Madaba wanabadili maisha kupitia zao la tangawizi

22Jan 2016
Nipashe
Madaba wanabadili maisha kupitia zao la tangawizi

KILIMO cha Tangawizi wilayani hapa hivi sasa kinasambaa kwa kasi kubwa, kila mkulima akihamasika kukiendeleza. Ni miongoni mwa mazao mahsusi kwa ajili ya kuinua uwezo wa wananchi masikini.

Mwishoni mwa mwaka jana, kulifanyika juhudi za wilaya zilizohamasishwa na mbunge Joseph Mhagama, iliwezesha kupatikana mbegu za tangawizi tani sita zenye thamani ya Sh. milioni 21, huku ikielezwa kwamba kuna soko kubwa limeshapatikana nchini Kenya ambalo linawsubiri wauzaji.

Mhagama anawaambia viongozi wawahimize wananchi kulima mazao ya tangawizi, mbaazi, alizeti na maharage na hadi sasa limeshakuwa na wakulima 2,745 na kunufaisha maisha ya wahusika.

Anasema kabla hajawa mbunge, wakati huo akiwa akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali, alifanya utafiti kuhusu shughuli za kilimo na mifugo na kubaini umasikini wa kipato unaowakabili wakulima wadogo, unakabiliwa na kilimo kisichokuwa na tija.

Mhagama anasema kuwa ugunduzi huo, ndio ulimfanya kuelekeza nguvu kwenye mazao mawili, alizeti na tangawizi anayoamini kuwa yana tija kwa uchumi wa mkulima.

Hivyo, walifanya kazi ya kuunda vikundi vya wakulima wadogo na kuwawezesha kuwa na soko la uhakika la kuuza mazao yao na
kabla ya kupelekwa kiwandani kwa ajili ya usindikaji na kuzalisha mafuta ya alizeti yenye ubora tofauti na ya viwandani

Anasema kuwa, shirika lilianza na wanachama wakulima 300 na hadi sasa wamefikia 2,745, huku mbegu zilizopandwa wakati huo zilikuwa kilo 10 na sasa ni zimefikia tani 9000.

Mratibu wa taasisi ya Rucodia inayosimamia uzalishaji wa zao hilo, Ladislaus Bigambo, anaieleza tangawizi kuwa ni zao la kiungo linalozalishwa kwa wingi nchini Jamaica.

Anasema kuwa, nchini Tanzania inazalishwa katika mikoa Kigoma, Tanga, Morogoro, Pwani, Mbeya, Kilimanjaro na Ruvuma wilayani Madaba.

Bigambo anaomba matumizi yake kuwa ni kiungo kcha kuongeza ladha, harufu na kuchangamsha katika vinywaji kama vile chai, soda, juisi na vilevi.

Pia, inatumika katika vyakula mbalimbali kama mikate, biskuti, keki, nyama za kusaga na achari

Anasema, hutumika zaidi katika viwanda vinavyotengeneza dawa za meno, kikohozi, tumbo na muwasho wa ngozi na hata vipodozi kama vile poda

WAKULIMA

Menas Mgaya ni mkulima wa zao hilo kutoka eneo la Mkongotema, anapongeza hatua ya wadau kuwawezesha kupiga hatua ya kimaendeleo katika kilimo hicho, ikiwemo kuwapeleka katika semina ya mafunzo maalum.

Anasema ni matunda ya uhamasishaji na wao wakulima kutikia wito, ambao sasa unawaletea manufaa ya fedha.

Mgaya anasema kuwa, kupitia kilimo hicho, sasa wana uhakika kijihudumia mahitaji yaonya kila siku kama vile gharama za elimu kwa watoto wao na mahitaji ya afya na makazi bora.

“Tungekuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kumudu maisha tena kwa kujiamini, kuliko ilivyo sasa, kama kweli viongozi wetu wangekuwa wanatumia utafiti sahihi wa kuondokana na umasikini katika maeneo yetu, kuliko kuendelea kufanya maisha ya kilimo au ki-ujasiriamali bila ya utafiti,” anasema Mgaya

Naye mkulima kutoka Magingo Njelekela anaitaja tangawizi kuwa mkombozi wa wakulima wa Madaba, kwani iimewaondoa kwenye unyonge na umasikini wa zamani.

Njelekela anasema kuwa, zamani umasikini wao wa kwenye kaya ulikuwa umekithiri, hata watoto katika familia wanakosa huduma nyinginezo.

Wanasema kukiwepo rasilimali ardhi na watu wanaopewa nyenzo, taifa halitakuwa miongoni mwa nchi zinazolalamika na umaskini, ilhali kuna mito, maziwa na mvua za kutosha.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Madaba, Vastus Mfikwa, anasema kuwa kwa kushirikiana na mbunge, wameweza kuzitembelea kata zote na kuainisha vipaumbe muhimu vya kuwakomboa wananchi kiuchumi, kielimu na kiafya

Anamwagia sifa mbunge wake kwamba juhudu yake ya kuhamaisha uanzushaji miradi mwelekeo wa kuwawezesha wananchi wa jimboni mwake, jambo anaahidi litashikiliwa vyema na timu ya halmashauri yake.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, mkazo uliopo sasa katika kampeni ya wilaya, ni kuhakikisha kila mkazi wa wilaya ana kipato cha wastani usiopungua Sh. 300,000 kwa mwezi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Robert Mageni, anatoa rai kwa wadau washirikiane kuipaisha kiuchumi wilaya hiyo.

Mwandishi wa Makala hii anapatikana kwa Simu: +255 715-928752.

Habari Kubwa