Ajali ilivyompokonya mguu mmoja, ndoto ya uanariadha haikuisha

18Apr 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Ajali ilivyompokonya mguu mmoja, ndoto ya uanariadha haikuisha
  • •Miaka minne chozi la baba halijakauka

“MGUU wangu ulikatwa, baada ya kupata ajali ya gari huko Yombo Vituka, jijini Dar es Salaam. Licha ya kukatwa mguu huo haujaondoa ndoto yangu ya kuwa mwanariadha,” ni sauti inayotoka kwa Abdul Hamad (10), akianika msimamo na hisia alizo nazo sasa.

Abdul Hamad akifurahia michezo. PICHA: ROMANA MALLYA

Hiyo ndiyo simulizi ya awali, akiitikia swali kutoka gazeti la Nipashe, kutaka kujua alikosimama na ndoto yake anakoelekea, hivi sasa akiwa mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Mkombozi, iliyopo Yombo Vituka, jijini Dar es Salaam.

Akiendelea na simulizi kilichomfikisha hatua ya kupoteza mguu wake, anasema: “Nilipata ajali mwaka 2015, nakumbuka nilikuwa nimepakiwa kwenye baiskeli.

Nilikuwa na rafiki yangu ambaye wakati huo alikuwa akiiendesha, tukiwa barabarani, ghafla gari lilitokea huko na kutufuata tulikokuwa na kutugonga.

“Nilisimuliwa kuwa baada ya kugongwa nilirushwa kwenye nguzo. Naweza kusema hapo ndipo maisha yangu yalipobadilika, badala ya kutembelea na miguu miwili ambayo Mungu alinipa.

“Nilinyanyuliwa eneo la ajali mguu mmoja ukiwa unaning’inia ‘umesagwasagwa’ umebaki ngozi tu ikiushikilia,” anasimulia Abdul.

Mwanafunzi huyo anaeleza kuwa baada ya ajali hiyo alipelekwa katika Hospitali ya Temeke na baadaye Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Huko nako alihamishiwa katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (Moi), walipoamua kumkata mguu kutokana kushindikana kuungwa.

Abdul anasimulia kuwa, kabla na baada ya ajali alikuwa na ndoto ya kuwa mwanariadha. Abdul anaendeleza simulizi kwa tabasamu, akisema:

“Napenda kukimbia napenda sana kuwa mwanariadha. Napenda kutambulika kitaifa, napenda kupeperusha bendera ya Tanzania kimataifa. Hii ndiyo ndoto yangu, naamini siku moja itatimia.”

“Kila mtoto anapozaliwa anapokuwa kwenye safari ya ukuaji huwa na ndoto yake. Mimi napenda sana kuwa mwanariadhara na mara kwa mara huwa namwambia baba yangu,” anasimulia Abdul, huku akinyoosha kidole kumwelekeza baba yake, Mzee Kipango.

“Ninaamini ndoto yangu itatimia, haijalishi nina mguu wa bandia au la. Kwanza, nikijifananisha nilivyokuwa awali baada ya kuwekewa mguu wa kwanza wa bandia na huu wa pili, najiona nipo tofauti.

“Mguu huu wa sasa niliyowekewa mwaka jana, najiona kama mtu wa kawaida. Nimeuzoea, naweza kucheza mpira na watoto wenzangu na kukimbia pia.”

Mguu bandia Abdul anasema baada ya kukatwa mguu mwaka 2016, aliwekewa mguu wa kwanza na MOI, anakiri katika siku za kwanza haukuzoea na ulikuwa ukimtesa.

“Niliwekewa mguu wa bandia ili uniwezeshe kutembea kama ilivyokuwa awali, lakini kwa sababu ulikuwa ni mgeni mwilini, nilipata nao tabu, hata baba nilikuwa nikimwambia,” anasema.

Anasimulia kuwa mwaka jana kupitia Hospitali ya CCBRT, jijini Dar es Salaam, alipata mguu bandia mwingine, anaoamini umerejesha kwa kiwango fulani ndoto yake ya kuwa mwanariadha.

