Zitto ahoji ziliko bil. 800/-

15Apr 2019
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Zitto ahoji ziliko bil. 800/-

KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ameitaka serikali kuonyesha ziliko Sh. bilioni 800 anazodai matumizi yake hayaonekani katika mwaka wa fedha 2017/18.

Zitto alitoa kauli hiyo jijini Dodoma jana, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha 2017/18 iliyowasilishwa na serikali bungeni jijini hapa Jumatano iliyopita.

Zitto alidai chama chake kimeichambua ripoti hiyo katika maeneo 10 muhimu, huku akitoa mapendekezo tisa ambayo serikali inabidi kuyafanyia kazi likiwamo la kuimarisha mifumo.

Mbunge huyo wa Kigoma Mjini pia aliishauri serikali kutambua kuwa njia bora ya kupambana na rushwa na ufisadi ni kuwezesha mifumo kufanya kazi, akieleza kuwa mtu mmoja hawezi kamwe kuwa dawa ya ufisadi ulioota mizizi nchini.

Zitto alidai: "Serikali ionyeshe ilipo Sh. bilioni 800 isiyoonekana matumizi yake katika ripoti ya CAG ya mwaka wa fedha 2017/18. Sh. bilioni 800 hazikutolewa kwa ukaguzi.

"Katika uchambuzi wetu wa mwaka jana, tulionyesha kuwa asilimia sita ya fedha zilizokuwa zimekusanywa na serikali hazijulikani zilipokwenda."

Alidai kiwango hicho ni sawa na Sh. trilioni 1.5 ambazo mjadala wake ulichukua mwaka mzima hadi hoja hiyo iliposababisha kufanyika kwa uhakiki maalum wa CAG.

Zitto alidai bado serikali ilishindwa kuonyesha zilipokwenda fedha hizo, zaidi ya kudai kuwa ilihamishia Ikulu matumizi ya Sh. bilioni 976 bila kumpa CAG uthibitisho wa uhamisho huo.

Aidai kuwa katika ukaguzi wa CAG wa bajeti ya mwaka 2017/18, ambayo ni ya pili kwa serikali ya awamu ya tano, ameonyesha bajeti ya Sh. trilioni 31.7 iliidhinishwa na Bunge.

“Serikali iliweza kukusanya Sh. trilioni 27.7 tu kutoka kwenye vyanzo vyote vya kodi, vyanzo visivyo vya kodi, mikopo ya ndani na nje, na misaada ya wahisani na washirika wa maendeleo.

"Ilishindwa kukusanya kiasi cha Sh. trilioni nne kama ilivyokuwa mwaka uliopita ingawa sasa ni sawa na asilimia 13 ya bajeti yote ya mwaka 2016/17," Zitto alidai.

Aliendelea kudai kuwa CAG anaonyesha Sh. trilioni 26.9 tu ndiyo zilitolewa kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali na kwenda kutumika, hivyo Sh. bilioni 800 kati ya Sh. trilioni 27.7 zilizokusanywa kutokujulikana ziliko na hazikutolewa kwa ukaguzi.

Zitto alinukuu ripoti ya CAG ya mwaka 2017/18 ukurasa wa 91 akisema: “Ikilinganishwa taarifa ya kutoa fedha (exchequer issue report) na taarifa ya fedha zilizopokewa na kuripotiwa katika taarifa za fedha za mafungu husika pamoja na barua za kukiri mapokezi ya fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, imebaini utofauti wa taarifa zilizoripotiwa.”

"CAG ameeleza kuwa tofauti hiyo imesababishwa na kutokuwapo kwa mifumo thabiti ya usuluhishi kati ya fedha zilizotolewa na Hazina na fedha zilizotolewa na wahisani wa maendeleo moja kwa moja kwenye miradi ya maendeleo katika wizara.

"Ni muhimu sana kusisitiza hapa kuwa kwa mujibu wa CAG kuna fedha Sh. trilioni 4.8 ambazo makusanyo yake hayakuingizwa mfuko mkuu wa serikali.

Kiongozi huyo pia alidai Sh. bilioni 678 za mamlaka nyingine ziliporwa na mlipaji mkuu wa serikali.

Alidai kwenye ripoti ya CAG ya 2017/18 imeonyeshwa kuwa bado serikali inatumia fedha ambazo siyo zake (ring fenced) kama ilivyoonyeshwa kwenye ripoti ya mwaka 2016/17.

Alidai kwa mwaka 2017/18 CAG amebaini jumla ya Sh. bilioni 678 zilizokusanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa niaba ya taasisi nyingine, hazikuhamishwa kwenda kwenye taasisi husika, na badala yake zilihamishiwa kwa Katibu Mkuu Hazina, ambapo huko hazikuonekana kwenye ukaguzi kama sheria inavyotaka.

“Fedha zilizoporwa na Hazina ni pamoja na Sh. bilioni 169 za Shirika la Reli, Sh. bilioni 168 za wadau wa korosho nchini na Sh. bilioni 16 za Wakala wa Umeme Vijijini (REA).

"CAG kwa mara nyengine tena amependekeza sheria iheshimiwe kuhusu matumizi ya fedha hizi za taasisi mbalimbali. Kwenye ripoti ya CAG ya mwaka 2016/17 kiasi cha Sh. trilioni 2.2 za mamlaka mbalimbali nchini hazikurejeshwa kwenye mamlaka husika baada ya fedha hizo kukusanywa na TRA," Zitto alidai.

Pia aliitaka serikali ieleze kwanini Sh. trilioni 4.8 hazikupita kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina ili utolewaji wake ufuate masharti ya katiba na sheria za nchi.

“Fedha hizi za wafadhili zinaonekana katika vitabu vya bajeti, lakini CAG hazioni kuingia Mfuko Mkuu na hivyo kutoka kwake kunaweza kuwa ni kinyume cha sheria,” alidai.

Zitto aliishauri serikali kutambua kuna njia ya bora ya kupambana na rushwa na ufisadi ni kuwezesha mifumo kufanya kazi, akieleza kuwa mtu mmoja hauwezi kamwe kuwa dawa ya ufisadi ulioota mizizi nchini.

Habari Kubwa