Zitto Kabwe ataka bei elekezi ya taulo za kike

17Jun 2019
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
Zitto Kabwe ataka bei elekezi ya taulo za kike

KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT –Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema serikali imeweka kodi katili kwa wanawake kwa kurejesha VAT kwa taulo za kike na mawigi na kuwa serikali ilipaswa kukaa na wafanyabiashara na kuweka bei elekezi ya taulo hizo badala ya kurejesha kodi katika vifaa hivyo.

KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT –Wazalendo, Zitto Kabwe,

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia chama hicho, ameifananisha hatua hiyo na kutoza kodi ya hedhi.

“Serikali ilipaswa kukaa na wafanyabiashara wa pads (taulo za kike) kuweka bei elekezi kwa sababu bei zinazowekwa kwa retail (rejareja), ni bei kubwa sana kutoka asilimia 30 hadi asilimia 40,” alisema Zitto.

Akizungumza na vyombo vya habari jana katika ofisi za makao makuu ya ACT-Wazalendo kuzungumzia bajeti ya mwaka 2019/20 iliyowasilishwa bungeni Alhamisi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, Zitto ambaye kitaaluma ni mchumi, alisema kuongeza kodi ya taulo za kike ni sawa na kuwaadhibu zaidi ya wanawake milioni 12 nchini ambao huingia katika siku zao kila mwezi.

Kiongozi huyo alisema serikali ilipaswa kufainyia utafiti biashara ya vifaa hivyo na kuangalia mfumo mzima wa usambazaji kabla ya kuja na mapendekezo ya kuongeza kodi kwa kuwa kufanya hivyo, bei ya taulo hizo inaweza kuongezeka zaidi.

“Inawezekana kabisa zikauzwa mpaka kwa ya Sh. 1,000 iwapo serikali itatazama mfumo mzima wa usambazaji,” Zitto alisema.

Ameishauri serikali kutenga eneo maalum (Special Economic Zone) kwa ajili ya viwanda vya uzalishaji wa taulo za kike mkoani Simiyu hasa kwa kuzingatia kuwa mkoa huo huzalisha pamba kwa wingi ambazo ndio hutumika katika kutengenezea hizo.

Akizungumzia Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2019/20, amesema bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ni bajeti ya vitu zaidi kuliko watu kwa kuwa miradi ya maendeleo inayowagusa wananchi wa kawaida imetengewa fedha kidogo na fedha nyingi kuelekezwa kwenye miradi ya vitu.

“Ni bajeti ya vitu, asilimia 55.7 ya bajeti yote ya maendeleo ni ya vitu… watu unawapata kwenye elimu, maji , afya, kilimo, uvuvi na mifugo,” alisema Zitto na kuendelea: “Kwa ujumla watu ni asilimia 17.3 yaani bajeti ya ndege ni bilioni 500 na afya bilioni 500.”

WAFANYABIASHARA

Akizungumzia sekta binafsi, kiongozi huyo alidai serikali imekuwa hairejeshi kodi ya VAT (TAX Refund) kwa wafanyabiashara, hivyo kuwafanya wafanyabiashara kushindwa kuzimudu biashara zao, ikiwamo kushindwa kulipa madeni waliyokopeshwa na kushindwa kulipa wafanyakazi wao.

WAFANYAKAZI

Kuhusu wafanyakazi, Zitto alilalamikia kodi katika mishahara ya wafanyakazi akidai ni eneo ambalo lilitakiwa kuangaliwa katika bajeti kwa kupunguza kodi katika mishahara yao sambamba na kupunguza michango inayolipwa na wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi za jamii.

Habari Kubwa