Zanzibar yapigia debe hospitali binafsi

19Mar 2017
Rahma Suleiman
Nipashe Jumapili
Zanzibar yapigia debe hospitali binafsi

WIZARA ya Afya Zanzibar imesema kuanzishwa kwa hospitali binafsi kutasaidia kupunguza msongamano mkubwa wa wagonjwa katika Hospitali ya Rufani ya Mnazi Mmoja.

Waziri wa Afya Zanzibar, Mahmoud Thabit Kombo, akisikiliza maelezo kutoka kwa, Dk Ameesh Mehta (kulia) baada ya wakati wa ufunguzia Hospitali hiyo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa hospitali ya binafsi ya Dk. Metha’s iliyoko Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Naibu Waziri wa Afya, Mahmoud Thabit Kombo, alisema kumekuwapo na mrundikano mkubwa wa wagonjwa katika hospitali za mikoa na rufani, hivyo kuanzishwa kwa hospitali hiyo kutasaidia kupunguza tatizo hilo.
 
Alisema kutokana na wingi wa wagonjwa katika hospitali hizo za serikali, madaktari waliopo hawakidhi mahitaji katika kuwahudumia wagonjwa.
 
“Zanzibar nzima ina madaktari 280 na 150 wako masomoni katika nchi mbalimbali, hivyo bado madaktari ni kidogo ikilinganishwa na idadi ya watu kwani sera ya afya inasema kila daktari mmoja anapaswa kuwa na wagonjwa 600, hivyo bado lengo hilo halijafikiwa,” alisema Mahmoud.
 
Alisema Serikali ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kama sera ya afya inavyoeleza ili wananchi wapate huduma bora za afya.
 
Alisema serikali haiwezi kuipuuza sekta binafsi kutokana na umuhimu wake kwa kuwa inasaidia kuokoa maisha ya wananchi, kutoa huduma za afya na kuajiri vijiana katika sekta ya afya.
 
Alimpongeza mmiliki wa hospitali hiyo kwa kuwajali wazalendo katika utoaji wa huduma za afya kutokana na kuweka kiwango nafuu cha matibabu kwa wazawa wa kijiji hicho na Wazanzibari kwa ujumla.
 
“Katika hospitali hii kila mzalendo atatozwa Sh. 2,000 kwa ajili ya kumwona daktari na kiwango hicho hicho kwa ajili ya huduma ya dawa,” alisema.
 
Mmiliki wa Hospitali hiyo, Dk. Gaurang Metha, alisema ameweka viwango tofauti vya matibabu kati ya watalii na wazawa ili fedha itakayotozwa kwa mtalii imsaidie pia mwananchi wa Zanzibar ambaye anahitaji huduma za matibabu.
 
Alisema kuwa kijiji cha Nungwi ni ukanda wa utalii na kimezungukwa na hoteli na watalii kutoka nchi mbalimbali hufika, hivyo ni vyema wananchi wa Nungwi wakanufaika katika kupata huduma bora za afya.
 

Habari Kubwa