Zitto kutinga Takukuru na ushahidi wa rushwa

06Dec 2018
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe
Zitto kutinga Takukuru na ushahidi wa rushwa

KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, kesho anatarajia kuitikia wito wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuhusiana na mambo aliyoandika kwenye mitandao ya kijamii.

KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, picha na mtandao

Takukuru kupitia Naibu Mkurugenzi Mkuu wake, Brigedia Jenerali John Mbungo, ilimtaka kiongozi huyo kufika ofisini kwake kutoa ushahidi wa tuhuma alizozitoa kuwa kuna kampuni tatu za chuma zimewahonga baadhi ya viongozi wa serikali.

Sehemu ya taarifa ya wito huo ilieleza kuwa: “Tunatoa taarifa hii kupitia vyombo vya habari kumwomba Zitto Kabwe afike ofisi za Takukuru Dar es Salaam mapema iwezekanavyo ili tushirikiane katika kulishughulikia suala hili muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa letu.”
 
Nipashe ilimtafuta Afisa Habari na Uhusiano wa Takukuru, Doreen Kapwani, kufahamu kama wamempangia siku maalum Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini kuripoti au amesharipoti naye alisema: “Atakuja tu kuripoti, kwa kuwa ameshaandika kwenye mitandao kuwa atakuja, basi lazima atakuja:”

Alipotafutwa Afisa Habari wa ACT-Wazalendo, Abdallah Khamis, kueleza ni lini kiongozi huyo atakwenda kuripoti Takukuru, alisema Zitto ataripoti Takukuru Ijumaa (kesho).

Kwenye mitandao ya kijamii Zitto alidaiwa kuandika kuwa amepata habari za kushtusha  kuwa kampuni tatu za China, Russia na Uturuki zimewahonga baadhi ya watendaji wa serikali kuchelewesha mradi wa Mchuchuma na Liganga. Lengo ni kuhakikisha nchi hizo zinapata soko la chuma chao.

Aliendelea kuandika kuwa kuhujumu mradi wa Mchuchuma na Liganga ni uhaini. Baadhi hawawezi kusahau hujuma hiyo na yeyote anayeshiriki atasakwa mpaka kaburini kwake, ikibidi kuondoa kinga za watu ili liwe fundisho  kwa uhujumu huu uchumi na uhai wa taifa letu.

Aliandika zaidi kuwa msamaha wa kodi kwa bomba la mafuta kutoka Uganda ni mkubwa na hauna faida kulinganisha na mradi wa Mchuchuma na Liganga utakaotoa ajira za kudumu 35,000 kuingiza fedha za kigeni bilioni 4.6 kwa mwaka na kuifanya nchi  yetu kuwa na viwanda vikubwa.

Zitto aliendelea kueleza katika ukurasa huo kuwa yote hayo yanafanywa chini ya uangalizi wa Rais Magufuli kiasi kwamba amelishwa matango pori dhidi ya mradi huo. Nchi yetu imegeuzwa dampo la kuagiza bidhaa za chuma kihayawani.

Aliandika kuwa watendaji hao kutoka Wizara ya Fedha, Viwanda na Biashara na Ofisi ya Rais wamekula njama kiasi cha kuwezesha Bunge kutunga sheria kuondoa kodi zote kwa mataruma ya reli yanayoagizwa kutoka nje na kuzuia mradi wa Mchuchuma na Liganga kupata msamaha wa kodi kuwezesha mradi kuanza.

 
 
 
 

Habari Kubwa