Kamati ya Mapinduzi somo kwa TFF

18Jan 2016
Sanula Athanas
Nipashe
Kamati ya Mapinduzi somo kwa TFF
  • DONDOO MUHIMU: Mbaya zaidi, mchezaji wa timu zinazotajwa kuwa ndogo akifanya kosa, anaadhibiwa. Kosa hilohilo linapofanywa na timu zinazotajwa kubwa, TFF inasita kuchukua uamuzi. Tunalipeleka wapi soka la Tanzania?

MICHUANO ya 10 ya Kombe la Mapinduzi ilimalizika wiki iliyopita huku klabu ya URA ikitwaa ubingwa baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

URA imekuwa timu ya pili kutoka Ligi Kuu ya Uganda kushinda taji la michuano hiyo tangu ilipoanzishwa 2007 kuenzi Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika Januari 12, 1964.
Licha ya kushirikisha timu nane pekee, tano pungufu ya ilivyokuwa mwaka jana, michuano hiyo mwaka huu imeonyesha ushindani na msisimko mkubwa.
Hata hivyo, umakini wa kamati ya uendeshaji wa michuano hiyo unapaswa kuigwa na mamlaka za soka nchini.
Wakati Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) bado linasita kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wachezaji, makocha na waamuzi waliofanya makosa mbalimbali msimu huu, Kamati ya Mapinduzi ilichukua saa chache tu kumwadhibu kwa kumwondoa kwenye oridha ya marefa wa Kombe la Mapinduzi mwaka huu refa Dalila Jaffar aliyeboronga katika mechi ya Azam FC dhidi ya Mtibwa Sugar.
Refa huyo mwenye beji ya Shirikisho la Soka la KImataifa (Fifa) alikataa bao halali la dakika ya 88 lililofungwa kwa kichwa na kinda wa Mtibwa, Shiza Kichuya katika mechi hiyo ya kwanza ya Kundi B la Kombe la Mapinduzi iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Amaan visiwani humo.
Marefa wengi wanaochezesha Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu wameonyesha udhaifu mkubwa, lakini TFF iko kimya!
Imekuwa kawaida kumwona Juuko Murshid wa Simba akiwanasa vibao wachezaji wa timu pinzani, marefa na TFF wako kimya! Kelvin Yondani anatema mate dhidi ya mchezaji wa timu pinzani, shirikisho liko linaona sawa tu. Refa anakataa penalti halali, anaonya kwa kadi ya njano katika tukio ambalo adhabu yake ni kadi nyekundu, mamlaka ya soka nchini inamwangalia tu!
Mbaya zaidi, mchezaji wa timu zinazotajwa kuwa ndogo akifanya kosa, anaadhibiwa. Kosa hilohilo linapofanywa na timu zinazotajwa kubwa, TFF inasita kuchukua uamuzi. Tunalipeleka wapi soka la Tanzania?
Mathalani, Amissi Tambwe wa Yanga alifunguliwa mashtaka kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kutokana na kumvuta katikati ya miguu beki wa kati wa Simba kutoka Uganda (Juuko) wakati wa mechi ya watani wa jadi Machi 8 mwaka jana, lakini hadi leo unaposoma safu hii, hakuna shirikisho hilo lenye mamlaka ya juu ya soa nchini halijatoa adhabu dhidi ya mshambuliaji huyo.
Kadhalika, klabu ya Mbeya City ilimshtaki beki huyo wa Simba kutokana na kitendo chake cha kumpiga ngumi (bila mpira) mmoja wa wachezaji wa timu hiyo wakati wa mechi yao ya VPL kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya Oktoba 17 mwaka jana, lakini hadi leo hakuna hatua za kinidhamu zilizochukuliwa dhidi ya mhusika.
Ukimya huu wa TFF unaashiria aidha shirikisho hilo linaunga mkono vitendo hivyo vya utovu wa nidhamu au 'halina meno' ya kudhiabu timu zinazotajwa kuwa kubwa nchini.
Shime, Kamati ya Uendeshaji wa Kombe la Mapinduzi inastahili pongezi kwa kuchukua hatua za haraka dhidi ya marefa wanaoboronga. Utaratibu huu uigwe na TFF kwa manufaa ya soka la Tanzania.

Habari Kubwa