Zilivyokuwa saa sita hukumu ya Sabaya

16Oct 2021
Allan Isack
ARUSHA
Nipashe
Zilivyokuwa saa sita hukumu ya Sabaya

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha imemtia hatiani na kumhukumu kifungo cha miaka 30 jela aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya (34) na wenzake wawili.

Mbali na Sabaya, washtakiwa wengine katika shauri hilo, ni Silvester Nyegu (26) na Daniel Mbura, waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka matatu ya unyang’anyi wa kutumia silaha.

Akisoma hukumu hiyo iliyochukua muda wa karibu saa sita jana, Hakimu wa Mahakama hiyo, Odira Amworo, alisema kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani, mahakama imewatia hatiani na kuwahukumu kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kutenda makosa hayo matatu.

Hakimu Amworo alisema kosa na kwanza na la pili ni la unyang’anyi wa makundi pasipo kutumia silaha, ambalo Sabaya na wenzake waliwatendea Numan Yasin na Ramadhani Rashi katika duka la Mohame Saad lililoko Mtaa wa Bondeni jijini Arusha.

Alisema kuwa kosa la tatu ni la unyang’anyi wa kutumia silaha ambalo washtakiwa hao walimtendea Bakari Msangi kwa kumpiga, kumfunga pingu, kumtishia kwa silaha na kumpora fedha Sh. 390,000.

Hakimu huyo, akisoma hukumu hiyo, alisema hakuna ubishi kwamba Sabaya akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mwenye mamlaka ya uteuzi, alitenda makosa hayo kinyume cha sheria.

Kadhalika, alisema kwa kuwa mikono yake imefungwa kutokana na sheria, hawezi kutoa adhabu za zaidi ya kifungo cha miaka 30 japokuwa wametiwa hatiani kwa makosa matatu na kila kosa ni miaka 30, hivyo watatumikia kwa pamoja.

Alisema kosa la kwanza, la pili na la tatu ni vifungo vya miaka 30 kwa kila kosa na wakati mwingine vifungo hivyo vinakwenda sambamba na adhabu ya viboko, lakini alikataa ombi la Wakili wa Jamhuri adhabu hiyo kutekelezwa sambamba na viboko.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Filex Kwetukia, alidai kwamba washtakiwa hao hawakuwa na kumbukumbu wala rekodi ya kutenda makosa ya jinai ya unyang’anyi wa kutumia silaha.

Kwa kosa la kwanza na la tatu aliomba mahakama kutoa hukumu ya kuwafunga miaka 30 jela sambamba na kuchapwa viboko kama sheria inavyoelekeza.

Vilevile, kwa kosa la pili aliiomba mahakama washtakiwa hao kuchwapwa vikoko kwa kuwa ni matakwa ya kisheria na hilo liko wazi.

“Tunaomba adhabu hii kali itendeke kwa kuwa Sabaya alikuwa mteule wa Rais na alifanya vitendo vya unyang’anyi wa kutumia silaha na kutumia makundi ni kinyume cha mamlaka iliyomteua ili iwe fundisho kwa wengine katika jamii hasa viongozi waliopewa dhamana na serikali na watu,”alidai Kwetukia.

Wakili huyo alidai kwamba utetezi wa umri kwa washtakiwa hao hauna mashiko katika kutaka kupunguziwa adhabu kwa kuwa walipaswa kufanya kazi ya kujipatia kipato halali pasipo kujiingiza katika vitendo vya uhalifu.

Baada ya maeleza hayo kutoka kwa Wakili wa Jamhuri, Wakili wa Mshtakiwa wa kwanza (Sabaya), Mosses Mahuna, alidai sheria imeeleza wazi ukitiwa hatiani kifungo ni cha miaka 30 na kinaweza kuambatana na viboko au vasiwapo.

“Tunaomba umwonee huruma mshatikiwa wa kwanza, hili ni kosa lake la kwanza na alikuwa mtumishi wa serikali na amelitumikia taifa hili, hivyo tunaomba mahakama kutoa adhabu ambayo imeangalia vizuri kwa kutambua huduma alizotoa katika jamii,” alidai Mahuna.

Alidai kuwa mshtakiwa alitoa ushirikiano kwa vyombo vya dola wakati alipokamatwa na pia bado ni kijana mdogo na ni nguvu kazi ya taifa na endapo atafungwa kifungo cha miaka mingi, maisha yake yataishia gerezani, hivyo aliomba kupewa adhabu ya muda mfupi ili arejee uraiani kulitumia taifa.

“Familia, mke na watoto wanamtegemea, tunaomba adhabu iwe kwa pamoja kwa makosa yote, kwa kuwa adhabu ikiwa kwa kila kosa atafungwa miaka 90, tunaomba ikiwezekana iwe miaka 30 tu," alidai Mahuna.

Awali majira ya saa mbili asubuhi, wananchi walianza kufurika katika viwanja vya mahakama huku askari wakiwa wametapakaa kila kona ya viunga vya mahakama hiyo.

Hakimu aliingia katika viwanja vya mahakama majira ya saa 2:25 asubuhi kabla ya kuanza kutoa hukumu hiyo majira ya 5:57 asubuhi na kufikia tamati ya hukumu saa 11:47 jioni.

Baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Sabaya na wenzake walionekana kuwa na nyuso za huzuni na wenye hofu kubwa huku ndugu jamaa na marafiki wakionekana kusikitika.

Nipashe ilishuhudia mama mzazi wa Sabaya akitoka ndani ya chumba cha mahakama mapema kabla ya kusomwa kwa hukumu hiyo.

Habari Kubwa