Zitto awataka Mwinyi, Mkapa, JK wasikae kimya

09Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
KAHAMA
Nipashe
Zitto awataka Mwinyi, Mkapa, JK wasikae kimya

KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe, amewataka marais wastaafu kutokaa kimya, badala yake wajitokeze kumshauri Rais John Magufuli wanapoona mambo hayaendi sawa, ili kuinusuru nchi na uchumi.

Akizungumza mikutano ya kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Isagehe, wilayani Kahama, Zitto alisema:

“ Hii nchi inaongozwa kwa misngi ya kidemokrasi, nawaomba marais wataafu wasikae kimya kuhusu kuinusuru nchi yetu, wamshauri rais kuhusu mambo mbalimbali likiwamo la vyama vya siasa kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara.”

Marais wastaafu waliopo ni Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.

Aidha Zitto alimuomba Rais Magufuli kufanya mabadiliko katika sekta ya madini kwa kuweka wazi mikataba ya wawekezaji na kwamba jambo hilo litasaidia wananchi kuwa na uelewa mpana wa mikataba hiyo.

Katika hatua nyingine, Zitto alieleza kushangwaza kuona barabara inayounganisha migodi mitatu ya dhahabu ya Buzwagi, Bulyanhulu na Geita Gold Mine kuwa barabara hiyo haina kiwango cha lami tangu uongozi wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere wakati barabara hiyo imekuwa ikitumia kusafirisha dhahabu kupitia malori makubwa ambayo yanaharibu barabara hiyo.

“ Hii Barabara sisi ACT, Wazalendo tunaiita barabara ya unyonyaji, haiwezekani barabara inayopitisha madini inatoka Kahama kwenda Bulyanhulu hadi Geita, lakini hakuna hata chembe ya lami na wananchi mpo mnaendelea kushangilia chama tawala,” alisema Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini.

Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo wilayani Kahama, Iddsam Mapende, aliwataka wananchi wa Kata ya Isagehei kutofanya makosa katika uchaguzi mdogo badala yake wamchague diwani anayetokana na chama hicho, ili kuwapigania maendeleo katika Halmashauri ya Mji wa Kahama.

Naye mgombea Udiwani wa Kata ya Isagehe kupitia ACT- Wazalendo, Ibrahim Maziku, aliwataka wananchi kumwamini na kumpa kura nyingi kwani atahakikisha anashirikiana na chama chake ngazi ya taifa kupigania maendeleo yao na ya Halmashauri Nzima ya Mji wa Kahama.

Habari Kubwa