Bil. 25/- zatumika kuboresha barabara

23Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
Musoma
Nipashe
Bil. 25/- zatumika kuboresha barabara

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa, amesema Sh. bilioni 25.3 zimetumika kuboresha barabara na mitaa ya Manispaa ya Musoma ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015.

Alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na wakazi wa mji wa Musoma katika mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Mara, mjini hapa.

“Sh.bilioni 18.7 zimetumika kujenga kilomita 14 za barabara kwa kiwango cha lami na kuweka taa za barabarani kupitia Programu ya Uboreshaji wa Miji (ULGSP) katika Manispaa ya Musoma na mradi umekamilika. Tunataka taa ziwake ili usiku uwe mchana, na mchana uwe mchana,” alisema

Pia alisema kupitia Mfuko wa Barabara, Sh. bilioni 6.6 zilitumika kwa ajili ya kufungua barabara mpya, kufanya matengenezo ya kawaida na matengenezo ya sehemu korofi na kwamba miradi yote imekamilika.

Majaliwa ambaye yuko mkoani Mara kumwombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Rais John Magufuli, alitumia fursa hiyo kuwaombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Musoma Mjini, Vedasto Manyinyi, mgombea udiwani wa kata ya Nyamatare, Masumbuko Magesa na wagombea wengine wa udiwani wa manispaa hiyo.

“Ninawasihi wana Musoma msisite kumpigia kura John Magufuli hata kama wewe ni mpenzi wa chama kingine kwa sababu yeye ndiye mleta maendeleo kwa nchi yetu,” alisema.

Kuhusu mambo mengine yaliyotekelezwa chini ya ilani hiyo, Majaliwa alisema “kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani” ililenga kumpunguzia mama kazi ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji na badala yake atembee hatua chache kutoka bombani hadi nyumbani akiwa ameshika ndoo yake mkononi.

“Ili kuboresha huduma za upatikanaji wa maji kwenye mji wa Musoma, Sh. bilioni 46 zilitolewa kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji safi katika Manispaa ya Musoma ambao tayari umeanza kutoa huduma,” alisema Majaliwa.

Alisema Sh. bilioni 18 zimetolewa kwa mradi wa kusambaza maji katika Manispaa ya Musoma na vijiji vitatu vya wilaya ya Musoma na Butiama na kwamba kazi zinazofanywa ni ujenzi wa tangi la Bharima lenye ujazo wa lita milioni tatu, ujenzi wa kituo cha kusukuma maji na ulazaji wa bomba la kusafirisha maji kwenda kwenye tangi la Bharima lenye kipenyo cha milimita 450 na urefu wa kilomita 1.56.

Alizitaja kazi zingine zilizofanyika kuwa ni ulazaji wa bomba la kusafirisha maji kutoka kwenye tangi la Bharima kwenda kwa wananchi lenye kipenyo cha milimita 450 na urefu wa kilomita 7.058; ufungaji wa pampu tatu zenye uwezo wa kusukuma mita za ujazo 175 kwa saa; ununuzi ya bomba za kusambaza maji kilomita 44.3 na ununuzi wa vifaa vya kutendea kazi.

Habari Kubwa