Zimamoto waongeza magari 12 kuboresha utendaji

10Aug 2020
Renatha Msungu
Simiyu
Nipashe
Zimamoto waongeza magari 12 kuboresha utendaji

JESHI la Zimamoto na Uokoaji, limeongeza magari 12 yaliyotengenezwa na kiwanda cha Nyumbu ili kuboresha utendaji kazi wake hasa kwenye majanga ya moto.

Kamishna wa Utawala na Fedha wa Zimamoto, Mbaraka Semwanza, alibainisha hayo wakati maonyesho ya Nanenane kwenye viwanja vya Nyakabindi mkoani hapa.

Semwanza alisema magari hayo yatawasaidia katika kazi zao za kila siku za uokoaji katika majanga ya moto yanayotokea sehemu mbalimbali.

"Tunaendelea kufanya jitihada za kuongeza vifaa, lengo ni kufanya kazi kiufasaha pale askari na watendaji wetu wanapohitajika waweze kufika kwa haraka," alisema Kamishna Semwanza.

Semwanza alisema magari hayo yako katika Kiwanda cha Nanyumbu jijini Dodoma yakitengenezwa kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika jeshi hilo.

Kamishna huyo pia alizungumzia kifaa cha kusaidia kuvuta hewa safi pale askari wao wanapokuwa katika kazi za uokoaji hususani katika majanga ya moto, akisema kimebuniwa ili kutoa huduma iliyobora katika kuwasaidia wananchi na kuokoa mali zao.

Alisema mbali na uhaba wa vifaa vya uokoaji, kuna tatizo la ujenzi holela wa makazi katika maeneo mbalimbali nchini, akibaininisha kuwa linachangia kuzorotesha utendaji kazi pale gari la Zimamoto linapotaka kwenda eneo la tukio.

“Watu wengi wanaongea kuwa magari ya Jeshi la Zimamoto yanachelewa eneo la tukio, lakini hawajui na sisi changamoto gani tunakutana nazo ambazo ni nyingi," alisema.

Alisema jeshi hilo linatumia maonyesho hayo kutoa elimu kwa wananchi jinsi ya kujikinga na majanga ya moto pamoja kutoa elimu ya kutumia vifaa vya Zimamoto kwenye sekta ya kilimo.

“Zimamoto pia imekuwa ikitoa huduma kwa wakulima kwani kuna wakati mashamba na ya maghala ya chakula yanaungua, hivyo elimu tunayoitoa hapa itawasaidia wakulima kujikinga na majanga ya moto," alisema.

Habari Kubwa