Zitto amkaribisha Membe upinzani

01Jul 2020
Na Mwandishi Wetu
Kilwa
Nipashe
Zitto amkaribisha Membe upinzani

KIONGOZI wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema sasa ni wakati mwafaka kwa Benard Membe kujiunga na vyama vya upinzani.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kilwa mkoani Lindi jana, Zitto alisema mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa mbunge na waziri wa wizara nyeti nchini, ana fursa ya kuunganisha Watanzania wenye kiu ya mabadiliko kupitia vyama mbadala vya siasa.

"Ndugu yangu Benard Membe kafukuzwa uanachama wa CCM. Ninajua bado anatetea haki yake ya uanachama huko. Ni hatua sahihi.

"Hata hivyo, muda wa kuleta mabadiliko katika nchi umewadia, ninamsihi afanye uamuzi wa kuunganisha nguvu kupitia vyama mbadala, ili kuwapa Watanzania mabadiliko wanayoyataka," alisema.

Zitto ambaye yuko katika ziara ya kichama ya mikutano ya ndani Kusini mwa Tanzania, alisema anaelewa mwanasiasa huyo bado anapambana kubaki ndani ya CCM, lakini muda huu anahitajika zaidi upinzani.

Membe, mmoja wa wanasiasa mashuhuri nchini, alifukuzwa uanachama wake CCM miezi michache iliyopita na hali yake kwa sasa iko kwenye sintofahamu.

Wiki iliyopita, Membe alikaririwa akisema kuwa, ingawa kwa sasa bado anaangalia hatma yake ndani ya CCM, upo uwezekano wa kuwania urais kupitia vyama vingine mbadala.

Hata hivyo, katika mkutano huo wa Kilwa, Zitto alisema historia itamhukumu vibaya mwanasiasa huyo endapo hatafanya uamuzi wa kujiunga na upinzani kwa sasa.

"Mimi ninajua Membe anaipenda Tanzania na ni mwana demokrasia. Adhihirishe mapenzi yake kwa nchi yetu kwa kuongeza nguvu wa vyama mbadala.

"Kama kuna kosa la uhaini, basi itakuwa ni kwa Membe kutofanya uamuzi wa kuwatumikia Watanzania nje ya CCM. Ninamsihi kuwa afanye tafakari na kufanya uamuzi sahihi na wananchi," alisema Zitto huku akishangiliwa na umati uliohudhuria mkutano huo.

Habari Kubwa