“Huu mguu bandia niliowekewa mwaka jana umenifanya niwe sawa. Naweza kupiga mpira kwa kutumia mguu huu mzima na huu wa bandia nikatumia kupata nguvu ya kusimama. Najiona nipo sawa sasa, ingawa siyo sawa kama nilivyokuwa na miguu yote miwili,” anasema.

Ni mazungumzo ya Nipashe na Abdul, katika Hospitali ya CCBRT, ambako alikuwa miongoni mwa waalikwa, walioshiriki kwenye uzinduzi wa jengo la kliniki ya huduma binafsi iliyoanzishwa hospitalini hapo.

Anayemvutia Abdul anamtaja kivutio kikuu chake ni mwanariadha mlemavu wa miguu yote miwili wa Afrika Kusini, Oscar Pistorius, ambaye anaamini, siku moja atafikia mafanikio ya kiwango chake.

Kwa kifupi, Pistorius ni mlemavu wa miguu yote miwili ambaye mwaka 2012 alinyakua medali ya dhahabu katika mbio za mita 400 na kuweka historia katika michezo ya Olimpiki iliyofanyika jijini London, Uingereza.

Wakati huo Pistorius alikuwa na umri wa miaka 25, alipotetea taji la mbio za mita 400 zijulikanazo kama ‘T44’ zilizokuwa maalum kwa watu walemavu wa ama miguu yote au mmoja.

Alikuwa mkimbiaji pekee katika mbio hizo, aliyetumia muda chini ya sekunde 50. Abdul anaeleza imani yake kuwa ni kitu ambacho kipo ndani ya hisia zake na kila mara amekuwa akikifanyia mazoezi dhamira hiyo, akifafanua: “Kama nilivyokuambia, napenda riadha.

Huu mpira unaouona huwa pia nacheza mtaani, mpira wa miguu na watoto wenzangu.” Baba yake? Baba wa mtoto huyo, Hamad Kipango, anasimulia siku na namna taarifa za mkasa wa mwanawe ulipotokea, kwamba alikuwa eneo la Vingunguti, Dar es Salaan, akiendelea na shughuli za ujasiriamali wa kuuza mihogo.

“Nakumbuka ilikuwa ni Julai 19, mwaka 2015, majira ya saa nne asubuhi, ilikuwa sikukuu. Nilipigiwa simu kutoka nyumbani, nikifahamishwa kuwa Abdul amepata ajali akiwa kwenye baiskeli,” anasema.

“Nilishtuka sana, nikaambiwa wakati huo ameshapelekwa Hospitali ya Temeke. Nakumbuka nilichukua usafiri wa pikipiki, nilipofika nilijikuta natokwa machozi baada ya kumuona Abdul mguu wake wa kushoto ni kama umekatika, imebaki ngozi tu inaning’inia.”

Kipango ambaye yeye na mke wake wanajishughulisha na uuzaji mihogo, anasema baada ya taratibu zote katika Hospitali ya Temeke walihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambako walipokelewa kitengo cha dharura.

“Alipofika kitengo cha dharura Muhimbili walitushauri afanyiwe kipimo cha ‘CT Scan’ kuangalia kama ameumia eneo la kichwani kwa sababu wakati huo alikuwa akitoka damu mdomoni na sikioni. Tunamshukuru Mungu majibu yalionyesha hakupata tatizo kichwani,” anasimulia.

“Baada ya majibu hayo ndipo tulipohamishiwa Taasisi ya Mifupa MOI na ilipofika saa moja usiku majibu ya mguu yalitoka, daktari aliniambia kuwa hawawawezi kuuunga watakachokifanya ni kuukata.

“Haikuwa rahisi kupokea jambo hilo,” anasema Kipango, huku kumbukumbu ya simulizi hiyo ikimtoa machozi. Anaendelea: “Kiukweli baada ya kuelezwa hivyo nililia sana hadi leo hii kila nikimwangalia mwanangu huwa natokwa na machozi.

