Corona ilivyogharimu maisha ya madaktari

14Oct 2021
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Corona ilivyogharimu maisha ya madaktari
  • RIPOTI MAALUM Madaktari watoa ushuhuda corona *Matabibu waliougua watoa ushuhuda *Daktari ICU Muhimbili aona shida bima

"ASIKWAMBIE mtu, ugonjwa huu ni hatari! Yaani unaumwa bila kujua utapona au la," Dk. Elisha Osati anakumbuka madhila wanayowapata madaktari baada ya kuambukizwa virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Uviko-19.

Daktari huyo wa magonjwa ya ndani ikiwamo moyo na mapafu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), anasema licha ya kwamba anatumikia taaluma hiyo, mara zote wao ndio wenyeji wa corona, ana mengi zaidi ya haya.

Dk. Osati ambaye pia ni Rais mstaafu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), anauogopa ugonjwa huo na ameshuhudia kwa kina madhila yake kutoka kwa wagonjwa wake ikizingatiwa huduma yake kuu inapatikana walipo wagonjwa mahututi, maarufu ICU.

Kwake unapomtajia maradhi ya corona kuanzia wimbi la kwanza, lilimuumiza na matabibu wenzake huku kukiwa na hisia za simanzi kutokana na baadhi yao kufariki dunia na yeye akiwa ni miongoni mwa waliougua, akishuhudia awamu ya pili aliyougua, "lakini Mungu ni mwema yakapita hayo".

Si kwamba anashabikia chanjo, bali ni mtetezi mkubwa na alionekana kwenye orodha ya mwanzo kabisa waliokuwa kwenye foleni ya kutaka kuchanjwa mara tu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuweka wazi utaratibu umeanza nyumbani.

Dk. Osati ambaye pia ni mtafiti na mhadhiri katika Chuo cha Utafiti na Tiba (MUHAS) anasema Februari mwaka huu baada ya kugundua amepata maambukizi, alijitenga na haikuwa rahisi kwake kwa sababu alilazimika kukaa mbali na mke, watoto na waliomzunguka mpaka alipopona.

Akiwa mwathirika wa janga hilo, anasimulia madhila yaliyompata kwa kusema: "Asikuambie mtu, ugonjwa huu ni hatari! Yaani unaumwa bila kujua utapona au la.

"Halafu kisaikolojia unaathirika zaidi hasa tunaokaa na wagonjwa wakati wote unakuwa unafahamu dalili zote, mawazo ni mengi, unawaza ugonjwa wenyewe, hatua utakazozipitia kipindi cha kuugua kuanzia za awali hadi mwisho."

Daktari huyo ambaye ni mchambuzi wa masuala ya tiba, anasema wakati wa mlipuko wa kwanza wa corona ulioripotiwa nchini Machi 16 mwaka jana, alishuhudia watumishi wenzake walioupata ambao waliugua na wengine kupoteza maisha.

"Niliona watumishi wenzangu walipata ugonjwa wa corona na wakaugua sana na wengine wakafa, wengi walikuwa ni vijana. Kwa kweli ni hali fulani ambayo ni ngumu kidogo, kwa waliougua watanielewa," anasema.

ATHARI KIUCHUMI

Dk. Osati anasema unapougua Uviko-19, mbali ya kupata athari za kiafya, pia unaathirika kiuchumi kwa kulazimika kutumia fedha kupata matibabu badala ya fedha hizo kutumika kwa ajili ya kuendesha familia.

"Hata kama una bima bado kuna gharama ambazo unaingia au familia itaingia au serikali itaingia. Kwa ujumla gharama ni kubwa kumuudumia mtu mwenye corona. Ukipata corona alafu ukaanza kukohoa, hewa inabana huwezi kupumua, kichwa kinauma, mwili unauma kwa kweli ni hatua ambayo haielezeki," anasema.

Dk. Osati anapaza sauti watumishi wa kada hiyo iwe ni lazima kukatiwa bima ya afya, akibainisha kuwa bima aliyonayo ni ya kawaida, sawa na watumishi wenzake wengi.

"Sina bima ya maisha, hata wenzangu wengi hawana na kwa bahati mbaya watu bado hawajaielewa bima ya maisha na kampuni za bima hawajajua hilo ni eneo ambalo linatakiwa kuwekeza zaidi kwa kuelimisha na kuhamasisha watu kuzikata," anashauri.

