Magendo yanavyolitikisa zao jipya la vanilla kwenda nchi jirani

22Jan 2016
Nipashe
Magendo yanavyolitikisa zao jipya la vanilla kwenda nchi jirani

KUFANYIKA magendo imekuwa ikipigiwa kelele kila kukicha mkoani Kagera, kutokana na mkoa kupakana na nchi za Rwanda, Burundi na Uganda.

Magendo yamekuwa yakidhoofisha uchumi wa mkoa na taifa, huku hujuma ikiendelea kunufaisha wachahe nchini na nje ya nchi.

Hata hivyo katika miaka yote biashara ya mazao ambayo yamekuwa yakipigiwa kelele kuwa yanauzwa kwa njia za magendo ni kahawa.

Lakini, kutokana na zao hilo kushambuliwa na magonjwa na kuanzishwa mbadala, sasa kuna malalamiko mapya yameanza kuibuka, nayo ni zao la vanilla kuuzwa kwa magendo.

Zao hilo la vanilla, hutumika kama kiungo katika vyakula na vinywaji mbalimbali.

KUIBUKA VANILLA

Vanilla ni zao mbadala la biashara, lililoanzishwa na Shirika la Maendeleo ya Wakulima (Mayawa) mkoani Kagera, kusaidia kuinua kipato cha wakazi wa mkoa huo.

Hiyo ilijitokeza baada ya mazao maarufu mkoani kama vile ndizi na kahawa, kuanza kushambuliwa na magonjwa, hali iliyoathiri sana uzalishaji.

Mbali na kushambuliwa na magonjwa, pia bei ya kahawa sokoni imekuwa ikishuka kila mara. Kwa mfano, hadi kufikia msimu wa mwaka 2014/2015 unaokamilika Mei mwaka huu, zao hilo limekuwa likinunuliwa kwa bei ya Sh.1000 kwa kila kilo moja ya maganda.

UVAMIZI WA WALANGUZI

Kutokana na bei kuwa kubwa, zao hilo walanguzi kutoka nchi jirani ya Uganda wamekuwa wakilalamikiwa kuingia mkoani hapa wakilangua zao hilo kwa bei inayodaiwa kuwapunja wakulima.

Baadhi ya wakulima wanasema, mbali na ulanguzi huo wa vanilla unaofanywa na matapeli kutoka nchi jirani, sasa unahusisha pia marando (mche wa mbegu) ya vanilla inayoibwa na kuuzwa.

Mkulima Prosper Katunzi, kutoka eneo la Bugorora wilaya ya Missenyi, anasema hata shirika la Mayawa likitangaza kununua zao hilo kwa bei moja na walanguzi, bado walanguzi watapandisha bei zaidi, wataendelea kuwaibia wakulima kupitia mizani.

Katunzi anasema, walanguzi wanaonunua vanilla ya wakulima wanabeba mizani zao wakiwa na mbinu ya kununua kwa bei kubwa kuliko inayouzwa nchini.

Anasema, Mayawa inapotangaza kununua vanilla mathalan kwa Sh. 12,000 kwa kila kilo moja, walanguzi wanaingia vijijini wakipandisha bei hadi Sh. 13,000 au Sh. 14,000.

"Lakini kwa sababu wanawaibia wakulima kwenye mizani, mkulima anaweza kuona ameuza kwa Sh. 13,000 kumbe ukifuatilia utakuta ameuza kwa shilingi 9,000," anasema Katunzi.

Anafafanua zaidi: "Mlanguzi anapopima na kumwambia mkulima ni kilo moja, vanilla ile ile ikipimwa kwa mzani usio na dosari utakuta ni kama kilo moja na nusu."

Katunzi anaongeza kuwa, wakulima wengi wanaibiwa kwa njia na anashauri elimi zaidi itolewe kwa wakulima, kutambua mbinu zinazotumika kuwaibia, kupitia magendo hayo.

Mkulima mwingine Mnawara Rwegoshora, kutoka kijiji cha Kasharu anashauri njia ya kudhibiti biashara hiyo ya magendo kuwa ni kuwaorodhesha wakulima na idadi ya miche ya vanilla waliyo nayo, ili inapotokea wanauza bidhaa zao kwa njia ya magendo wafahamike.

"Mkulima akiorodheshwa, pia wataalam watakuwa na uwezo wa kujua katika msimu huo atavuna na kuuza kiasi gani, lakini pia mkulima akihitaji mkopo kutoka Mayawa, apewe hela ili amalize shida yake na siku akiuza vanilla yake atalipa deni," anasema.

