Zitto ajitosa kupinga kodi ya taulo za kike 

22Jun 2019
Godfrey Mushi
DODOMA
Nipashe
Zitto ajitosa kupinga kodi ya taulo za kike 

MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), ameitaka serikali ijitafakari kama mwaka mmoja ilioutoa unatosha kupima matokeo ya sera ya mwaka jana iliyoruhusu msamaha wa kodi kwenye taulo za kike.

MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe.

Kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo amepinga pendekezo la serikali kurejesha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye taulo za kike, akiamini ni uamuzi wa haraka na unaharibu sifa ya Tanzania.

Zitto aliyasema hayo bungeni jijini Dodoma jana, alipochangia mjadala kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2019/20 na mapendekezo ya bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha.

Katika mapendekezo hayo ya bajeti ya Sh. trilioni 33.1, serikali imeweka wazi kuwa ina mpango wa kurejesha VAT kwenye taulo za kike iliyoifuta mwaka jana kwa kuwa uamuzi wake huo haukufanikiwa kupunguza bei ya bidhaa hiyo muhimu.

"Inawezekana kabisa serikali ikawa sawa, kwamba bei ya taulo za kike haikushuka kutokana na mapendekezo ambayo serikali iliyaleta, lakini serikali inapaswa itafakari, je, mwaka mmoja ambao utekelezaji umefanyika unatosha kuweza kupima matokeo ya sera ile ambayo iliyafanya mwaka jana?" Zitto alihoji.

"Ukurasa wa 38 wa hotuba ya Waziri wa Fedha (Dk. Philip Mpango), anasema pendekezo lile halijawezesha kupatikana kwa bidhaa hiyo muhimu kwa bei nafuu na hasa kwa walengwa na badala yake pendekezo lile limefaidisha wafanyabiashara."

Alisema anaikumbusha serikali kwamba mwaka jana, ilitoa pendekezo la kuongeza kodi kwenye mafuta ghafi yanayotoka nje ya nchi ili kulinda wazalishaji wa mbegu za mafuta nchini, lakini uamuzi huo haujawa na matokeo chanya.

Zitto alisema: "Nataka Bunge lako tukufu Mheshimiwa Naibu Spika, tutazame nini matokeo ya pendekezo lile ambalo serikali ililileta. Mwaka 2017, kabla ya kodi zile kupandishwa, tulikuwa tunalinda uzalishaji wa mazao ya mafuta.

"Tulikuwa tunazalisha tani milioni 6.6 mwaka 2017 kabla ya kupandisha kodi ili kudhibiti uagizaji wa mafuta kutoka nje, mwaka 2018, Mheshimiwa Naibu Spika, tumezalisha tani milioni 1.6.

"Yaani pendekezo ambalo serikali imelileta mwaka jana, matokeo yake hayakuzalisha tegemeo la uzalishaji wa mbegu kuongezeka," Zitto alisema na kuongeza kuwa anashangaa kuona serikali haijaja na pendekezo la kufuta pendekezo lake ambalo halijawa na matokeo mazuri.

Kwa kutumia mfano huo, Zitto alisema haiwezekani pendekezo la kikodi likazaa matunda ndani ya mwaka mmoja.

"Kodi imeanza Julai 2018, kuna watu walikuwa na bidhaa ambazo wamenunua hazikuwa na punguzo hilo, lazima watauza kwa bei ileile, pia fedha yetu imeporomoka thamani dhidi ya Dola ya Marekani na taulo hizi nyingi tunaagiza kutoka nje, je, tumetazama hili?"

"Serikali itazame vizuri na kutoa muda wa kutosha kama ilivyofanya katika mafuta. Mwaka jana, suala la taulo za kike tulikuwa mfano na India, Afrika Kusini na Australia, wametuiga?" Zitto alihoji.

Katika mjadala huo, Mbunge wa Bukoba Mjini, Willfred Lwakatare (Chadema), alimtaka Waziri Mpango, Dk. Philip Mpango kueleza ni maajabu atayaotumia kukusanya fedha zilizokadiriwa katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha.

Aliliambia Bunge kuwa katika miaka yote ambayo amekuwa bungeni, hajawahi kuona wabunge wa CCM wanasema kuwa bajeti ni mbaya, bali wamekuwa wakisema ni ya wanyonge.

Mbunge huyo pia alihoji uwezo wa wataalamu wanaotengeneza bajeti nchini na kushauri wataalamu nchini wajaribu kufanya utafiti ili kubaini tatizo la msingi liliko.

"Tujaribu kuona kwanini miaka hadi miaka, tunatengeneza bajeti lakini haziondoi umasikini wa watu wetu. Tuna masikio, tuna macho, tunasikia, tunaona," Lwakatare alisema.

Lwakatare ambaye pia aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Chadema, alisema katika bajeti ya mwaka huu, Mamlaka ya Mapato (TRA) ilitembea na wawakilishi wa vyombo vya dola kwenda kudai fedha pamoja na kuanzisha vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo, lakini imefanikiwa kukusanya wastani wa Sh. trilioni 1.2 kwa mwezi.

Habari Kubwa