Haki pekee ndio mwarobaini wa amani ya Bunge

25Jan 2016
Mhariri
Sema Usikike
Haki pekee ndio mwarobaini wa amani ya Bunge

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaanza vikao vyake Mjini Dodoma wiki hii.

Bungeni Dodoma

Katika mazingira ya kawaida tunaweza kusema bunge hili ni ‘jipya’ kutokana na ukweli kwamba ndio kwanza linaanza majukumu yake, lakini ki uhalisia ni kwamba mabadiliko ni machache sana.
Tunasema ni machache kwa vile kwa utamaduni wa nchi yetu, wabunge hutokana na vyama vya siasa. Hivyo pamoja na kwamba sura nyingi ni mpya, lakini sera, falsafa na itikadi tunaweza kusema ni zilezile.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba Bunge lililopita lilijaa wabunge wa CCM na wale wa CUF na Chadema. Na kama inavyojulikana ni kwamba vyama hivyo ndio vimepeleka wabunge wengi.
Tumejaribu kuyakumbushia haya kwa vile tunaamini mtu yoyote hawezi kuzungumzia mwanzo wa bunge la 11 bila kuzungumzia mwisho wa bunge la 10.
Katika bunge hilo la kumi, kuna mambo kadhaa yaliyojiri, yakiwemo mipasho, zomeazomea na hata mapigano!
Chanzo cha yote hayo kilidaiwa kuwa ni viongozi wa vikao (Kiti) kupendelea wabunge wa Chama tawala CCM na kuwakandamiza wale wa upinzani.
Kama tulivyokwisha sema kuwa wabunge ni wa vyama vilevile, kwa bahati mbaya dalili ya mambo ya fujo zimejitokeza katika ufunguzi wa bunge hili la 11.
Hivyo japokuwa mambo haya yanaonekana makubwa na kuchukua nafasi katika mijadala mbalimbali, sisi tunaona kwamba hayana ukubwa wa kiwango hicho kwani dawa yake ni ndogo.
Dawa yenyewe ni moja, kwamba pande zote zitambuane na kuheshimiana.
Kama ambavyo wenyewe wanadai ni kwamba wapinzani wanasema Spika anapendelea CCM, lakini Spika na viongozi wenzake nao wanadai kuwa wapinzani wanadharau kiti.
Hivyo basi kama Spika anataka kuheshimiwa, ni vema akatambua haki ya wapinzani hao kwamba wamefika hapo walipo kwa mujibu wa Katiba, hivyo wana haki sawa na wale wa Chama tawala CCM. Hatua yoyote ya kuwaona wabunge wa Chama chake ni bora kuliko wa upinzani, au kudhani hoja zao ndizo zenye kubeba agenda ya Watanzania ni kukaribisha vurugu.
Vilevile wabunge wa upinzani wanapaswa kutambua mamlaka ya Spika yanatokana na Kanuni zao na kwamba yupo kitini kwa mujibu wa Katiba ya nchi.
Hivyo basi hatua ya kudharau mamlaka yake, kwa vile tu anatoka Chama tawala ambacho wana malengo ya kuking’oa kwa udi na uvumba, haitawaacha salama na wala malengo yao hayatatimia kirahisi.
Hivyo ni ombi letu kwa pande zote mbili kutambuana na kuheshimiana.
Ni jambo lisilokubalina na lisilo la kusheria, wabunge kutumia muda mwingi kutatua migogoro inayotokana na mitafaruku yao ya kivyama inayoanzia nje ya bunge na kisha kuingizwa kwenye chombo hicho cha wananchi kwa mlango wa nyuma.
Wabunge wote wanapaswa kutambua kwamba bunge si chombo chao hivyo hawapaswi kulitumia kwa lengo la kujinufaisha wao wenyewe wala vyama vyao, bali wananchi waliowachagua.
Hivyo basi nimatumaini yetu kwamba watakuwa na jitihada za kujenga utaifa na uzalendo bungeni na kuweka mfukoni itikadi za vyama vyao na manufaa yao. Na Katika hili tunavisihi vyama vya siasa kuwafungua minyororo ya kiitikadi hao wabunge wao, ili waweze kutekeleza majukumu yao wakiwa huru.
Kama vyama vya siasa vina agenda zao za kisiasa, hiyo sio dhambi kwani ni haki yao, lakini wanapaswa kuziwasilisha moja kwa moja kwa wananchi, na sio kupitia ukumbi wa bunge.

Habari Kubwa