Zitto ahukumiwa kifungo cha nje mwaka 1

30May 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Zitto ahukumiwa kifungo cha nje mwaka 1

MBUNGE wa Kigoma Mjini wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe, amehukumiwa kutumikia kifungo cha nje cha mwaka mmoja baada ya kukutwa na hatia ya makosa matatu ya uchochezi.

Kadhalika, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemwamuru kutoandika na kutoa maneno ya uchochezi kwa muda wa mwaka mmoja.

Hukumu hiyo imetolewa jana na mahakama hiyo iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi 15 wa Jamhuri na wanane wa utetezi akiwamo Zitto mwenyewe.

Alisema, maneno aliyoyatoa Zitto hayana ukweli, makali na magumu mno ambayo yameshindwa kuthibitishwa kwenye utetezi wake mahakamani.

"Mahakama hii bila kuacha shaka imeona utetezi wa mshtakiwa umeshindwa kuthibitisha kwamba askari wamemuua nani na ushahidi unaonyesha tukio lilifanyika alfajiri muda ambao huwezi kusema nani alimuua nani, maneno yalikuwa mazito, watu 100 kufa sio kitu kidogo mpaka kutaja watu wa kabila fulani hii ni sawa na kuwasha moto kwenye nyasi kavu," alisema.

Alisema jamii ina watu wenye uelewa tofauti kutokana na uwezo wa kuchuja maneno, hivyo kila mmoja anaweza kuchuja kwa kadiri anavyoweza.

"Mahakama hii imekuona una hatia, inakutia hatiani kwa makosa yote matatu, mmezoea kuandika mitandaoni kwamba Kisutu imegeuka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mshitakiwa utatumikia kifungo cha nje cha mwaka mmoja kwa masharti, usiandike na kutoa maneno ya uchochezi kwa muda huo," alisema Hakimu Shaidi.

Alisema kama kuna upande ambao haujaridhika na hukumu hiyo una haki ya kukata rufani ndani ya siku 30.

Awali, Upande wa Jamhuri uliopokea hukumu hiyo uliongozwa na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Renatus Mkude na Wankyo Simon.

Mkude alidai kuwa Jamhuri inaomba mahakama kutoa adhabu kali kwa Zitto ili iwe fundisho kwake na kwa wengine.

Hata hivyo, wakili wa utetezi, Frank Mwakibolwa, aliiomba mahakama kuwa mshtakiwa ana familia inayomtegemea, baba wa watoto wadogo wanne na ni mkosaji wa mara ya kwanza.

Wakati wa usikilizwaji wa ushahidi, kesi hiyo iliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka, akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga, huku upande wa utetezi ukiongozwa na mawakili Jebra Kambole, Mwakibolwa na Bonifacia Mapunda.

Kadhalika, wakati wa kipindi cha usikilizwaji wa kesi hiyo upande wa mashtaka uliwasilisha mahakamani vielelezo vya nyaraka na video iliyodaiwa kurekodiwa na askari mpelelezi, Sajenti James, kwenye mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam, Oktoba 28, 2018.

Video hiyo iliwasilishwa mahakamani hapo Desemba 4, 2019, na kupokelewa baada ya mabishano huku upande wa utetezi ukitaka video hiyo isipokelewe, lakini hatimaye mahakama ilipokea ushahidi huo na video hiyo ilionyeshwa.

Katika kesi ya msingi ilidaiwa kuwa Oktoba 28, 2018, Zitto aliitisha mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika ofisi za Makao Makuu ya ACT-Wazalendo, uliodaiwa kuwa na lengo la kuleta chuki kwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinyume na sheria na kwamba alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi.

Habari Kubwa