Zitto amshtaki Spika Jumuiya ya Madola

11Jan 2019
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe
Zitto amshtaki Spika Jumuiya ya Madola

KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amemwandikia barua Katibu Mkuu wa Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA) kumwomba kuingilia kati uamuzi uliochukuliwa na Spika Job Ndugai wa kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, kufika mbele ya ......

KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, picha mtandao

Kamati ya Maadili, Kinga na Haki ya Bunge kuhojiwa.

Pia amewatumia barua hiyo Spika wa mabunge yote ya Afrika kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola, Wadhibiti na Wakaguzi Wakuu wa Hesabu za Serikali wa Afrika katika nchi za Jumuiya ya Madola pamoja na Spika wa nchi za Jumuiya ya Nchi Kusini mwa Afrika (SADC).

Hatua hiyo imekuja baada ya Spika Ndugai kumtaka CAG, Prof. Assad kufika mbele ya kamati hiyo Januari 21, mwaka huu, kujieleza kuhusu kauli yake aliyoitoa akiwa nchini Marekani kuwa ‘Bunge ni dhaifu’.

Akiwa nchini humo, CAG alihojiwa na chombo cha habari cha Idhaa ya Amerika kuhusu ripoti za ukaguzi ambazo zimekuwa zikifanywa na ofisi hiyo, lakini hazifanyiwi kazi pamoja na kuonyesha ubadhirifu.

Kwenye maelezo yake, Prof. Assad alisema hilo ni jambo ambalo kimsingi ni kazi ya Bunge.

“Kama tunatoa ripoti inayoonyesha ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu mimi ni udhaifu wa Bunge, Bunge linatakiwa lisimamie na lihakikishe kwamba kwenye matatizo hatua zinachukuliwa,” alisema.

Kutokana na kauli hiyo, Spika Ndugai, aliagiza CAG Assad afike mbele ya Kamati hiyo ili kujieleza kwanini anaudhalilisha mhimili huo.

Kwenye barua hiyo aliyoisambaza kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, Zitto alieleza kuwa amewaomba viongozi hao waongee na Spika Ndugai ili aachane na uamuzi wake wa kumwita CAG kuhojiwa na Kamati ya Bunge.

Sehemu ya barua hiyo aliyomwandikia Katibu Mkuu wa CPA, Akbar Khan ilieleza.  

“Kwa kuwa Bunge la Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Madola, naiomba ofisi yako ifanye mawasiliano ya kidiplomasia kwa kuwasiliana na Spika wa Bunge la Tanzania kumweleza hatari ya maamuzi anayotaka kuyachukua,” alisema na kuongeza:

“Ninaamini suala hilo linaweza kumalizwa kwa ustaarabu na kuimarisha uhusiano kati ya taasisi hizo mbili, yaani Bunge la Tanzania na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambao wote wanategemeana katika ufanyazi kazi,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.

Hatua ya Spika Ndugai kumwita CAG Prof. Assad, kwenye kamati ya maadili kuhojiwa iliibua mjadala kwa wadau mbalimbali.
Aliyewahi kuwa CAG, Ludovick Utouh, alisema pande hizo zinapaswa kuelewana kiutendaji ili zifanye kazi vizuri.

Naye, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume, alisema kanuni za Bunge zinampa mamlaka Spika kumwita mtu aliyezungumza suala linalohusu Bunge nje ya Bunge iwapo ameanzisha uchunguzi kuhusu suala hilo, lakini ni kwa ajili ya kutoa tu ushahidi katika kamati.

Naye wakili Albert Msando kwenye ukurasa wake wa Twitter, alipinga hatua ya Spika Ndugai kumwita CAG na kwenye andiko lake alisema:

“Unamwita CAG kwa Press Conference na kumtishia kwa pingu? Marehemu babu yangu aliwahi kunionya kwamba kufanya jambo kwa haraka ni kiashiria cha udhaifu.

“Alichosema CAG ni kwamba kazi ya ofisi yake ikishakamilika anakabidhi Bunge lichukue hatua. Anadhani Bunge halichukui hatua kwa sababu ni dhaifu.”

Habari Kubwa