni sekta mama. Karibu asilimia 28 ya GPD ya uchumi inategemea utalii na fedha za kigeni zaidi ya asilimia 80 zinatokana na mchango wa sekta ya utalii. Kipindi cha Corona Zanzibar tuliathirika sana, ilifika kipindi hoteli zilifungwa, viwanja vya ndege vilifunga, bandari zilifungwa, sisi wenyewe ilibidi tufunge. Ilifika wakati income (kipato) tulitetereka sana hatuna kabisa kipato mpaka salary (mshahara) ikawa changamoto kwa serikali. Wageni tukawa tunapata 300 tu kwa mwezi. Kipindi kile cha lockdown (kujifungia) Wizara ya Utalii haikukaa tu, ilikuja na recovering plan (mipango ya ufufuaji), lazima tujipange ili hali itakapoisha turudi katika hali ya kawaida na kipindi kile watu wengi walikosa ajira, si kwa hoteli tu hata wananchi wa kawaida. Kila mmoja kwa nafasi yake aliathirika na hata huduma muhimu ziliathirika kama umeme na maji.

Hata hivyo, katika ‘recovering plan’, tulifanya mikutano ya kimkakati kwa kufanya mawasiliano na balozi mbalimbali duniani kuangalia sehemu gani imeathirika sana na corona na wakati ule soko letu kubwa lilikuwa Ulaya Magharibi, nchi kama Uingereza, Canada, Marekani na Italia, ziliathirika sana. Tulioopona nchi za Ulaya Mashariki hazikuathirika sana, ikabidi tuhamie huko kutangaza soko letu la utalii, nchi kama Poland na nyingine, ndiyo maana soko letu limehamia huko. Unaona sasa mashirika mengi sana mageni ambayo yalikuwa hayana safari za Zanzibar yanakuja. Tulikuwa katika hali mbaya sana. Asante Mungu sasa wamerudi na biashara Zanzibar inaendelea.

 

Swali: Zanzibar inasifika kwa kuwa na fukwe nzuri na kubwa, je, ni kwa kiasi gani utalii wa fukwe umeendelezwa na umesaidia kiasi gani kuongeza idadi ya watalii na mapato visiwani humo.

Jibu: Zanzibar is a beautiful island (kisiwa kizuri) it’s a romantic, natural beauty (kina uzuri wa asili), ukiingia tu unavutiwa na mandhari yake, ukiingia Zanzibar unatokea kwenye fukwe ya pale Forodhani, nakubali kuwa fukwe hazijaendelezwa kwa potential (uwezo) ya uvutiaji kwa utalii. Serikali katika awamu ya nane imeamua kujipanga kuhakikisha mtalii atakapofika Zanzibar anapata vivutio mbalimbali kama michezo ya kwenye maji, ngoma za asili na sehemu za kitamaduni za asili, badala tu ya kuangalia fukwe anapotoka anapata ladha tofauti.

Tunataka mtalii apate vivutio vingine, tunayo misitu kama ya Jozani na Ngezi, ambayo tutaiongezea ubora na viwango ili badala ya mtalii anapoingia kukutana na kitu kimoja pekee, apate vitu mbalimbali na kuwa na kumbukumbu nzuri ya pale anapokwenda.

Zanzibar tunajitangaza sana kwenye fukwe, mara nyingi watalii wanapokuja kwenye fukwe na wakishaziona anakuwa hana hamu ya kurudi tena. Kwa hiyo awamu ya nane itatangaza vyanzo vyetu vya historia, mtalii asiishie kwenye fukwe tu, atembelee vyanzo hivyo kama House of Wonders (jumba la maajabu), ambalo ndiyo alama ya Zanzibar. Hivi vyanzo vya historia, serikali itafanyakazi pamoja na sekta binafsi kwa kukodisha, kuingia ubia au kupangisha, katika maeneo yanayovutia sana. Hivyo lazima tuviboreshe viwe katika hali ya kisasa ili watalii wapate kwenda. Kuna nchi nyingi ambazo hazina fukwe, lakini maeneo yao ya kihistoria yanawaingizia watalii wengi. Kwa mfano nchi ya Misri zile pyramids zinawaingizia mapato mengi.

