Zuio la RC matangazo ya misiba lazua jambo

25Feb 2021
Nebart Msokwa
MBEYA
Nipashe
Zuio la RC matangazo ya misiba lazua jambo

BAADA ya kuanza kutekelezwa kwa marufuku ya magari ya matangazo kutangaza misiba barabarani iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila hivi karibuni, umoja wa wamiliki wa magari ya matangazo na washereheshaji umeibuka na kudai kuwa haukushirikishwa kuhusu hatua hiyo.

Katibu wa Umoja huo, Emmanuel Abel, alisema jana kuwa katazo hilo liliwashtusha na wanakusudia kufanya mkutano kujadiliana namna ya kufanya maridhiano na serikali ili ikiwezekana shughuli hiyo iendelee kufanyika.

Aliwataka wanachama wa umoja huo kuendelea kuwa watulivu na wasiifanye shughuli hiyo wakati wakisubiri majadiliano ambayo yataleta mwafaka.

"Hii kazi ni miongoni mwa ajira ambazo tumeamua kujiajiri. Tumekuwa tukijiingizia kipato na hata halmashauri imekuwa ikiingiza mapato kwa sababu kila tunapotaka kutangaza, tunalipia Sh. 50,000 ili tupewe kibali cha kutangaza," alisema Abel.

Hezron Mwanditili, mmoja wa wamiliki wa magari hayo ya matangazo, alisema wamekuwa wakiajiri watu wengi kwenye shughuli hizo ikiwamo madereva, watu wa mziki na washereheshaji na hivyo kukataza ni kuua ajira za watu.

Alisema shughuli hiyo ni miongoni mwa shughuli za kijamii na hivyo wananchi wamekuwa wakizitegemea kuendesha maisha yao kwa kutumia shughuli hizo.

Alisema hawaelewi sababu hasa ya kukataza matangazo hayo kwa maelezo kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakiyakodi magari hayo na washereheshaji ili kujifariji baada ya kufiwa na ndugu zao.

"Hatuelewi sababu hasa ya kukataza matangazo haya, yawezekana pengine wanadhani ndiyo yanayosababisha vifo vya watu kwenye jamii au yanawakera kwa sababu gani? Pengine wangetuelewesha, tungeelewa lakini hawakutuhusisha," Mwanditili alalamika.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Nipashe kuhusu katazo hilo, walibainisha kulifurahia wakidai matangazo hayo yalikuwa kero barabarani kiasi kwamba walikuwa wanayachukia.

Mmoja wa wananchi hao, Emmanuel Mwankapa, mkazi wa Ilolo jijini hapa, alisema kila siku walikuwa wanayasikia matangazo hayo barabarani, akidai yalikuwa yanakwamisha hata shughuli zao kwa kuacha kufanya kazi na kuanza kusikiliza kinachotangazwa.

"Tunamshukuru sana mkuu wa mkoa kwa kukataza matangazo haya. Ilikuwa ukikaa pale Soweto, kila muda ni matangazo hayo mpaka inakuwa kero. Ninaamini sasa hivi kelele zitapungua mjini," alisifu.

Februari 22, mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Chalamila, alipiga marufuku matangazo hayo huku akiwataka wahusika wayafanyie maeneo ya nyumbani inakokuwa misiba, kanisani na misikitini wanakofanyia ibada na makaburini.

Chalamila alitangaza katazo hilo kuanza kutekelezwa jana na kubainisha kuwa alikuwa amesambaza barua kwenye mamlaka mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa suala hilo.

Habari Kubwa