Anasema kutokana na hali waliyopitia na wenzake, wameamua kutafuta namna ya kupata bima ya maisha kwa sababu wanafanya kazi kwenye mazingira yenye hatari nyingi.

"Binafsi ninawaona wagonjwa wa corona na ninafanya kazi kwenye kitengo cha moyo na mapafu na Chumba Maalum cha Wagonjwa wa Uangalizi Maalum (ICU), ambako kuna wagonjwa hao sana.

"Huwa ninawafanyia vipimo vya moyo kadri wanavyokuja, athari ni kubwa. Kuna wenzangu ambao niko nao kwenye idara moja waliugua zaidi, wanatumia oksijeni na gesi hiyo kwa sasa imekuwa shida kidogo, kwa ujumla ni hali ambayo ni ngumu na inaogopesha," anasimulia.

Anakumbuka mwaka jana ugonjwa huo uliporipotiwa nchini kwa mara ya kwanza na kusimulia kuwa baadhi yao baada ya hofu, walipatwa na woga na kukimbia lakini kadri siku zinavyokwenda wakajifunza zaidi namna ya kujikinga.

KINGA YA BARAKOA

Dk. Osati anataja barakoa kama mkombozi mwingine kwao, akisisitiza kuwa imekuwa kinga kubwa kwao na wameona namna ilivyosaidia na maambukizi ya corona.

Wakati mtaalamu huyo akiitaja barakoa, mtaani zinauzwa kati ya Sh. 500 hadi 1,000 kulingana na ubora -- zipo zinazotengenezwa kiwandani na zile za kushonwa mitaani.

"Barakoa na kunawa kila wakati, matumizi ya vitakasa mikono, kwa sababu tunahudumia wagonjwa na mara zote tunakutana nao uso kwa uso, barakoa zimekuwa zikitusaidia kwa kiwango kikubwa," Dk. Osati anasema na kuongeza:

“Katika wimbi la kwanza la corona la mwaka jana, hospitali yetu (Muhimbili) tulikuwa na wafanyakazi zaidi ya 200 waliokuwa wamelazwa kwa wakati mmoja.

"Hata hospitalini ilishindikana ikabidi wakalazwe hospitali za wanafunzi kule Chole Road. Hao wote walikuwa wanaumwa na wanatumia oksijeni," Dk. Osati anasema.

Anasimulia kuwa baadhi yao walipata nafuu na wengine wachache walifariki dunia na katika hilo walijifunza barakoa inasaidia, hivyo kwa sasa wanavaa muda wote wakiwa kazini au katika mazingira yenye mikusanyiko.

WASIWASI NYUMBANI

Ili kuzikinga familia zao dhidi ya baa hilo, Dk. Osati anasema anachofanya na matabibu wenzake ni kuhakikisha wakiwa kazini au kwenye mikusanyiko, wanachukua tahadhari zote ikiwa ni pamoja na kujisafisha vizuri kabla ya kurejea nyumbani na kubadilisha nguo na barakoa.

"Kwa sababu ninaona wagonjwa wa corona, lazima nichukue tahadhari zote niwapo kazini ili niwe salama ninaporejea nyumbani.

"Imekuwa ni utamaduni wangu kila siku ninapomaliza kazi nguo ambazo nimezivaa ninazivua kazini na kuvaa nyingine. Ninajisafisha vizuri, ninavaa barakoa mpya na kabla ya kuingia kwenye gari, ninahakikisha sanitizer (kitakasa mikono) inahusika, angalau hapo ninakuwa nimeondoa wasiwasi.

"Nyumbani kwangu lazima kunawa, ninahakikisha nguo nilizotoka nazo kazini ninaziweka pembeni na kujisafisha ndipo ninakutana na familia yangu. Utamaduni huu nimejiwekea baada ya athari tulizozipata na wenzangu," Dk. Osati anawasilisha.

CHANJO YA CORONA

Dk. Osati anasema baada ya serikali kuridhia chanjo na kuipokea Julai 24 mwaka huu, alikuwa miongoni mwa watu wa awali kuchanjwa.

"Watu wengi siyo kwamba wanapinga chanjo lakini ni wasiwasi tu kulingana na maneno yaliyotoka kwenye mitandao, kiujumla Watanzania siyo kwamba wanapinga chanjo, wataipokea tu taratibu.

"Ilipoingia nilichanja mapema sana na hii ilinisaidia na imenijengea kujiamini zaidi kuwahudumia wagonjwa, watu wengi wa afya wamechanja, inawezekana kuna baadhi bado wana wasiwasi kidogo kama ilivyo kwa watu wengine.