Rwegoshora anaongeza kuwa, iwapo utaratibu huo ukifuatwa, haitakuwa rahisi mkulima kuuza vanilla kwa magendo, kwa sababu ana fursa ya kumaliza shida yake na uhalisia utamuanika.

MAYAWA YAINGILIA KATI

Charles Kamando ni meneja wa Mayawa anayesema kuwa nchi jirani ya Uganda wanapenda kununua vanilla inayolimwa Kagera kwa sababu inang'ara sokoni.

Kamando anasema kuwa, vanilla ya Kagera hununuliwa nchini Uganda na wanaichanganywa na inayopatikana huko kuongezea ubora.

Anasema mbali na kuzuia biashara hiyo ya magendo, pia kinachopaswa kufanyika ni kushirikisha wataalam katika kila hatua, ikiwamo ukataji wa marando kwa ajili ya kupanda au kuuza.

"Katika kukata marando wakulima, wanapaswa kuwahusisha mabwana shamba ili wanapokata marando ya kuuza waweze kupata faida badala ya hasara, kutokana na kuyakata bila utaalam maana mhusika anaweza kukata hata sehemu ambayo haistahili na kusababisha kupoteza mavuno," anasema.

Anasema kuwa endapo rando hilo lililokatwa lingekuwa na uwezo wa kutoa vanilla kilo moja na nusu,linapokatwa linauzwa kwa bei kati ya Sh. 500 na 1000, wakati kila kilo moja ya zao hilo ni Sh.12,000 kwa bei ya msimu wa mwaka 2014/2015.

Kamando anasema, shirika hilo hivi sasa litaanza kufuatilia na kuona namna wakulima wanaweza kuanzisha kilimo cha mkataba kuinua uchumi wao.

Mwenyekiti wa Mayawa, Slyvester Katemana, anakiri wakulima kuuza vanilla yao kwa magendo na anatumia ulingo huo kuwatahadharisha wakulima kuwa makini na kupunjwa haki zao kupitia magendo ya vanilla.

"Tumeishalifikisha suala hili kwa serikali, ili itusaidie kukabiliana nalo, maana sisi pekee hatuwezi.

"Wanaofanya hivyo, mbali na kusababisha wakulima kuendelea kuwa maskini, pia wanasababisha kushusha uchumi wa nchi na kuikosesha fedha za kigeni," anasema Katemana.

Anafafanua kuwa, Mayawa ilianzishwa ili kuwawezesha wakulima kuingia katika kilimo cha kibiashara, itakayowapunguzia umasikini.

Miongoni mwa mazao ya biashara walioyaanzisha mbali na
Vanilla ni pilipili, uyoga na rosella.

Anasema katika msimu wa mwaka jana, walisambaza na kuwagawia wakulima marando 3,135, katika wilaya za Missenyi, Bukoba na Muleba na wanategemea kugawa marando 400 katika wilaya ya Karagwe.

Katemana anasema, Mayawa itaendelea kuongeza ufanisi wa kuhudumia wakulima kwa kuwalipa pesa wanapopeleka mazao hayo, kukusanya, kukausha na kufungasha na kisha wanawatafuta masoko katika nchi za Ulaya na Marekani.

"Tutaendelea kuboresha bei za mazao kila msimu. Mfano msimu wa mwaka 2013/2014, vanilla mbichi kilo moja kuanzia daraja la kwanza hadi la tatu tulinunua kwa shilingi 8,500, lakini katika msimu wa mwaka 2014/2015 ilipanda hadi shilingi 12,000," anasema.

Jingine analosema ni kwamba, Mayawa itaboresha utengenezaji wa mvinyo ya rosella, ili kujenga na kuinua soko kwa ajili ya wakulima waliokosa soko la zao hilo.

Katemana anasema, katika shughuli zao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo mwitikio mdogo wa wakulima kulima zao la vanilla.

CHANGAMOTO

Anasema, iwapo zao hilo litalimwa
kwa wingi, kuna uwezekano wa kuinua pato la wakulima kwa kusaidiana na mazao mengine kama vile kahawa.

Changamoto nyingine anayoitaja ni upungufu wa fedha za ugani, kwani wataalam wao hawatoshi, hali inayosababisha wakulima wanaotaka kujiunga na kilimo cha mazao wanayohamasisha, kukosa ushauri.

Katemana anasema kuwa, ili kukabiliana na changamoto zilizo mbele yao, wana mpango wa kujenga kiwanda cha kusindika rosella, kwa kutengeneza juisi na mvinyo na kuangalia uwezekano wa kuanzisha kituo cha redio, kusaidia uelimishaji wa wakulima katika kilimo na ufugaji.

