Kombe la FA litatue changamoto za usajili

25Jan 2016
Mhariri
Nipashe
Kombe la FA litatue changamoto za usajili

MICHUANO ya Kombe la FA iliingia raundi ya tatu mwishoni mwa wiki kusaka timu moja itakayoiwakilisha Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho barani Afrika mwakani.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeamua kuirejesha tena michuano hiyo baada ya kupata wadhamini.
Ikishirikisha jumla ya timu 64 za Ligi Daraja la Pili, Darala la Kwanza na Ligi Kuu, michuano hiyo imeonekana kuwa na ushindani mkubwa huku mechi zake zikionyesha moja kwa moja kwenye luninga.
Tukiwa wadau namba moja wa michezo nchini, Nipashe tunapongeza uamuzi wa kurejeshwa kwa michuano hiyo, tukiamini itakuwa na faida kubwa kwa timu shiriki na soka la Tanzania kwa ujumla.
Tunaamini kuwa Kombe la FA litaongeza idadi ya mechi ambazo wachezaji wa soka nchini watacheza kwa msimu, hivyo kuimarisha viwango vyao.
Nipashe tunaamini pia kuwa michuano hiyo itatua changamoto ya usajili hasa kwa klabu za Ligi Kuu ikiwa itatumika vizuri katika kusaka wachezaji wapya wenye vipaji.
Pia tunaamini michuano hiyo itatoa nafasi nzuri kwa wachezaji ambao hawapati nafasi kubwa kwenye vikosi vya timu za Ligi Kuu kuonyesha uwezo wao.
Lakini si lazima timu zote za Ligi Kuu zitumie wachezaji wa akiba kwenye mechi za Kombe la FA kutokana na ukweli kwamba michuano hiyo ndiyo itakayotoa mwakilishi wa Tanzania katika michuano ya kimataifa mwakani.
Tunafahamu kwamba klabu nyingi za soka nchini zinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa maskauti kwa ajili ya wachezaji kiasi cha kuziingiza kwenye gharama ya mamilioni ya shilingi zinaposajili wachezaji kutoka nje ya mipaka ya Tanzania.
Kombe la FA linaweza kutatua changamoto hii ikiwa makocha na wataalumu wa ufundi wa klabu za Ligi Kuu nchini watatumia fursa hii kusaka wachezaji wapya wa ligi za madaraja ya chini ambao bila shaka si wa gharama kubwa.
Ni imani yetu kuwa Tanzania ina vipaji vingi vya soka ambavyo havijaonekana kutokana na changamoto ya kuwa na maskauti wachache wa timu za madaraja ya juu.
Nipashe tunatoa rai kwa TFF na waamuzi kujikita kwenye misingi ya kanuni, taratibu na Sheria 17 za Soka kuhakikisha mechi za michuano hiyo zinachezwa kwa haki kwa timu zote shiriki kwa vile kinyume chake Kombre la FA halitakuwa na maana yoyote kwa soka la Tanzania.

Habari Kubwa