Uzoefu unaonyesha watalii wanapokuja hawana utamaduni wa kurudi, labda hatuwapatii huduma nzuri kwa sababu hatuwapi vitu vya kutosha. Kuna sehemu za kihistoria kama Mwinyi Mkuu, Mtoni, Pukuchani ruins, hizi tutaziboresha ili mtalii akija kwa siku zake nane hawezi kuchoka.

Swali: Kuna fursa ilitolewa kwa Zanzibar na Rais John Magufuli wiki iliyopita kwamba iuziwe wanyamapori kutoka hifadhi ya taifa. Hatua zipi zilizofikiwa hadi sasa?

Jibu: Hiyo ofa tuliisikia na tulifurahi sana, kwa sababu katika plan zetu (mipango) tulisema tujenge national park, kwa sababu Zanzibar tuna sehemu za kihistoria, tuna beach (fukwe), lakini tuna miradi mingi ya kuanzisha ya kuibua vivutio vipya sehemu za kitalii. Focus yetu kwa sasa ni private enterprises kuhamasisha wawekezaji kuja kuwekeza katika shughuli za utalii na iwe rahisi kushindana. Serikali iwezeshe kuboresha miumbombinu, kama barabara, viwanja vya ndege, hilo tumelichukua na tunalifanyia kazi, kuna walioonyesha kuvutiwa na kuja kuomba katika miradi mbalimbali ya uwekezaji.

Swali: Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imeeleza kuwa ifikapo 2025 Tanzania iwe inapokea watalii kutoka milioni 1.5 hadi milioni sita, mapato ya utalii kutoka Dola za Marekani milioni 2.6 hadi Dola milioni sita. Je, Zanzibar imejipangaje?

Jibu: Katika kipindi cha miaka mitano matarajio yetu kama tulivyoahidi kwenye ahadi zetu ni kuingiza watalii 800,000 na kutoa ajira 300,000 kwa upande wa Zanzibar. Wizara kwa upande wake itahakikisha inaongeza vivutio vya utalii pamoja na miundombinu ya hoteli. Vitu hivi vinapoongezwa namba ya ajira itaongezeka katika taasisi hiyo.

Mkakati wetu unasema Tourism for all (utalii kwa wote), kwa kuanzisha kamati za wilaya za utalii ambazo zitaongozwa na wakuu wa wilaya kuhamasisha wanavijiji husika kuangalia usalama wa watalii, shughuli za maendeleo za miradi ya utalii na kupewa nafasi za ajira katika vituo hivyo vya utalii. Hii inakuwa rahisi kwa kuwa mpaka mtu wa chini atafaidika katika eneo husika na kuchangia. Tumeamua kuwa watu wa chini kwa mfano walinzi, watoke eneo lile lile badala ya kutoka nje kwa sababu wanajisikia na wao sehemu ya mradi badala ya kuwa wapenzi watazamaji, hiki kitu katika sekta ya utalii hatutaki, tunataka kila mtu anufaike katika sekta hii.

Swali: Mji Mkongwe ni sehemu ya kihistoria ya Zanzibar na hali ya majengo yake inaonyesha kuchoka. Je, serikali ina utaratibu gani wa kushirikisha wadau wengine ili kuyafanyia ukarabati na kurudisha hadhi yake?

Jibu: Baada ya kuanguka Jumba la Maajabu, Rais Dk. Hussein Mwinyi, aliitisha kikao cha wizara pamoja na wadau wa mji mkongwe. Majengo yale yapo tangu mwaka 1800 na yamejengwa na mawe, udongo na chokaa, lakini mji wa stone town ni urithi wa dunia ambao Shirika la Umoja wa Mataifa UNESCO, linakuwa na masharti yake katika kuyajenga.

