Zimamoto: Tulichelewa kupata taarifa za moto Soko la Karume

19Jan 2022
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Zimamoto: Tulichelewa kupata taarifa za moto Soko la Karume

JESHI la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala, limesema taarifa za kuungua moto kwa Soko la Karume, Mchikichini zilichelewa kuwafikia.

Kadhalika, limesema linaamini kama taarifa hizo zingefika mapema, wangeokoa mali kwa asilimia kubwa na kuepusha athari kubwa iliyojitokeza katika tukio hilo.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mrakibu Msaidizi wa Jeshi hilo Mkoa wa Ilala, Elisa Mugisha, wakati akihojiwa na kipindi cha Super Breakfast cha East Africa Radio, Mikocheni, Dar es Salaam.

Alisema licha ya kufika na kukuta moto umekuwa mkubwa, pia mazingira katika soko hilo hayakuwa rafiki kutokana na kutokuwa na nafasi ya kupitisha gari.

“Watu waliona moto mapema, lakini wakaanza kupambana nao. Sisi tulipata taarifa saa 9:30 usiku, wakati wanatupatia taarifa tayari moto ulikuwa umeshakuwa mkubwa,” alisema Mugisha.

“Kulikuwa na magari manne ya kuzima moto na tulizunguka sana kulingana na mazingira ya pale. Taarifa ingetolewa mapema, tungeudhibiti na waliokuwapo walipoona umewashinda wakaanza kuokoa mali zao,” aliongeza.

Soko hilo liliungua usiku wa kumkia Januari 16, mwaka huu, huku chanzo chake kikiwa bado hakijajulikana.

Tayari timu ya uchunguzi imeundwa na inasubiriwa ndani ya siku saba kutoa majibu ya chanzo pamoja na athari halisi zilizosababishwa na moto huo.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’ilabuzu Ludigija, timu hiyo inajumuisha ofisi yake, ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jeshi la Polisi na la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Pamoja na kuundwa timu ya kufanya kazi hiyo, juzi wafanyabiashara wa soko hilo walifunga barabara na kuandamana hadi ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, wakishinikiza waruhusiwe kujenga vibanda vya muda ili waendelee na biashara.

Walidai kuwa hawawezi kusubiri mpaka siku saba kutokana na ugumu wa maisha na sehemu hiyo ndiyo ilikuwa tegemeo lao.

Kutokana na maandamano hayo, Jeshi la Polisi liliwatawanya kwa mabomu ya machozi na baadaye Mkuu wa Wilaya alifika na kuwaomba wavute subira mpaka uchunguzi umalizike.

Mkuu wa Wilaya aliwaruhusu kuweka alama katika maeneo yao na kwamba baada ya timu kumaliza kazi yake kwa muda uliowekwa wataruhusiwa kujenga vibanda vyao.

Habari Kubwa