"Endapo watu wengi watachanja, watatupa kujiamini zaidi, kwa sababu hawajachanja, tunawahudumiwa kwa tahadhari kubwa kwa kufuata miongozo ya kujikinga na magonjwa ya kuambukiza," anasema.

Anabainisha kuwa wapo watumishi wa sekta ya afya ambao ni madaktari wamefariki dunia, wamefiwa na ndugu zao na mmoja wao alipofiwa na wanafamilia sita ndani ya wiki moja kutokana na maradhi ya Uviko-19.

"Madaktari, watumishi wa sekta ya afya ndiyo tunaowahudumia siku zote, tunachowaambia wachanje, sisi tumechanja, chanjo ni salama sana, tumechanja hatujaona madhara yoyote yaliyotutokea, pia tunaelewa kama hujachanja madhara ni makubwa. Corona inaleta madhara makubwa," anasisitiza.

AJITOSA UTAFITI

Mtaalam huyo wa afya anasema amelazimika kufanya utafiti wa janga la corona ili kubaini athari zake.

“Nilikuwa ninafanya utafiti kwenye TB (Kifua Kikuu), moyo na mapafu lakini kwa sasa kwenye PhD (Shahada ya Uzamivu) utafiti wangu umelenga kuangalia madhara ya muda mrefu ya corona ambayo mpaka sasa utafiti unaonyesha ni makubwa, utafiti umeonyesha wagonjwa waliopata corona kali wanapata kitu kinaitwa pafu kutengeneza kovu.

Anafafanua zaidi kuwa" Kwa sababu wadudu wanapoingia mwilini kupitia kwenye pua, baadaye kukimbilia kwenye mapafu, mapafu yanakuwa ni uwanja wa mapambano kati ya mdudu na kinga za mwili, mapafu yametengezwa na mifumo midogo midogo inayobeba hewa.

"Baada ya kupata corona inaleta madhara na mtu anakuwa hana uwezo wa kubeba hewa, anabeba kwa kiasi kidogo kwa sababu yameharibika, hivyo yanabeba hewa kwa kiasi kidogo. Tuna wasiwasi pia corona inaweza kuleta madhara kwenye vina vya uzazi."

RAIS WA MAT

Rais wa MAT, Dk. Shadrack Mwaibambe, anashuhudia alivyougua corona katika wimbi la pili na kulazimika kujitenga nyumbani kwake kwa muda wa wiki tatu.

"Nilikaa nyumbani kwa muda wa wiki tatu. Bahati nzuri mke wangu ni daktari, akawa ananihudumia. Kuna mambo mengi ambayo ni sintofahamu.

"Pamoja na kuugua, niliendelea kulala kitanda kimoja na mke wangu lakini mke wangu hajaugua."Niliona wanandoa wengi akiwamo... (anamtaja mmoja wa maprofesa na hospitali anayofanyia) aliyeugua corona, akalala wiki tatu na alikuwa anakwenda kuhudumiwa na mke wake ambaye alikuwa havai barakoa wala glovu, chumba kimoja, mke wake hakuugua."

Dk. Mwaibambe anasema aliugua wakati yuko likizo na muda wa kutakiwa kazini ulipowadia, ilibidi aongeze wiki nyingine nyumbani ili kuhakikisha hapeleki ugonjwa kwenye eneo lake la kazi.

"Nilipopata corona, kitu kikubwa nilichoondoa na mke wangu ni ile hofu, tulihakikisha hofu haipati nafasi, hivyo tuliendelea na maisha kama kawaida, hii ilitusaidia sana.

"Watu wafahamu kwamba kuna watu asilimia 80 wanaweza kupata corona na wala asiwe na dalili na wengine asilimia 15 wakaugua na kwenda hospitalini, ninajiona nipo miongoni mwa asilimia 15 na mke wangu yawezekana alikuwa miongoni mwa hao asilimia 80, wanaupata lakini wanaendelea na maisha yao.

"Hii ilikuwa mara ya kwanza kwangu kuugua na kulala nyumbani kwa muda mrefu namna hii tangu mwaka 1993 nilipoumwa malaria nikiwa darasa la saba," anafafanua.

MTIKISIKO WIMBI LA PILI

Dk. Mwaibambe anasema wimbi la kwanza la corona lililoripotiwa Tanzania Machi 16 mwaka jana, lilisababisha hofu kwa madaktari wengi kutokana na kutokuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu ugonjwa wenyewe.