Katika huu ushirikiano na sekta binafsi tunafanya tathimini ya majengo yote kuhakiki kujua ubora wa majengo hayo, kuna mengine yapo katika hali mbaya ambayo watu wanatakiwa kuondoka na mengine ni ya kuboresha, ndiyo maana ya kuwashirikisha wadau, kwa sababu serikali haiwezi kumiliki kila kitu. Na katika yale majengo kuna yanayomilikiwa na serikali na mengine ya watu binafsi, cha msingi ni kuwasimamia katika kuboresha kwa kiwango ambacho UNESCO inataka. Kuna majengo ambayo ni mali ya Shirika la Nyumba Zanzibar na mengine ni kwaajili ya wakfu ambayo yapo kwaajili ya wakfu tangu kipindi hicho, kuna yale ambayo watu hawawezi kuishi tumeona tuyafunge kwanza yaweze kurekebishwa na ambayo hayafai ni bora watu kuwaondoa. Pia tumeona umuhimu wa kuanzisha mfuko wa mji mkongwe na serikali iko katika mchakato wa kuwezesha wadau kulipwa fidia na kutakuwa na fedha maalumu kwa ajili ya ukarabati.

 

Swali: Jumba la Maajabu baada ya kuanguka litarudi katika hadhi yake ya zamani au litabadilishwa.

Jibu: Jengo lilifanyiwa assessment na jana tumewapokea watu wa UNESCO kwa ajili ya kuliscan na umadhubuti wake, na kama litawezekana vipi liwe, lakini no matter what, lazima lirudi kama lilivyo. Jengo limeanguka likiwa katika mikono ya makandarasi. Kilichoanguka ni kuta na madirisha, ndani kulikuwa hakuna kitu chochote, vitu vyote vya kumbukumbu vimehifadhiwa. Jengo limeanguka asilimia 16.6 tu. Jengo lina muumiza kila Mzanzibari hatuwezi kukubali alama yetu kuondoka kirahisi.

Wafadhili Serikali ya Oman wamekuwa nasi bega kwa bega katika ujenzi, serikali tunachofanya ni kulilinda ili lisiendelee kuanguka kwa kuweka nguzo kufunika mabati ili ikitokea mvua lisiendelee kuharibika. Kwa hiyo msijali lile litarudi.

Swali: Serikali ina mpango gani wa kurahisisha upatikani wa vipimo vya corona.

Jibu: Zanzibar tunakusanya sample (sampuli) na kupima, inapotokea baadhi ya wakati pengine vifaa vinashindwa kufanyakazi ndiyo tunakwenda bara, lakini ni kweli kuna changamoto kupatikana kwa majibu inapotokea wageni kuwa wengi. Tumeweka vituo kama hospitali binafsi, kwa mfano Lumumba, Nungwe, vipimo vyote vinapimwa sehemu moja. Kama serikali tunahakikisha kero zote hizi zinapungua. Sampuli kwa wageni iko katika kituo cha Migombani. Lakini pamoja na changamoto hiyo tumesikia hata watu wa bara wanakuja Zanzibar kuchukua vipimo. Kila siku serikali iko katika kuboresha mazingira na sasa hivi sisikii tena malalamiko ya kuchelewesha kupata majibu.

Swali: Serikali imejipanga vipi kutumia mitandao ya kijamii kutangaza sekta ya utalii.

Jibu: Utalii ni biashara na biashara ni kujitangaza. Ndiyo changamoto kubwa tunaikuta sasa hivi, kwa sababu watu walikuwa wanasubiri watalii waje ofisini kuulizia. Kama serikali tunataka kutumia effectively mitandao ya kijamii. Tuna timu kama Yanga na Simba na watu mashughuli kutoa hamasa kwa kutumia kurasa zao kutangaza vivutio vyetu vya utalii katika mitandao ya kijamii.

Habari Kubwa