Zitto ashtukia janja ya Spika

14Sep 2017
Joseph Mwendapole
Nipashe
Zitto ashtukia janja ya Spika

WAKATI Spika wa Bunge, Job Ndugai, akiagiza kwa mara ya pili jana Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, akamatwe na kuhojiwa kwa tuhuma za kuendelea kulidhalilisha Bunge, mbunge huyo amesema amegundua kiongozi huyo wa mhimili wa kutunga sheria ana agenda ya siri.

Zitto Kabwe.

Ndugai alitoa maagizo hayo jana asubuhi wakati akitoa matangazo mbalimbali, baada ya kumalizika kwa kipindi cha Maswali na Majibu.

Ndugai alilalamikia alichokiita hatua ya Zitto kuendelea kukashfu Bunge kwenye mitandao ya kijamii na kulinganisha ufanisi wa Bunge la Tisa, la 10 na la sasa.

Spika alisema ulinganishaji huo hauna msingi wowote kwa kuwa "kila zama na kitabu chake." Aliagiza akamatwe popote alipo na kufikishwa mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Juzi Spika aliagiza Zitto akamatwe na kufikishwa mbele ya kamati hiyo kwa tuhuma za kudhalilisha Bunge kupitia mitandao ya kijamii.

Zitto alikuwa, kupitia mitandao hiyo, amekosoa kitendo cha Ndugai kuomba kwa Rais John Magufuli ushauri wa uteuzi wa majina
ya wajumbe wa kamati maalum ya Bunge iliyochunguza uchimbaji na biashara ya madini ya almasi na Tanzanite.

Kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter jana, Zitto alisema amegundua amri ya kukamatwa kwake ina uhusiano na majeruhi wa risasi, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, aliyelazwa katika Hospitali ya Nairobi, Kenya.

"Nimegundua Spika ameibua mashtaka yangu, ili kufunika ufuatiliaji wa wananchi kuhusu Lissu kupigwa risasi," aliandika Zitto. "Nimeamua sitawapa hilo."

Lissu alinusurika kifo baada ya kupigwa risasi tano mwilini na miguuni, katika shambulizi la risasi dhidi yake Jumatano iliyopita, lililofanywa na watu wasiojulikana saa 7:30 mchana akiwa ndani ya gari lake, akiwa amefika nyumbani maeneo ya Area D, Manispaa ya Dodoma, baada ya kutoka kwenye kikao cha Bunge.

Miongoni mwa 'madongo' mapya ya Zitto kwenye mitandao ya kijamii tangu kutoka kwa amri ya kwanza ya kukamatwa kwake juzi ni tathmini kwamba Ndugai hajafikia hata asilimia 10 ya utendaji wa Spika wa Bunge lililopita, Anne Makinda.

Makinda alikuwa akilalamikiwa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa kupendelea wabunge wa upande wa chama tawala cha CCM na hoja za serikali.

“Kwenye mazishi ya Spika wa watu Mzee (Samuel) Sitta, Ndugai aliomba afike japo robo ya Sitta. Hajafika hata asilimia 10 ya Anne Makinda miaka miwili sasa," aliandika jana.

KASI NA VIWANGO
Sitta aliyefariki dunia Novemba 7, mwaka jana, alikuwa Spika wa Bunge kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2010 akisifiwa kuendesha chombo hicho kwa kasi na viwango na kuruhusu hoja nyingi za upinzani.

“Kwanza nimwambie yeye na wenzake wote wanaolinganisha Bunge hili na yaliyopita kuwa kila Bunge la miaka mitano huwa tofauti sana na Bunge lingine," alisema Ndugai.

"Sitaki kuchambua hapa, ila uwezo wa kuchambua ninao maana kote huko nilikuwapo.Itoshe tu kumwambia Zitto na wenzake kuwa Mheshimiwa Sitta na Makinda ni walimu wangu na hata siku moja sikio haliwezi kuzidi kichwa."

Sitta alikuwa Spika wa Bunge la tisa ambalo lilishuhudia aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, akijiuzulu kutokana na uchunguzi wa kashfa ya kampuni ya ufuaji umeme ya Richmond, ambayo iliibuliwa bungeni na upinzani.

Ndugai alisema Zitto anatakiwa katika Kamati ya Maadili, ili ahojiwe kwa kudhalilisha Bunge kutokana na maneno mengi ambayo amekuwa akiandika kwenye mitandao ya kijamiii.

Mbali na Zitto, Spika Ndugai juzi aliagiza kukamatwa popote alipo Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea, ili naye akahojiwe na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na ile ya Ulinzi na Usalama inayoongozwa na Mbunge wa Muheza (CCM), Adadi Rajabu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na madaraka ya Bunge, George Mkuchika, alipotafutwa jana kwa njia ya simu kuhusu maandalizi ya kikao cha kujadili wabunge hao, alijibu kwa kifupi kuwa yuko kwenye mkutano.

Habari Kubwa