Zitto kuanika majibu ya Madola

13Jan 2019
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Zitto kuanika majibu ya Madola

MBUNGE wa Kigoma Mjini, (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, ameahidi kuwa leo ataweka hadharani majibu aliyopatiwa baada ya kuandika barua kwa Katibu Mkuu wa Chama cha  Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA).

MBUNGE wa Kigoma Mjini, (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, picha mtandao

Zitto aliandika barua hiyo akipinga hatua iliyochukuliwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad kufika mbele ya Kamati ya Maadili ya, Kinga na Haki ya Bunge kuhojiwa.

Zitto aliliambia Nipashe jana kuwa tayari ameshajibiwa barua yake na leo atakuwa na mkutano na waandishi wa habari na ataanika yote aliyojibiwa.

Mbunge huyo na Kiongozi Mkuu wa ACT- Wazalendo, aliwatumia barua hiyo maspika wa mabunge yote ya Afrika kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola, Wadhibiti na Wakaguzi Wakuu wa Hesabu za Serikali wa Afrika katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola pamoja na wale   wa nchi za Jumuiya ya Nchi Kusini mwa Afrika (SADC).

Hatua hiyo imekuja baada ya Spika Ndugai kumtaka Prof. Assad kufika mbele ya kamati hiyo Januari 21, mwaka huu, kujieleza kuhusu kauli yake aliyoitoa akiwa nchini Marekani kuwa ‘Bunge ni dhaifu’.

Kwenye barua hiyo aliyoisambaza kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, Zitto alieleza kuwa amewaomba viongozi hao waongee na Spika Ndugai ili aachane na uamuzi wake wa kumwita CAG kuhojiwa na Kamati ya Bunge.

Sehemu ya barua hiyo aliyomwandikia Katibu Mkuu wa CPA, Akbar Khan, ilieleza:  

“Kwa kuwa Bunge la Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Madola, naiomba ofisi yako ifanye mawasiliano ya kidiplomasia kwa kuwasiliana na Spika wa Bunge la Tanzania kumweleza hatari ya uamuzi anaotaka kuuchukua,” alisema na kuongeza:

“Ninaamini suala hilo linaweza kumalizwa kwa ustaarabu na kuimarisha uhusiano kati ya taasisi hizo mbili, yaani Bunge la Tanzania na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambao wote wanategemeana katika ufanyaji kazi,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.

Habari Kubwa