KUFURU : Messi hizi rekodi ni balaa

13Jan 2016
Lete Raha
KUFURU : Messi hizi rekodi ni balaa

LIONEL Messi anazidi kuandika upya historia ya soka. Kabla ya kuibuka kwa straika huyo Muargentina miaka 10 iliyopita, rekodi za soka zilikuwa zinagawanywa kwa magwiji kadhaa wa soka waliokuwa wakizishikilia. Lakini sasa ni ngumu sana kukuta rekodi iliyobaki kwa yeyote kati yao.

Lionel Messi

Hapakuwa na mchezaji aliyewahi kutwaa tuzo nne za Ballons d'Or kabla ya Messi, achilia mbali tuzo tano. Lakini akiwa na umri wa miaka 28 tu, nyota huyo wa Barcelona alitwaa tuzo yake ya tano mjini Zurich juzi na hata kama atashindwa kupata nyingine katika miaka michache ijayo, haitarajiwi apitwe hivi karibuni. Au asipitwe tena.
Na stori iko hivyohivyo katika rekodi zake nyingine kibao alizoweka. Muargentina huyo ana muda mrefu sana tangu aivuke rekodi ya zama zote ya kufunga magoli mengi zaidi kwa klabu ya Barcelona na sasa amefunga magoli mengi kuliko mwanasoka yeyote katika historia ya soka la Hispania pia. Na zaidi, anashikilia rekodi ya kufunga magoli mengi zaidi katika msimu mmoja wa La Liga (50) na katika michuano yote ya klabu Ulaya (73) kwa msimu mmoja na alikuwa wa kwanza kuivunja rekodi ya Raul ya kufunga magoli 71 katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, ingawa kwa sasa amezidiwa na Cristiano Ronaldo katika michuano hiyo ya klabu ya barani humo.
Kufikia sasa, yeye ndiye mchezaji aliyefunga magoli mengi zaidi katika Clasico kuliko mchezaji mwingine yeyote na ndiye mchezaji pekee aliyefunga 'hat-trick' mbili katika historia ya mpambano huo wa watani wa jadi wa Hispania.
Lakini si magoli tu. Messi aliipita rekodi ya Luis Figo ya kutoa pasi zilizozaa magoli mengi zaidi katika La Liga mwaka jana, na yeye pamoja na Andres Iniesta, ndiyo pekee waliotwaa makombe mengi (26) kwa Barca kuliko wachezaji wengine wote katika historia ya klabu hiyo.
Mataji yake manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya pia ndiyo rekodi ya juu zaidi, wakati Barcelona imekuwa ni klabu ya kwanza kutwaa mataji yote matatu makubwa katika msimu mmoja mara mbili wakiyafikia mafanikio yao ya msimu wa 2008-09 kwa mataji mengine matatu msimu uliopita wa 2014-15. Na wiki iliyopita tu, magoli mawili ya Messi dhidi ya Espanyol yalimfanya kuwa ametupia mabao katika michuano sita tofauti kwenye msimu mmoja kwa mara ya pili. Mchezaji mwenzake wa zamani wa Baeca, Pedro, alikuwa ndiyo mchezaji wa kwanza kufanya hivyo 2009, lakini Messi sasa ametisha zaidi kwa kumpita kwa mara moja zaidi yake.
Na orodha inaendelea. Na baada ya kushinda mataji sita 2009, Barca walimaliza msimu uliopita kwa kutwaa mataji matano wakilikosa moja tu la Spanish Supercopa, lakini walitwaa Kombe la Dunia la Klabu kabla ya Krismasi huku Messi akiongoza mauaji katika fainali dhidi ya River Plate, timu ambayo ilikaribia kumsajili utotoni.

NANI KAMPIGIA NANI
Kufuatia ushindi wa Messi wa tuzo ya tano ya 2015 Ballon d'Or, imebainishwa namna manahodha wa timu za taifa za nchi zao walivyopiga kura zao tatu kila mmoja katika kumchagua mshindi.
Kwa mujibu wa nyaraka zilizotolewa, Messi alimpigia kura Luis Suarez wakati Cristiano Ronaldo alimpigia kura Karim Benzema, wachezaji ambao wote walishindwa kuingia katika Top 3.
Messi ambaye alishinda tuzo hiyo akifuatiwa na Cristiano Ronaldo na Neymar, aliwapigia kura nyota wenzake wa Barcelona, Suarez, Neymar na Andres Iniesta, wakati Ronaldo aliwapigia Benzema, James Rodriguez na Gareth Bale.
Nyota wa England, Wayne Rooney, alimpigia kura Messi, akamweka straika wa Bayern, Thomas Muller, katika nafasi ya pili na nyota mwenzake wa zamani klabuni Manchester United, Ronaldo, katika nafasi ya tatu.
Kipa wa zamani wa Chelsea, Petr Cech, ambaye sasa anadakia Arsenal, alimchagua Messi katika nafasi ya kwanza, Lewandowski ya pili na nyota mwenzake wa zamani wa Chelsea, Eden Hazard, katika nafasi ya tatu.
Straika wa Bayern Munich, Robert Lewandowski na kiungo wa Manchester United, Bastian Schweinsteiger, wote walimpigia kura yao ya ushindi Manuel Neuer.
Nahodha wa Wales, Ashley Williams wa Swansea City, alimpigia mtu wa taifa lake, Gareth Bale, huku nafasi ya pili akimuweka Messi na wa tatu Lewandowski.
Zlatan Ibrahimovic na Hugo Lloris, wao ndiyo waliotisha, kwani kura zao tatu zilienda kama washindi walivyopatikana, Messi namba moja, Ronaldo mbili na Neymar wa tatu.

WASIFU
Jina: Lionel Messi
Mechi: 503
Magoli: 430
Pasi za mabao: 162
Makombe: 26
Ballon d'Or: 5

Habari Kubwa