"Kama unakumbuka, dunia nzima ilikuwa na taharuki. Hata pale ulipojaribu kutafuta takwimu mtandaoni hazikuwa nyingi, sehemu kubwa kwa madaktari ilikuwa ni hofu kujua unasambaa kwa njia gani."Katika wimbi la kwanza, uvaaji wa madaktari hata wale waliokuwa wanakwenda kuzika waliofariki dunia tulishuhudia maziko yakifanyika usiku, wazikaji walivaa kama mtu anakwenda mwezini, mwili mzima ukiwa umefunikwa.

"Hofu ya namna hii ilichangia watu washindwe kuhudumia wagonjwa, kwa sababu wakati ule tulikuwa hatuna vifaa vya namna hiyo, hivyo ilikuwa huwezi kumgusa mgonjwa."

Dk. Mwaibambe anasema ilipotokea daktari ameingia kwa mgonjwa na kumgusa, hofu iliongezeka zaidi na wengi waliogopa kurudi nyumbani wakihofia kupeleka maambukizi kwenye familia zao.

"Ninakumbuka madaktari wengi walikaa karantini (kujitenga), walikuwa hawaendi nyumbani kukutana na familia zao kwa sababu tu ya hofu ya kumgusa mgonjwa wa corona.

"Wapo wengine walikwenda mbali zaidi, hata viatu walivyokuwa wakivaa waliona walikokanyaga labda wameondoka na mdudu," anasimulia.

Rais huyo anasema kadri elimu ilipotolewa zaidi na wao wakafahamu kuwa wanaweza kuwahudumia wagonjwa kwa kuchukua tahadhari za maambukizi, hofu hiyo ilizidi kupungua.

Tatizo lingine analitaja kuwa, katika wimbi la kwanza la corona, wengi waliamini wagonjwa hao wanatakiwa kuhudumiwa na hospitali kubwa kama Muhimbili, Bugando, KCMC lakini kadri siku zilivyokwenda, ikabainika hata zile za kawaida wahudumu waliopo huko wanaweza kuwadumia.

"Corona haina dawa, kinachofanyika ni kutibu dalili, mfano mgonjwa anakuja na homa kali, unampa dawa za kuishusha.

"Vilevile, kwa sababu kuna kuwa na maambukizi, utampatia dawa za 'antibiotics' ambazo kila mtaalamu wa afya anaweza kufanya," anasema.

Dk. Mwaibambe pia anasema kuwa kutokana na ugonjwa huo kutoeleweka vizuri katika siku za mwanzo, idadi kubwa ya magari ya kubeba wagonjwa (ambulance) ilionekana mitaani, kitendo ambacho anakitafsiri kuwa kilisababisha hofu zaidi hasa ile milio ya mara kwa mara barabarani iliyokuwa ikisisika.

Anabainisha kuwa madaktari walipitia katika kipindi kigumu wakati wa wimbi la pili, akifafanua kuwa daktari alikuwa achukua vipimo kwa mgonjwa lakini majibu ya nini mgonjwa huyo anaugua, yalikuwa hayarudi kwao.

Katika hilo, Rais wa MAT ana ufafanuzi zaidi kwamba: "Hii ilikuwa changamoto kubwa kwa daktari katika utendaji kazi, ili kugundua tatizo linalomsumbua mgonjwa, daktari hutakiwa kuchukua historia ya mgonjwa, hufanya uchunguzi wa vitendo na ukishaandika maelezo ya ugonjwa unaouhisi utamwandikia vipimo, akipimwa ndipo unabaini tatizo lake.

"Hiki kipengele cha mgonjwa anaumwa ugonjwa gani ndiyo ilikuwa changamoto kwa madaktari, unachukua vipimo, majibu hayaji kulingana na mtazamo wa serikali kipindi hicho.

"Kwa hiyo katika matibabu yetu na elimu tuliyoipata katika wimbi la pili, hii ilikuwa ni changamoto kubwa kulinganishwa na mawimbi yote ya corona."

Kiongozi huyo wa MAT anaweka wazi kuwa wapo matabibu waliugua na kufariki dunia kutokana na maradhi ya Uviko-19, lakini hakuwa tayari kuanika takwimu halisi kutokana na miiko ya kitabibu na itifaki iliyopo.

