Zitto Kabwe aushtukia muswada wa Azaki

25Jun 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Zitto Kabwe aushtukia muswada wa Azaki

KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema muswada wa mabadiliko ya sheria mbalimbali unaotarajia kusomwa bungeni Jumatatu kama hati ya dharura, usipozuiliwa unakwenda kuua asasi zisizo za kiserikali (NGO).

KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Zitto, alidai kuwa kama muswada huo hautazuiliwa, wiki ijayo, inakwenda kuwa moja ya wiki nyeusi katika nchi.

“Wiki ijayo, Jumatatu kama hii tutaweka historia kwamba wastaafu wetu hawawezi kufanya shughuli zao, mtu kama Ludovick Utouh (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali-CAG), taasisi yake ya Wajibu ni ‘Company Ltd’ inakwenda kufa kwa sababu sheria inakwenda kuondoa tafsiri ya company Ltd, sheria ya kampuni ambayo ipo duniani kote,” alisema.

Zitto aliongeza: “Maana yake Mkapa, (Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa), Kikwete (Rais mstaafu wa Awamu ya Nne) wasiweze kufanya shughuli yoyote ya kijamii, kina Joseph Butiku (Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere - MNF) waende Butiama, wanataka Kituo cha Sheria cha Haki za Binadamu (LHRC), Twaweza, TGNP na mashirika mengine yafe.”

Alisema hiyo ndiyo hatari ambayo wanaiona ndani ya wiki ijayo mjini Dodoma kama muswada huo utawasilishwa bungeni.

Zitto alisema wito wao kwa serikali ni kuuondoa muswada huo bungeni kwa sababu unakwenda kuua biashara.

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini, alidai kuwa kwa kuonyesha muswada huo unahila, umepelekwa bungeni kama hati ya dharura ili usomwe mara ya kwanza, ya pili, ya tatu ndani ya siku tano.

“Leo (jana) wabunge wanamaliza kujadili bajeti, kesho (leo) tunaipigia kura, Jumatano tunakwenda kujadili Sheria ya Fedha, Alhamisi tunajadili mgao wa fedha, Ijumaa Bunge linaahirishwa, kwa hiyo sheria hii yenye kubadili sheria zote ambazo ni Sheria ya Kampuni, Sheria ya Bodi ya Wadhamini, NG’O na pia kuna mabadiliko mengine yanakuja ya Sheria ya Filamu ili kudhibiti,” alidai na kuendelea:

“Tunapitisha sheria za hatari, ambazo zitajadiliwa siku moja ili kuhakikisha kwamba wanapitisha kile ambacho wamekikusudia.”

Zitto alisema akiwa Mbunge na Kiongozi wa ACT-Wazalendo anatoa wito kwa serikali iachane nazo kwa sababu hazina maana yoyote.

“Sheria hizi zitazuia uhuru wa watu kufanya shughuli zao, kujumuika kwenye taasisi na kujiendesha kwa mujibu wa sheria, na pia ni sheria inayokwenda kuua biashara hasa kifungu cha 400 (a) cha sheria namba 10 kinachokwenda bungeni,” alidai.

Akizungumzia Sheria ya Takwimu alisema walilalamika, lakini hawakusikilizwa na nje nako walifanya hivyo, na sasa serikali inafanya marekebisho yake.

“Ni kweli sheria zinatungwa, zinapita kwa hati ya dharura kwa sababu ya wingi ya watu wa CCM ndani ya Bunge, lakini msukumo ukiwa mkubwa wanarudi bungeni, mfano mzuri ni Sheria ya Takwimu ambayo ipo hati ya dharura.”

Zitto alidai wanahitaji Watanzania wote kuunganika kwa sababu zimekuwa zikija sheria za kuwashughulikia mmoja mmoja kwa kuwa hawaunganiki zinapita kirahisi.

“Sheria ya vyombo vya habari ilivyokuja, tulisema inawahusu waandishi, baadhi tulisema wakasema wewe siyo mwandishi inakuhusu nini, hata waandishi walitushangaa wakasema wanasiasa tunawaingilia, Sheria ya Vyama vya Siasa ilivyokuja hivyo hivyo tukasema wanasiasa wenyewe na sasa wanashughulikia NGO,” alisema.

Alisema ni wakati mwafaka wa Watanzania kuungana kwa pamoja kupinga, wasione zinahusu NGO peke yao.

MADAI YA KUTUMIKA

Kuhusu kutumika, Zitto alisema anaona ni viroja na vichekesho, na kwamba wataendelea kuelimisha na kuueleza umma ukweli.

“Kuingia kwenye malumbano kati yangu na Katibu Mkuu wa CCM, Bashiru Ally, nashangazwa sana nimeingia chuoni (UDSM) 1999 nimemkuta yupo mwaka wa tatu na alikuwa amegombea urais Daruso (Chama cha Wanafunzi) akawa ameshindwa, akawa rafiki yangu ninamuona kama ndugu zaidi ya rafiki,” alisema.

Zitto alisema Dk. Bashiru anayemjua yeye ni mtu anayejadili hoja, masuala, siyo anayejadili nani anavaa nini, analishwa nini au analishwa na nani.

Zitto alimtaka Dk. Bashiru arudi kwenye kujadili hoja.

Habari Kubwa