Mahakama Wilaya ya Serengeti yapewa msaada wa kompyuta.

25Jan 2016
Nipashe
Mahakama Wilaya ya Serengeti yapewa msaada wa kompyuta.

Mahakama ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, imepokea msaada wa vifaa vya kisasa vya Teknolojia, Habari na Mawasiliamo (Tehama) kutoka kwa kampuni ya utalii ya Singita Grumeti Reserves Ltd na shirika lake dada la Grumeti Fund.

Katibu Tawala Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Cosmas Qamara (wa pili kushoto), akikamkabidhi seti ya kompyuta.

Vifaa hivyo ikiwamo kompyuta na printa, vilikabidhiwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Serengeti, Ismael Ngaile, katika hafla iliyofanyika katika ofisi za mahakama hiyo iliyopo mjini Mugumu.

Ngaile alishukuru Grumeti kwa kuitikia ombi lao kuwapatia vifaa hivyo na kuahidi kuvitumia kuboresha huduma katika mahakama hiyo.

“Tulikuwa tunafanya kazi kwa kutumia kompyuta moja, lakini sasa ufanisi utaongezeka na nakala za hukumu zitatoka mapema kuliko ilivyokuwa zamani. Hivyo kwa kweli tunashukuru sana,” alisema Ngaile.

Meneja wa Mahusiano wa Singita Grumeti Reserves na Grumeti Fund, Ami Seki, alisema msaada huo ni sehemu tu ya mchango wanaotoa kuboresha huduma mbalimbali kwa wananchi wa Wilaya za Serengeti na Bunda mkoani Mara.

“ Tunaamini kuwa vifaa hivi vitasaidia kurahisisha kazi za kiofisi na hivyo kuboresha huduma na hii ni sehemu tu ya misaada inayotolewa na Singita Grumeti Reserves kwa kushirikiana na Grumeti Fund kuboresha huduma kwa wananchi,” alisema Seki.

Akizungumza katika halfa hiyo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Serengeti, Cosmas Qamara, alisema vifaa hivyo vitaiwezesha mahakama hiyo kufanya kazi kwa kutumia teknolojia ya kisasa na hivyo kuharakisha upatikanaji wa haki.

“Nina imani sasa wananchi watakuwa wanapata nakala za hukumu ndani ya wiki moja badala ya miezi mitatu na ni hatua nzuri katika kupata haki kwa wakati,”, alisema Qamara.

Aidha, aliishukuru Grumeti kwa kuendelea kutoa misaada mbalimbali ambayo inasadia kubadilisha maisha ya wananchi.

“Tunathamini sana juhudi mnazozifanya. Hii siyo mara ya kwanza kupata msaada kutoka Grumeti. Mmefanya mambo mengi mazuri katika sekta za elimu, maji na afya,” alisema Qamara.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Naomi Nnko na Mwenyekiti wa halmashuri hiyo, Juma Porini.

Viongozi hao pia walisema kampuni ya Grumeti imeonyesha mfano ambao unapaswa kuigwa na wawekazaji wengine ambao wamewekeza katika wilaya hiyo.

“Grumeti ni wadau wetu muhimu sana. Wamefanya mambo mengi sana na wadau wengine wajifunze kutoka kwao”, alisema Mwenyekiti wa Halmashauri ya Serengeti, Juma Porini.

Uwekezaji katika miradi ya jamii ambao unafanywa na Singita Grumeti Reserves kwa kushirikiana na Grumeti Fund, unaripotiwa kupunguza vitendo vya uwindaji katika mapori tengefu ya Ikorongo na Grumeti.

Habari Kubwa