‘M-Mama’ inavyomweka rahani mjamzito, mtoto

21Jun 2022
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
‘M-Mama’ inavyomweka rahani mjamzito, mtoto

MFUMO wa kielektroniki wa kitaifa wa kusafirisha kwa dharura wajawazito na watoto wachanga M-Mama, unaotumiwa zaidi vijijini, umethibitisha kuwa ni mwarobaini wa kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.

Dereva Edmund Kinubi akiwa kazini. PICHA: MARCO MADUHU

M-Mama unaotumiwa kuwawahisha wajawazito kwenye huduma za kiafya ili kujifungua salama, unaelezwa kuwa umeokoa maisha ya mama na watoto wengi hapa Shinyanga, anasema dereva Edmundi Kinubi.

Ni dereva anayetoa huduma katika mahojiano na Nipashe, anasema hutolewa na madereva wa magari binafsi waliko vijijini wanaowapa msaada wa dharura muda wote mjamzito kwa kumtoa nyumbani na kumpeleka kwenye huduma za afya ili kujifungua salama.

Anaeleza kuwa ilianzishwa baada ya kuwepo changamoto ya usafiri kwa kinamama wajawazito hasa vijijini, ili kuwasaidia kwenda hospitalini badala ya kujifungulia njia au majumbani jambo linalosababisha ongezeko la vifo vinavyotokana na uzazi.

Kinubi anakumbusha kuwa mkoani Shinyanga, huduma ilianza mwaka 2017 kwa ushirikiano na kampuni ya Vodacom Tanzania Foundation, Vodafone Foundation na Shirika la Pathfinder International, lakini sasa ipo chini ya serikali.

Kinubi anayetoa huduma hiyo akisafirisha wajawazito kwa dharura kutoka nyumbani kwenda kwenye vituo vya afya, anajisifu kuwa ameokoa maisha ya wajawazito wengi.

Anasema ili kumfikia mama anapigiwa simu kwa namba za bure ambazo zimetolewa na Vodacom hivyo kuwahi kwa wakati ili kumfikisha mjamzito hospitalini haraka iwezekanavyo ili kujifungua salama.

Anasema tangu alipoanza kutoa huduma hiyo ya usafiri wa dharura kwa wajawazito mwaka 2019, ameokoa wajawazito wengi na kubainisha kuwa endapo asingewafikia huenda wangepoteza maisha kwasababu ya kukosa usafiri.

“Nakumbuka nimekumbana na matukio mengi kwa kuwakuta wajawazito katika hali mbaya, na baada ya kuwafikisha hospitalini walijifungua papo hapo,”anasema Kinubi.

“Kuna mwingine nilipomfikisha hospitali alijifungua lakini alipoteza damu sana, mfano huyu angejifungulia nyumbani ingekuwaje? Maisha yangeweza kupotea,” anaongeza.

Anasema maeneo mengi ya vijijini hakuna usafiri salama kwa ajili ya wajawazito na huduma zake za afya hua zipo umbali mrefu, na mara nyingi usafiri ambao hutumia ni bodaboda au mikokoteni ya ng’ombe, ambayo hukatisha tamaa wajawazito na kuamua kujifungulia nyumbani licha ya kwamba ni eneo ambalo siyo salama.

Anasema kutokana na kufahamu tatizo hilo la ukosefu wa usafiri maeneo hayo ya vijijini, alikuwa anahakikisha gari lake linakuwa zima, lina mafuta ya kutosha, na simu yake kuwapo hewani wakati wote, ili akipewa taarifa anakuwa tayari kwenda kumchukua mjamzito na kumwahisha hospitali.

“Zamani nilikuwa nafanya biashara ya kusafirisha abiria wakati nikiendelea na huduma hii ya M-Mama ya usafirishaji wajawazito kwa dharura, lakini baada ya kuona wajawazito wengi wapo katika hatari ya kupoteza maisha, nikasitisha biashara ya kusafirisha abiria na kubaki kutoa huduma hii hadi sasa,”anaeleza Kinubi.

“Huduma hii ya kusafirisha wajawazito inataka moyo wa huruma pamoja na kujitoa sana, hapa Tinde tulikuwa madereva sita ambao tunatoa huduma hii, lakini wengine wote wameacha na kubaki peke yangu, sababu nimeguswa na wajawazito wanavyoteseka kwa kukosa usafiri, na kubebwa kwenye bodaboda na mikokoteni ya ng’ombe ni usafiri ambao siyo salama kwao,” anasema Kinubi.

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuzindua huduma hii ya M-Mama nchi nzima, ninachokiomba tu kwa serikali iboreshe miundombinu ya barabara hasa vijijini, ni kwa sababu kuna muda unashindwa kabisa kumfuata mjamzito nyumbani kwake, hadi asogezwe na bodaboda kuvuka upande wa pili ndipo upakie kwenye gari na kuwahi hospitali. Hili si jambo jema anaweza kuchelewa .

Kama barabara zingefunguka ingekuwa rahisi zaidi kumsaidia,” anaeleza Kinubi. Mnufaika wa huduma hiyo ya M-Mama ya usafiri wa wajawazito kwa dharura, Judith Kayegeji, anasema bila kuwapo na huduma hiyo huenda angekuwa ameshapoteza maisha.

Anasema ilimnusuru kwa kumuwahisha hospitali na alipojifungua alipoteza damu nyingi, lakini kutokana na huduma na wataalamu yeye na mtoto wake wako salama.

Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Flora Kajumulla, anasema huduma hiyo ya M-Mama, imekuwa msaada mkubwa mkoani humo na imepunguza vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi.

Anasema huduma hiyo kwa sasa inasimamiwa na serikali na kwamba madereva wanaowahudumia wajawazito huwalipa, na kila wanapombeba mjamzito na kumfikisha kwenye huduma ya afya kuna kuna fomu za kujaza na mwisho wa mwezi hulipwa pesa zao.

Anasema tangu huduma hiyo ya M-Mama ianze kufanya kazi mkoani Shinyanga mwaka 2017, hadi kufika mwaka jana imeshawafikia kinamama 5,769. Wamepatiwa elimu ya afya ya uzazi pamoja na kuhimizwa kujifungulia kwenye huduma za afya maeneo ambayo ni salama.

“Mwaka 2016 vifo vya mama vitokanavyo na uzazi vilikuwa 74, lakini baada ya kuanza huduma hii ya M-Mama mwaka 2017 na hadi kufikia mwaka jana (2021) tulipunguza vifo hadi 50 sawa na upungufu wa asilimia 40,” anasema Kajumulla.

“Vifo vya watoto wachanga mwaka 2016 vilikuwa 1,080, lakini mwaka jana 2021, kutokana na M-Mama vimepungua hadi 665 sawa na asilimia 45,” anaongeza.

Habari Kubwa