Zanzibar yatahadharisha magonjwa ya kuambukiza

24Feb 2021
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Zanzibar yatahadharisha magonjwa ya kuambukiza

SERIKALI ya Zanzibar imewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya maradhi ya kuambukiza ikiwamo corona.

Tamko hilo lilitolewa jana na hayo yalielezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi), Dk. Khalid Salum Muhammed, na kusema hivi karibuni kumejitokeza wananchi wengi kusumbuliwa na maradhi ya homa ya mapafu, homa kali na shida ya kupumua.
 
Alisema serikali inaelewa jambo hilo na inalifuatilia kwa karibu sambamba na kuchukua jitihada kubwa kupitia wataalamu wa afya ili kudhibiti hali hiyo.
 
“Kama tunavyofahamu kuwa dunia imeendelea kuathiriwa milipuko mbalimbali ya maradhi, yakiwamo maradhi ya homa ya mapafu, homa kali, shida ya kupumua na maradhi yanayosababishwa na virusi vya corona (Covid-19); hali hii inapelekea haja ya kuchukua tahadhari kwa ajili ya kulinda maisha ya wananchi wetu,” alisema waziri huyo.
 
Alieleza kuwa wakati serikali inaendelea na jitihada hizo, ni vyema kuchukua tahadhari za kujilinda na maradhi  hayo ili kupunguza maambukizi ya maradhi yanayoambukiza katika jamii.
 
Aidha, Dk. Khalid alisema kila mmoja anatakiwa kuzingatia kudumisha usafi wa mikono kwa kunawa mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni au vitakasa mikono (sanitizers).
 
“Maeneo yote yanayotoa huduma kwa watu wengi ni vyema wahusika wakaweka sehemu na vifaa vya kunawia mikono kwa maji tiririka na sabuni au vitakasa mikono,” alisema Dk. Khalid na kuongeza:

“Tuepuke mikusanyiko isiyo ya lazima muda wote na pale tunapolazimika kukaa watu wengi kwa pamoja tukae kwa masafa ya angalau mita moja kati ya mtu na mtu.”
 
Aliwataka wananchi kuvaa barakoa hasa zile zilizotengenezwa kwa vitambaa na barakoa hizo zifuliwe kwa maji na sabuni kabla ya kutumia tena.
 
Alisema kwa wale wenye dalili za kukohoa, mafua makali au shida ya kupumua wanatakiwa kuripoti katika kituo cha afya kilicho karibu ili kupata ushauri unaostahiki.
 
Alizitaka taasisi zote za serikali na zisizo za kiserikali kuweka mazingira mazuri ya kutekeleza masharti ya kiafya ili kujilinda na maradhi hayo, ikiwamo kuweka vitakasa mikono katika maeneo mbalimbali, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na kuelimishana juu ya kinga ya maradhi ya kuambukiza katika maeneo ya kazi.
 
Katika kukabiliana na tatizo hilo, Dk. Khalid alishauri kuendelea kutumia dawa za kiasili kwa ajili ya kinga na tiba ya maradhi mbalimbali, na wananchi waendelee kutulia na kusikiliza maelekezo ya wataalamu yatakayokuwa yakitolewa kupitia Wizara ya Afya au taasisi zengine za kiserikali. 

Habari Kubwa