"Tutaimarisha duka letu la Mayawa, kuwezesha kuuza pembejeo za kilimo na bidhaa nyingine zinazotumiwa na wakulima na wadau wengine, ili tutengeneze mapato ya ziada kwa ajili ya kuwahudumia wakulima wetu ipasavyo," anasema.

Mwenyekiti huyo anadokeza kuwepo mpango wa kuanzisha chuo cha kufundisha wananchi, stadi za kazi na kilimo cha mazao yanayohamasishwa na Mayawa.

Anakiri kuwa miradi hiyo ni mikubwa, hivyo shirika linaendelea kutafuta wahisani wa kuisaidia.

Changamoto nyingine anayotaja ni wakulima kuibiwa vanilla yao ikiwa shambani, tatizo linalosababishwa na kuwapo walanguzi wa zao hilo vijijini, na kuwa hali hiyo inawafanya wakulima kuvuna vanilla ambayo haijakomaa na imekuwa ikikaushwa, inashusha ubora wake sokoni.

Hata hivyo, anasema shirika lina mipango ya baadaye ya kuwainua wakulima kiuchumi, ikiwamo kuendelea kugawa marando kwao kwa mwaka 2016, ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo katika mkoa.

Katemana anaahidi kuwahamasisha wakulima kuwapatia mafunzo ya kilimo hai na mseto, ili kuwawezesha kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kuongeza thamani kwenye vanilla na pilipili, ambayo sasa ina soko kubwa.

MSIMAMO WA SERIKALI
Adam Swai ni Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia uchumi na uzalishaji mkoani Kagera, anaunga mkono hoja kuwa bei ya vanilla iko juu sokoni, kulinganisha na kahawa na chai.

Anasema, vanilla imeingizia serikali Sh. milioni 793.3 katika msimu wa mwaka 2014/2015, kutokana na mauzo yaliyofanyika nje ya nchi.

"Takwimu zinaonyesha mwaka 2014/2015 vanilla ilinunuliwa kwa shilingi 12,000; pilipili kwa shilingi 2,800, uyoga mbichi shilingi 5,000; uyoga mkavu shilingi 40,000; na rosella shilingi 5,000 kwa kila kilo moja ya mazao haya; huku kilo moja ya kahawa ya maganda ikiuzwa kwa shilingi 1,000," anasema.

Swai anashauri Mayawa kuhamasisha wakulima katika wilaya za Ngara, Kyerwa, Karagwe na Biharamulo, kuanzisha kilimo cha mazao yanayohamasishwa na shirika hilo, ili wajiinue kiuchumi.

Kuhusu malalamiko ya walanguzi wa vanilla, anawashauri wakulima kujiunga katika vikundi vyama vya ushirika vya akiba na mikopo (Saccos), ili kuwawezesha kuanzisha ujasiriamali, utakaowasaidia kupambana na ulanguzi.

Pia, ana rai wakazi wa Kagera kutumia fursa ya kupakana na Rwanda, Burundi, Uganda na nchi ya Sudan Kusini ambayo ni jirani wa Uganda kwa upande wa Kaskazini, kuuza ziada ya mazao wanayozalisha.

Swai anaoanisha hilo na Dira ya Taifa kuelekea mwaka 2025, inayotaka kuondokana na umaskini kwa kuwezesha kuwapo uhakika wa wananchi kupata chakula, kupeleka watoto shule na huduma bora za afya.

"Hili linaweza kufikiwa kwa Kagera, kama wakulima wengi watajiunga na Mayawa na kuongeza kipato chao kwenye familia na kupunguza umaskini kwa kiasi kikubwa," anasema.

Shirika la Mayawa lilianzishwa mwaka 1997 kwa malengo ya kuongeza kipato cha wakulima waliojiunga katika vikundi, katika wilaya tatu za Bukoba, Missenyi na Muleba na wakulima wachache wa wilaya ya Karagwe.

Hadi sasa lina vikundi 278 vyenye wakulima 4,948 wanaolima pilipili, vanilla, rosella na uyoga na katika
msimu wa mwaka 2014/2015, waliuza vanilla kilo 4,640 nchini Marekani na kuingiza nchi Sh. milioni 793.3.

mfanikio hayo yanaifanya Mayawa kuwa na mpango wa kuwalipa wakulima nyongeza ya bei ya Sh. 1,000 kwa kila kilo moja ya vanilla mbichi.

Zao hili hutumika kama viungo katika vyakula na vinywaji mbalimbali.

Habari Kubwa