“Nakumbuka ilikuwa saa nne usiku nikaambiwa Abdul anaingia chumba cha upasuaji na baada ya muda akatolewa. Ulikuwa mtihani kwangu. Ni mtihani wa maisha ambao sijawahi kuusahau hasa kila nikimwangalia mwanangu Abdul. Siamini kilichotokea,”

Kipango anatamka huku akirejea hisia ya kilio. Anasema, katika kipindi hicho chote, alitumia muda wote akiwa hospitalini, kwa sababu wakati Abdul anapata ajali mke wake (mama Abdul) alikuwa na siku ya tatu tangu ajifungue.

Maisha mapya Kipango anasimulia kuwa baada ya kukatwa na kupitia kipindi cha mateso na maumivu makali ya jeraha, hatimaye mwanawe alianza safari mpya ya kutumia mguu bandia aliopatiwa na taasisi ya MOI mwaka 2016.

“Alikuwa akilalamika mara kwa mara kuwa anaumia, lakini kadiri siku zilivyokuwa zinasonga, aliuzoea, ingawa haikuwa rahisi kama tunavyofikiria,” anasema.

Anasema mwaka jana, Hospitali ya CCBRT ilimpatia mguu mwingine ambao akiulinganisha na awali, sasa una sura ya matumaini zaidi. “Mwanangu mbali ya ndoto yake ya kuwa mwanariadha, anapenda sana mpira kama unavyomuona na mpira wake.

Hata akiwa nyumbani hupenda kucheza mpira, kupiga danadana hayo ndiyo maisha yake. “Pia, kukimbia ndiyo ndoto aliyokuwa nayo tangu awali na hajaibadilisha anapenda kuitimiza,” anasimulia Kipango.

Kipango anasema, kiwango cha ufaulu wa mwanawe umeshuka shuleni, mara baada ya ajali hiyo, akifafanua: “Kabla ya ajali alikuwa akifanya vizuri kwenye masomo yake.

“Kipindi anapata ajali alikuwa darasa la pili, lakini baada ya ajali, ufaulu wake umeshuka sana. Ile ajali ilimwathiri kwa kiwango kikubwa, ufaulu wake siyo mzuri sana.” Maoni ya Baba Kipango anasema umasikini kwenye familia nyingi, umechangia ndoto za vijana hao kutotimia. Anaendelea:

“Kama unavyojua familia zetu ni za kimaskini, Muda mwingi huwa tunatumia kutafuta riziki na kurudi nyumbani.” “Mara nyingi unakuta watoto wameshalala au mwenyewe unakuwa umechoka hata muda wa kukaa na watoto unakosa,” anasema. Anaendelea: “Binafsi sina ajira, najitafutia.

Kwa hiyo wakati mwingine nakosa hata muda wa kukaa na watoto, ila ninapoupata ingawa ni ‘mchache’ tunaelekezana mawili matatu. “Mara kwa mara Abdul huniambia kuwa anapenda kuwa mwanariadha. Namuombea kwa Mungu ndoto yake itimie, ndicho nachoweza kusema kwa sasa.

” Pia, mzazi huyo wa Abdul, anaiomba serikali iendelee kuwasaidia walemavu na wapatia vifaa bandia kila inapowezekana ndivyo matumaini mapya kwao yanapoonekana. Ushauri wake ni kwamba, vifaa hivyo ni vyema viondolewe kodi ili visiuzwe kwa bei kubwa.

“Mguu huu wa bandia aliouvaa Abdul nimeambia unauzwa sio chini ya milioni sita. Abdul ameupata kwa msaada wa CCBRT. Ukweli ni kwamba ingehitajika niununue. Sidhani kama ningeweza.

“Naishukuru CCBRT, kwa sababu nikimwangalia mtoto wangu kwa sasa, licha ya kwamba amewekewa mguu wa bandia, lakini unamsaidia kutembea kama watu mwenye miguu miwili. Mungu awabariki sana,” anahitimisha.

•Mzazi wa Abdul Kipango, anapatikana kwa simu: (+255) 0787 432696

Habari Kubwa