Zimamoto Kagera kuanza ukaguzi shule, vyuo

15Sep 2020
Lilian Lugakingira
BUKOBA
Nipashe
Zimamoto Kagera kuanza ukaguzi shule, vyuo

Kaimu Kamishna Oparesheni Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Charo Mangare ameagiza makamanda wote wa mikoa kuhakikisha wanakagua mara kwa mara shule na vyuo, ili kuhakikisha kama kuna vifaa vya kuzimia moto na kama idadi ya wanafunzi wanaolala kwenye bweni umezingatiwa kwa mujibu wa kanuni ya ukaguzi.

Hayo ameyazungumza leo Septemba 15, 2020 katika eneo la Shule ya Msingi Byamungu Islamic ambayo bweni moja la wavulana liliteketea kwa moto usiku wa kuamkia jana na kusababisha vifo vya wanafunzi 10 na majeruhi sita.

Mangare amewataka wamiliki wa shule kuzingatia ujenzi unaofuata ushauri wa kitaalamu kwa kuwasilisha michoro wanapotaka kujenga mabweni, kuongeza madarasa au vyumba vya ofisi, ili majengo yanayojengwa yawe salama zaidi.

"Nina imani kubwa kuwa kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu wakati wa ujenzi, tutapunguza kwa kiwango kikubwa matukio ya moto" amesema.

Pia amewataka wamiliki wa shule za bweni na vyuo kuhakikisha wanafunga vifaa vya kung'amua moshi na vizimia moto vya awali, kwa lengo la kuimarisha usalama na kupata taarifa mapema na kukabiliana na moto kabla haujaleta madhara.

"Hivi karibuni kumekuwa na matukio mengi ya moto katika shule kadhaa za bweni, ambayo yameleta athari mbalimbali ikiwamo vifo kwa wanafunzi na kuteketea kwa mali, hivyo jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaendelea kuweka mikakati ya kukabiliana nayo" amesema Mangare.

Aidha amewataka wananchi kuwa watulivu kwa kipindi hiki ambacho uchunguzi juu ya tukio hilo unaendelea, na kusubiri hatua zitakazochukuliwa baada ya kugundua chanzo na sababu za moto huo. 

Habari Kubwa