Zungu aagiza ufanyike uchunguzi mbegu za GMO

13Aug 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Zungu aagiza ufanyike uchunguzi mbegu za GMO

KAMATI ya Kitaifa ya Matumizi Salama ya Bioteknolojia ya Kisasa, imeagizwa kuchunguza na kuthibitisha mbegu za uhandisi jeni (GMO), zinazodaiwa kuwa na mkakati wa kuendeleza njaa barani Afrika.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mussa Zungu, alitoa agizo hilo jana alipokuwa akizindua kamati hiyo.

Kamati hiyo ina jukumu la kuishauri serikali mambo mbalimbali ikiwamo maombi ya matumizi ya viumbe na bidhaa zitokanazo na biotekinolojia ya kisasa na kuishauri kuhusu sera, sheria, utafiti na ushiriki wa sekta binafsi na umma kwa ujumla katika matumizi ya biotekinolojia ya kisasa.

Akizindua kamati hiyo, Waziri Zungu alisema “Kuna habari zinatembea ambazo hazijathibitika na inawezekana, kuna baadhi ya product (bidhaa) mpya ambazo zinaletwa nchini au Afrika zina mkakati mrefu wa kuendeleza njaa barani Afrika.”

Alisema kamati hiyo ina jukumu la kuchunguza na kuthibitisha GMO hizo kama kweli zinafaa ndani ya nchi bila madhara yoyote.

Alibainisha kuwa vita kubwa duniani inakuja na sera ni chakula na maji vikikosekana vitu hivyo taifa litaangamia.

“Lakini tunaamini majukumu na uzalendo mliopewa mtasimamia vizuri tafiti zenu na mtashauri vizuri serikali ili tujue ni njia ipi sahihi ambayo Tanzania itaitumia,” alisema.

Zungu alisema kwa kawaida tafiti hizo zilishafanywa muda mrefu, lakini hazifanyiwi kazi zinakaa chini ya meza, huku taifa linaangamia licha ya tafiti kufanyika.

“Miaka ya nyuma Mpango wa Maendeleo wa Tanzania haukutumika vizuri, lakini ulitumika vizuri nchi za nje miaka 80 na miaka 90 Mipango wa maendeleo wa nchi yetu ilichukuliwa na nchi nyingine sisi wenyewe tuliiweka chini ya meza, lakini kwa awamu hii ya tano mabadiliko mmeyaona,” alisema.

Hata hivyo, alisema serikali imeandaa na kuweka nyenzo mbalimbali za usimamizi wa teknolojia hiyo ikiwamo Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, Mpango wa Kitaifa wa Usimamizi wa Matumizi Salama ya Bioteknolojia ya Kisasa 2007.

Pia alisema kanuni za matumizi salama ya bioteknolojia ya kisasa ya mwaka 2009 na marekebisho yake ya mwaka 2015, miongozo mbalimbali za mwaka 2010.

Alisema hadi sasa usimamizi wake umewezesha kufanyika kwa utafiti ndani ya maabara wa mihogo unaolenga kupata ukinzani dhidi ya magonjwa ya virusi vya zao hilo.

“Pamoja na hatua hizi, bado kuna changamoto mbalimbali zinazokabili eneo hili ikiwa ni pamoja na uelewa mdogo miongoni mwa jamii kuhusu biotekinolojia ya kisasa, uchache wa wataalam wa masuala ya biotekinolojia ya kisasa na usimamizi wake,” alisema.

Habari Kubwa