Zitto achambua kitabu cha Mkapa

14Nov 2019
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Zitto achambua kitabu cha Mkapa

MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, amesema wakati akiwa mbunge hakuwahi kumuelewa Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, na kwamba kupitia kitabu hicho amemuelew

MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, picha mtandao

Aidha, alisema kitabu hicho kimempa majawabu ya baadhi ya mambo ambayo alikuwa akijiuliza wakati ule. Kwa mfano suala la ubinafsishaji wa mashirika ya umma na namna ulivyotekelezwa.

Kwa mujibu wa uchambuzi wake wa kitabu hicho kilichozinduliwa juzi jijini Dar es Salaam, alisema Mkapa ameandika na amejitahidi kuwa mkweli wa nafsi yake.

“Watu wanaweza kuwa na tafsiri tofauti, lakini kama alivyosema mwenyewe mengi ni kuibua mjadala. Naamini mjadala utakuwapo tu,” alisema Zitto.

Alisema akiwa kijana mdogo wa miaka miaka 29, alichaguliwa kuwa Mbunge, na akiwa humo alikuwa ni mwenye hasira kulingana na namna nchi ilivyokuwa inaongozwa.

“Niliona utawala wa Rais Mkapa kama mmoja ya tawala za rushwa kuliko zote kupata kutokea. Nilikuwa naumizwa sana na hali ya umasikini nchini na namna rasilimali madini zilivyokuwa zinaporwa.

Kwa hiyo nilikuwa nikimtazama Mkapa kama kiongozi asiyejali watu maskini na aliyeuza nchi kwa wageni,” alisema Zitto.

Zitto ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, alisema Mkapa ameeleza mageuzi makubwa aliyoyafanya kwenye uchumi.
“Nimeridhika na maelezo yake mazuri, lakini sikubaliani naye kuhusu ulazima wa kubinafsisha mashirika namna ile,” alibainisha.

Mbunge huyo ambaye wakati huo alikuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini, alisema Mkapa anasema hapakuwa na mbadala kwenye ubinafsishaji lakini . ulikuwepo kwa kuwa Rais Ali Hassan Mwinyi alishafungua Uchumi.

Alisema alipaswa kuachia sekta binafsi kushindana na mashirika ya umma badala ya kuwauzia watu kwa bei ya kutupwa na mashirika kutoendelezwa. Alisema serikali ya Mkapa ilijielekeza kwenye ubinafsishaji kama tafsiri ya kujikwamua kiuchumi na kwamba China hawakuuza mashirika bali waliruhusu sekta binafsi kushindana na mashirika na matokeo yake yakawa chanya sana.

Alisema kuhusu fedha za kodi kuendesha mashirika, Rais Mkapa angekuwa wazi zaidi kuwa kutoyapa fedha mashirika na kuruhusu sekta binafsi kuanza kushindana nayo, kungekuwa na viwanda vya nguo, korosho na vinginevyo.

Kwa mujibu wa Zitto, Mkapa ameonyesha kukiri kuhusu wizi wa EPA, na kwamba anafurahi kwa kuwa alikuwa mbunge pekee niliyeamua kuzuia jambo kama EPA kutokea tena kwa kuweka sheria ya vyama vya siasa kukaguliwa na CAG.

“Katika hili Mkapa ametendea haki nchi, lakini alipaswa kwenda hatua ya pili na kuomba radhi kwa kuruhusu wizi wa namna ile ambayo ulikuwa na madhara makubwa kwa nchi yetu,” alisema.

Mambo mapya

Kwa mujibu wa Zitto, wasomaji wa kitabu hicho watafurahia historia ya nchi kwa kuwa Mkapa alifanya kazi karibu na Hayati Mwalimu Julius Nyerere. Kadhalika, alisema katika kitabu hicho kuna mambo mapya unayapata kuhusu Nyerere kama wakati wa vita ya Uganda, alikuja Rais wa Sudan, Jaffar Nimeiry kujaribu kusuluhisha.

“Mwalimu alimwambia Mkapa, yaani hata huyu anaongelea demokrasia, ameingiaje madarakani? Mwalimu alimpotezea Rais huyo. Kuna simulizi tele kuhusu ukombozi wa Afrika na namna sera yetu ya mambo ya nje ilivyokuwa inatekekezwa,” alisema Zitto.

Alisema Mkapa ametoa mafunzo kwa viongozi wa sasa na wa baadaye kuhusu msingi wa maamuzi mengi ya nchi yetu.

Kwa mujibu wa Zitto, kuna mambo Mkapa hakusema na ingetupa maarifa sana, akitolea mfano vita ya uasi Jimbo la Biafra nchini Nigeria na maamuzi ya Mwalimu kuunga mkono waasi Biafra.

Alisema Mkapa anaeleza kuhusu yeye kuwa balozi nchini humo baada ya vita na ziara ya Mwalimu Nigeria, lakini haelezi kwa undani hali ulikuwaje?

“Alipofika Nigeria watu walikuwaje? Mzee Obasanjo alipata kunihadithia kuwa ilibidi amsindikize Mwalimu kila mahala kwenye ziara ile kwa sababu wa Nigeria walikuwa na hasira na Tanzania, Zambia, Gabon na Ivory Coast kwa kutambua uasi wa watu wa kabila la Igbo,” alisema na kuongeza:

“Nilitaraji Rais Mkapa angesema zaidi eneo hili. Hapa ametunyima uhondo.”

Mkapa akemee yanayoendelea

Kwa mujibu wa Zitto, Rais Mkapa anapaswa kukemea yanayoendelea nchini haswa ukandamizaji wa demokrasia na kuwatenga wapinzani.

Zitto alisema Mkapa ameonyesha kuhusu kuumizwa na mambo hayo kwenye kitabu, lakini hakemei hadharani.

“Sura ya mwisho ya kitabu chake ni malalamiko ya namna Afrika inaendeshwa na haswa Tanzania na mambo mengi asiyoyapenda hayasemi hadharani. Kama Rais mstaafu anapaswa kusema na kuonya. Wasipoonya sasa wasionye nchi ikiwa kwenye machafuko,” alisisitiza Zitto.

Aidha, alisema amefurahishwa na jinsi Mkapa alivyoeleza maisha yake ya utoto na makuzi, ikiwamo maisha yake ya ujana pale Chuo Kikuu cha Makerere.

“Sikujua kuwa Rais Mkapa alikuwa na ‘demu’ wa Kimarekani akiitwa Hilary. Pia alipenda sana dansi na siasa za wanafunzi. Mungu ampe maisha marefu zaidi Mzee Mkapa,” alimalizia Zitto.

Habari Kubwa