Machinjio Vingunguti, Pugu wapuuza agizo la Waziri

17Jan 2016
Nipashe Jumapili
Machinjio Vingunguti, Pugu wapuuza agizo la Waziri

KATIKA hali ya kushangaza, baadhi ya maofisa wa serikali wanaosimamia shughuli za kila siku katika machinjio ya Vingunguti jijini Dar es Salaam, wamezikimbia ofisi baada ya mwandishi wa gazeti hili kufika kazini kwao.

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Simbachawene

Nipashe ilifika katika mchinjio hayo jana ili kubaini iwapo agizo la Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba, limetekelezwa baada kufanya ziara ya kushtukiza usiku, mapema mwezi huu na kuagiza malipo ya ushuru wa mifugo yafanyike katika machinjio ya Vingunguti pekee.
Maofisa ambao walikutwa kwenye ofisi za viongozi wa machinjio hayo lakini walikataa kata kata kuzungumza na mwandishi wa gazeti hili wakidai kuwa wao si wasemaji.
Gazeti hili lilishuhudia hali ya usafi ikiwa mbaya kwenye maeneo mbalimbali ya machinjio hayo kutokana na baadhi ya sehemu kutapakaa damu na vinyesi vya mifugo.
Nipashe ilimtafuta Ofisa Afya ambaye naye alikataa kuonyesha ushirikiano kwa mwandishi wa habari hizi na alipogundua kuwa anatafutwa na mwandishi wa habari alitokomea kusikojulikana.
Wafanyabiashara waliozungumza na gazeti hili walisema viongozi wa machinjio hayo ni kama wamepuuza agizo la Waziri kwani wamekuwa wakiwalipisha ushuru katika mchinjio hayo ya Vingunguti na mnada wa Pugu pia.
Mmoja wa madalali wa mbuzi na ng'ombe, Huruma Ngosha aliiambia Nipashe kuwa katika mnada wa Pugu, mbuzi mmoja hulipiwa ushuru wa Sh. 2,000 na machinjioni Vingunguti hulipiwa tena Sh. 1,500.
"Jumla ya tozo kwa mbuzi mmoja ni Sh. 3,500 na kwa siku hapa Vingunguti wanaweza wakachinjwa mbuzi kati ya 300 hadi 400," alisema Ngosha.
Alisema ng'ombe mmoja katika mnada wa Pugu hulipiwa Sh. 8,000 na akifika machinjioni Vingunguti hulipiwa tena ushuru wa Sh. 5,000, hivyo jumla huwa ni Sh. 13,000 kila ng'ombe.
Katika ubao wa matangazo wa machinjio ya Vingunguti, idadi ya mbuzi, kondoo na ng'ombe wanaochinjwa na kulipiwa ushuru kila siku ilikuwa ni tofauti tofauti.
Wakati jana idadi ya ng'ombe ilikuwa 395 na mbuzi na Kondoo 625, Januari 14 mwaka huu, ng'ombe walikuwa 352 na Januari 13 ng'ombe walikuwa 316 wakati Januari 12 ng’ombe walikuwa 296.
Mwigulu alipofanya ziara hiyo aliwasimamisha Mkuu wa Mnada wa Pugu na watumishi waliokuwa zamu machinjio ya Vingunguti Desemba 24 mwaka jana na Januari Mosi mwaka huu.
Pia aliagiza ukusanyaji wa ushuru ufanyike kwenye Machinjio ya Vingunguti kwa kutumia mashine za kielektroniki.
Alisema mnada wa Pugu sasa utakuwa unatumika kutoa vibali tu vya mifugo ili kudhibiti ubora wa mifugo inayotakiwa kuchinjwa.
“Sitakuwa na huruma na hatua stahiki zichukuliwe kwa mtu yeyote mwenye dhamana ya kusimamia sekta hiyo atakayebainika kutowajibika kwa mujibu wa Sheria,” alisema Nchemba.
Waziri huyo alisema ubadhirifu uliopo ni wa uandikaji wa vibali kwa mifugo michache kwa ajili ya kwenda machinjioni, tofauti na idadi ya mifugo inayoingizwa machinjioni Pugu. Alisema mifugo mingi inaingizwa machinjioni bila kibali.

Habari Kubwa