Zitto ambana Lugola ubakaji wajane

22May 2019
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Zitto ambana Lugola ubakaji wajane

BUNGE limemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, kwenda Kigoma kutatua changamoto ya ubakaji na ukatili dhidi ya wanawake, hasa wajane inayodaiwa kushika kasi katika mkoa huo.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe.

Agizo hilo lilitolewa bungeni jijini Dodoma jana na Mwenyekiti wa Bunge, Najima Murtaza Giga, baada ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), kumbana waziri huyo kuhusu kutochukua hatua dhidi ya wanaofanya ukatili dhidi ya wanawake mkoani Kigoma.

Akiwasilisha hoja bungeni jana asubuhi, Zitto alihoji sababu za kile alichokiita kufumbia macho vitendo viovu vya uhalifu licha ya kuwa wizara kupokea taarifa kutoka kwa viongozi na wananchi.

Hata hivyo, Lugola alizitishia taasisi zisizokuwa za kiserikali zinazofanya utafiti wa masuala ya ukatili na kuonyesha viashiria vya uchochezi kuwa zitachukuliwa hatua kali za kisheria na kwamba serikali inaendelea kuzifuatilia.

Zitto alisema utafiti uliofanywa na taasisi zisizokuwa za kiserikali, umebaini kuwapo kwa vitendo vya unyanyasaji, huku serikali ikiwa imefumba macho kwa kutochukua hatua zozote za haraka na za kisheria.

Zitto alisema katika jimbo lake la Kigoma Mjini, kwa takribani miaka mitatu sasa kumezuka tabia ya vijana kujipata oil chafu na kuvamia wanawake, hasa wajane na wanawake ambao wenza wao hawaishi nao, na kuwabaka na wakati mwingine hata kuwajeruhi kwa kipigo.

Alisema usiku wa kuamkia juzi, mama mmoja alijeruhiwa kwa kupigwa nondo kichwani na mmoja wa vijana na mwingine amechomwa kisu na wote wako hospitalini.

Zitto alibainisha kuwa shirika lisilokuwa la kiserikali la Tamasha, limefanya utafiti wa matukio hayo na tangu mwaka 2016, limebaini matukio 43 ya aina hiyo yametokea Kigoma na limemwandikia barua waziri, mbunge na taasisi mbalimbali zisizokuwa za kiserikali, likiomba vikao ili kuangalia namna ya kutatua changamoto hiyo.

“Kwa hiyo, nimelileta hapa bungeni ambacho ndicho chombo cha wananchi na tukio hili ni tukio la aibu kwa kweli na mimi kama Mbunge wa Kigoma Mjini, najisikia vibaya, najisikia aibu na linanisononesha, inanisikitisha na ninaona aibu sana.

"Kwamba tunaweza tukashindwa kulinda kinamama, dada zetu, shangazi zetu, watoto wetu kufanyiwa vitendo vya kinyama ambavyo wanaendelea kufanyiwa.

Kwa hiyo, naomba kiti, nisingependa niombe mjadala kwa kuwa ni jambo ambalo ndio kwanza nimelileta na watu hawatakuwa na takwimu za kutosha ili kujadili.

“Lakini, naomba kiti kiielekeze serikali ilete ndani ya Bunge taarifa ni ya aina gani hatua ambazo wamezichukua mpaka sasa za kukabiliana na hali hii kukomesha vitendo hivi na kuchukua hatua kali za kisheria kwa watu wote ambao wanadhalilisha, kuumiza na kunyanyasa wanawake hata katika Kata ya Mwanga Kusini na Kata ya Kasibuba katika Halmashauri ya Kigoma Mjini," Zitto aliwasilisha.

Kutokana na hoja hiyo, Giga aliitaka serikali kutoa taarifa kuhusu matukio hayo.

Baada ya agizo hilo, Waziri Lugola alisimama na kusema: "Mheshimiwa Mwenyekiti, ubakaji ni kosa la jinai, vitendo hivi vya makosa ya namna hii vimekuwa vikitokea katika nchi yetu na siyo Kigoma tu, bali katika maeneo mbalimbali.

"Makosa haya huwa yanadhibitiwa na Jeshi la Polisi na watuhumiwa wanapopatikana na ushahidi, wanafikishwa mahakamani na kuwajibika.

“Lakini, Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende pia kusema bayana kwamba kwa Mkoa wa Kigoma matukio ambayo Mheshimiwa Zitto Kabwe ameyazungumzia ni matukio ambayo ni kweli yanawadhalilisha kinamama, vitendo ambavyo sisi kama serikali hatuwezi kuvipa nafasi na kuvivumilia.

"Na niseme bayana kuwa vilianzia 2014, Mheshimiwa Mwenyekiti, kinamama wa Kigoma ambao ni wajane au wasiokuwa na wanaume au waume zao wamesafiri, walikuwa wanakuta mtu ambaye haonekani kwa macho na mwanamama anajikuta sehemu zake za siri zimeloa halafu anaponyanyuka anaona kama mtu, anapotaka kumshika yule mtu, anateleza.

"Ndipo dhana ya udhalilishaji kwa mtindo wa teleza ilipoanzia na ikaonekana walikuwa wanaingilia kwenye pembe ya nyumba au kwenye kona.

“Lakini Mheshimiwa Mwenyekiti, vitendo hivi vimeendelea kudhibitiwa na nilipopata barua hii na kushirikiana na Mheshimiwa Zitto Kabwe pamoja na Mkurugenzi wa Twaweza, Aidani Eyakuze, nilitoa maelekezo kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma.

“Lakini mwenyekiti jambo hili si la ukubwa huo kama inavyoelezwa na hizi taasisi zisizokuwa za kiserikali zinazotoa huu utafiti ambao Mheshimiwa Zitto Kabwe anausema, na tukiangalia kwenye kumbukumbu zetu kwenye vitabu vya polisi, mpaka jana katika mwaka huu hakuna taarifa yoyote ambayo inahusisha tukio la ubakaji.

“Ninachokisema mimi kama Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, sina taarifa yoyote na kama kuna taarifa, nipo tayari kuondoka hata sasa kwenda Kigoma ili kuona kama kuna ukubwa wa taarifa ambayo imetolewa hapa bungeni, sina sababu ya mimi ya kusema uongo."

Hata hivyo, Giga alimtaka Waziri Lugola kwenda Kigoma kushughulikia changamoto hiyo, akieleza kuwa vitendo vya unyanyasaji havipaswi kufumbiwa macho.

Habari Kubwa