ZEC yatangaza mshindi kabla ya kura kupigwa

30Jul 2021
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
ZEC yatangaza mshindi kabla ya kura kupigwa

TUME ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imemtangaza Mgombea wa CCM, Ali Hassan Mambo, kuwa mshindi katika uchaguzi mdogo wa nafasi ya udiwani baada ya mgombea wa ACT-Wazalendo kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari kwenye Ofisi za ZEC Wilaya ya Kati Unguja Dunga, Msimamizi wa Uchaguzi kutoka ZEC, Said Ramadhan Mgeni, alisema amelazimika kumtangaza mgombea huyo kuwa mshindi baada ya mgombea mwenzake, Haji Omar Iddi, kujiengua katika uchaguzi huo kutokana na agizo la chama chake.

Alisema kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ya mwaka 2018, analazimika kumtangaza Mambo kuwa mshindi hata kabla ya siku ya uchaguzi huo ambao ulitarajiwa kufanyika Agosti 14, mwaka huu.

"Kwa mamlaka niliyopewa kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi Na. 14 ya Mwaka 2018, ninamtangaza Ali Hassan Mambo kuwa mshindi katika uchaguzi wa nafasi ya udiwani wa wadi ya Chwaka kwa sababu mpinzani wake amejiondoa katika kinyang’anyiro hicho," alisema.

Baada ya kutangazwa mshindi, diwani mteule alisema: "Ninapenda kuchukuwa nafasi kukishukuru chama changu kwa kunipendekeza kugombea nafasi hii na hatimaye kuibuka na ushindi bila ya kupingwa."

Katibu wa CCM Kusini Unguja, Suleiman Mzee Charasi, alimpongeza mgombea huyo kwa kuibuka na ushindi bila ya kupigwa, akisisitiza kudhihirisha uwezo wa CCM na kukubalika kwa wananchi.

"Huo ndiyo ubora wa Chama Cha Mapinduzi katika siasa za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ambapo ushindi ni lazima katika ngazi mbalimbali," alisema.

Uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Agosti 14, mwaka huu, kufuatia kufariki dunia kwa aliyekuwa diwani wa wadi hiyo, Mlenge Khatib Mlenge, Machi mwaka huu.