Mechi hiyo ya raundi ya tatu ilichezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro na kushuhudiwa kocha mkuu wa muda, Mganda Jackson Mayanja akianza na viungo wanne, Jonas Mkude, Said Ndemla, Joseph Kimwaga na Abdi Banda kupata ushindi wake wa tatu mfululizo tangu arithi mikoba ya Dylan Kerr.
Mabingwa mara 18 wa Tanzania Bara walilazimika kusubiri hadi dakika ya 77 kupata bao la kwanza, Kiiza alipounganisha kwa kuugusa kwa kisigino mpira wa krosi iliyomiminwa ndani ya boksi na Banda kutoka wingi ya kushoto kaskazini mwa Uwanja wa Jamhuri.
Ndemla aliyekuwa hatua mbili kutoka kwenye boksi la Bukinafaso, alitupia la pili kwa shuti kali la kimo cha mbuzi kwa mguu wa kulia katika dakika ya 90+2.
Wakati mashabiki wakiamini mechi hiyo ingemalizika kwa matokeo ya 2-0, Ndemla alikwatuliwa ndani ya boksi na Kiiza alimchambua kwa shuti la kimo cha panya kwa mguu wa kulia penalti iliyoamuliwa na refa Andrew Shamba katika dakika ya 90+4.
Kung'ara kwa Mganda huyo (25), kunazidi kuwaamiza mashabaki wa Yanga kwani mkali huyo wa mabao alitemwa na uongozi wa Jangwani Desemba 2014 akidaiwa kushuka kiwango, lakini sasa anakamata nafasi ya pili kwenye orodha ya wafumania nyavu hatari wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu akiwa na magoli 10, matatu nyuma ya kinara, Amissi Tambwe wa Yanga.
YANGA vs FRIENDS RANGERS
Vinara wa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga ambao tangu Desemba 12 walipotoka suluhu dhidi ya Mgambo Shooting jijini Tanga, wameshinda mechi tano mfululizo dhidi ya African Sports, Mbeya City, Stand United, Ndanda na Majimaji, wakifunga mabao 14 bila kuruhusu nyavu zao kutikiswa, wataanza kusaka taji la FA leo watakapochuana na Friends Rangers kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm amepanga kuwatumia wachezaji wa akiba katika katika mechi hiyo ya kwanza ya Kombe la Shirikisho ambayo bingwa wake ataiwakilisha Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika mwakani.