ZEC yafyeka majimbo ya uchaguzi

03Jul 2020
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
ZEC yafyeka majimbo ya uchaguzi

TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imefanya mapitio ya idadi, majina na mipaka ya majimbo ya uchaguzi Zanzibar na kuyapunguza kutoka 54 hadi 50.

Imesema mapitio hayo yamefanyika kwa kuzingatia kifungu cha 120(4) cha Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Hamid Mahmoud, alisema tume imeamua kuyafuta majimbo manne ya uchaguzi, hivyo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kutakuwa na 50 badala ya 54 yaliotumika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Jaji Mahmoud alisema kuwa katika uchaguzi uliopita, majimbo ya uchaguzi yalikuwa 54, lakini kuliibuka malalamiko ya wadau kuhusu mabadiliko yaliyofanyika kupata idadi hiyo ya majimbo kutokana na kusababisha usumbufu kwa wapigakura kwa baadhi ya majimbo.

Kiongozi huyo alisema wadau wa uchaguzi waliibua matatizo ya uwapo wa tofauti kubwa ya wapigakura kati ya jimbo moja na lingine.

Alisema kuwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, ZEC ilijadili kwa kina suala hilo na iliamua kwa mamlaka iliyonayo kufanya uchunguzi wa kina juu ya madai ya dosari ziliripotiwa na wadau kwa lengo la kujiridhisha kama kweli kuna shida.

“Katika kazi hiyo, tume iliangalia kigezo cha idadi ya watu katika majimbo na uwakilishi unaofaa katika miji mikubwa na miji ya mashamba yenye idadi ndogo ya watu," alisema.

Alibainisha kuwa tume imeangalia kigezo cha ongezeko la idadi ya watu katika maeneo mbalimbali kwa kutumia takwimu za hesabu ya Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012.

Mwenyekiti huyo alisema uchunguzi huo unaonyesha idadi ya watu wanaohamia katika miji ya mashamba kutokana na sababu mbalimbali za kiuchumi na kijamii, inaongezeka kwa kasi sana katika maeneo ya Wilaya za Magharib A na B Unguja, Wete na Mkoani, Chakechake kisiwani Pemba.

Alisema tume pia iliangalia kigezo cha njia kuu za usafiri katika majimbo na mipaka ya utawala ili kuondoa usumbufu wa kuwachanganya wananchi katika maeneo yao ya uchaguzi.

Aliyataja majimbo yaliyofutwa kuwa ni Jimbo la Kiwengwa, Mtopepo, Kijitoupele na Chukwani ambapo Wilaya ya Magharibi B kutakuwa na majimbo matano badala ya saba na Kaskazini B kutakuwa na majimbo matatu badala ya manne na Magharib A kutakuwa na majimbo matano badala ya sita.

Alisema kwa upande wa Pemba, Jimbo la Mgogoni limefutwa na limeundwa Jimbo la Pandani, hivyo Unguja sasa kutakuwa na majimbo 32 na Pemba 18.

Habari Kubwa