Majabvi: Ajibu ni zaidi ya Samatta

20Jan 2016
Lete Raha
Majabvi: Ajibu ni zaidi ya Samatta

KIUNGO wa ulinzi wa Simba, Justice Majabvi, anaamini kuna mchezaji Simba mwenye uwezo wa kipekee na anayeweza kumpiku Mbwana Samatta.

Justice Majabvi

Amemtaja mchezaji huyo kuwa ni wa Ibrahim Ajibu na amedai kuwa iwapo nyota huyo atakuwa tayari kujituma anaweza kupata mafanikio zaidi ya Samatta ambaye kwasasa ndiye mshindi wa tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani ya bara hili.
Majabvi alisema, “Ajibu hapaswi kuzubaa hadi afikishe miaka 25 kwani kwa Ulaya atakuwa amezeeka, kwasasa akiongeza bidii kidogo anaweza kupata mafanikio makubwa nje ya Tanzania.
“Ana kipaji ambacho sijakiona kwa mchezaji mwingine tangu nilipokuja hapa Tanzania. Na mpaka sasa ndiye mchezaji pekee mwenye uwezo wa kubadili matokeo wakati wowote anapokuwa uwanjani.
“Mbali na kipaji, ana umbo zuri na ana uwezo wa kupambana na mabeki wenye miili mikubwa, kama atajituma zaidi ya anavyofanya sasa, naamini anaweza kwenda mbali zaidi ya alipo Samatta,” alisema kiungo huyo wa zamani wa timu taifa ya Zimbabwe.
Naye kocha msaidizi wa zamani wa Simba, Seleman Matola, amemtaka Ajibu kutumia vyema kipaji chake cha uchezaji hili aweze kufika alipo Samatta kwani ana uwezo huo.
Matola alisema mshambuliaji huyo ni mdogo na ana kipaji kikubwa ambacho iwapo atakitumia vizuri ipasavyo ataweza kufika mbali kwani soka lake ni la kutumia akili nyingi.
"Ajibu anapaswa kutambua kuwa kwa uwezo alionao hapaswi kuwa hapa Tanzania. Ana uwezo wa kufika alipo Samatta na hata njia alizopita nyota huyo tayari Ajibu amepita.”
Naye kiungo wa Toto African, Abdallah Seseme, ambaye aliwahi kuichezea Simba, alisema anatambua uwezo wa Ajabu tangu walipokuwa wakicheza timu za mtaani ambazo ni Amana Shooting na Bombom FC.
"Ana umri mdogo ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa, nimecheza naye Simba ‘B' na kikosi cha wakubwa. Kama wanataka afanye vizuri basi anapowakosea viongozi wake, wanatakiwa kumuelimisha na siyo kumlaumu. Kwa msaada wao, watafaidika na matunda ya kipaji chake,” alisema Seseme.

Habari Kubwa