"Ukimwangalia mgonjwa, unaona anaugua corona lakini huna ushahidi wa majibu, kuna madaktari na watumishi wa afya walifariki dunia baada ya kuugua, lakini ulikuwa huwezi kusema kafa kwa sababu ya corona, kwa sababu huna ushahidi, na ukisema ni corona na huna ushahidi unaweza kushtakiwa," anabainisha.

Kuhusu taarifa za baadhi ya watumishi wa afya kukimbia, Rais huyo anasema hazikumfikia, lakini anachojua miongoni mwao walichukua likizo ambazo ilikuwa siyo rahisi kujua zilikuwa ni za mwaka au kukwepa kuhudumia wagonjwa Uviko-19.

"Mtu akichukua likizo, huwezi kusema 'ninachukua kwa sababu ya jambo hili', ila unaweza kuhisi tu amechukua ili hili lipite. Suala lililojitokeza lilikuwa ni kwenye hospitali ndogo ambazo zilikuwa zinakataa wagonjwa, wakiuliza ana shida gani na wakaambiwa 'tatizo la kupumua', walikuwa hawawataki," anasema.

Kiongozi huyo wa MAT anaunga mkono hoja ya wataalamu wa afya kuwa na bima ya maisha kutokana na mazingira ya kazi yao.

"Wengi wanapendekeza bima ya maisha, wanataka mwajiri ndio awalipie iwe mbali na mshahara, lakini mwajiri akisema hapana na wakiambiwa wakatwe katika mshahara, mtu anaona utapungua, anakataa.

"Nchi zilizoendelea kuna kitu kama hiki -- bima ya maisha, ila kama kuna madaktari wanataka wajitokeze, wapendekeze utekelezaji wake uweje ili lipelekwe kwenye mamlaka husika.

"Muhimu kwa sasa tuchanje. Unarudi nyumbani unakutana na mke, mume, bibi, babu, mama, baba na watoto, tuwe mstari wa mbele kupata chanjo na tuwaelimishe wananchi kuwa chanjo ni salama.

"Maeneo walikochanja watu wengi, maradhi yamepungua, ukiangalia nchi ambazo bado wanaugua na kupoteza maisha ni zile ambazo hawakuchanja.

"Mwisho wa siku likija wimbi lingine la nne, wanataaluma tutakuwa hatuna sababu ya kwenda kulalamika. Mfano mtu anaugua halafu hajachanja, maana yake taaluma yake haijamsaidia, mambo sijui eti nguvu za kiume ni uongo mtupu, tuchanje.

"Bahati mbaya katika wimbi la tatu kirusi kimekuja vibaya kama vile kimebadilika, hatukuambiwa kama tunakabiliana na Delta lakini kirusi kimeonekana kina makali, kinaeneza ugonjwa kwa haraka na kuua," anahadharisha.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani na Damu kwa Watoto wa MNH, Khadija Mwamtemi, anasema katika kitengo chao hicho wamehakikisha hakuna maambukizi ya corona.

"Mgonjwa wa saratani kinga zake zipo chini. Kwa hiyo wodi yangu tunawakinga na maradhi haya, tunahakikisha wazazi au walezi wanaokaa na watoto wodini wanachukua tahadhari zote ikiwamo uvaaji wa barakoa.

"Mtoto tunapomuona ana dalili anakohoa, labda oxgeni tunapima inashuka, tunatenga na kuwafanya vipimo kujiridhisha siyo yenyewe. Kwa kweli tumejitahidi kuwakinga na janga hili," anasema.

UONGOZI MUHIMBILI

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa MNH, Aminiel Aligaeshi, anabainisha kuwa hospitali hiyo ya ngazi ya juu zaidi nchini inafuata na kutekeleza mwongozo uliotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kukabiliana na virusi vya corona.

"Hospitali inafuata miongozo yote iliyotolewa na serikali na WHO (Shirika la Afya Duniani) ili kuwakinga watoa huduma na wanaohudumiwa, ndiyo maana kwa nyakati mbalimbali tumekuwa tukisikitiza uvaaji wa barakoa kwa wafanyakazi na huwa tunasisitiza wakati mwingine mtu asimguse mgonjwa bila kuvaa barakoa na hili linaendelea kusisitizwa mpaka sasa," anasema.

KAULI YA SERIKALI

Nipashe inatua mezani kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya anayeshughulikia Idara Kuu Afya, Prof. Abel Makubi, kupata undani wa kinachowasibu madaktari kipindi hiki cha corona, lakini kiongozi huyo anaelekeza majibu yatolewe na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Aifello Sichalwe.

Katika ufafanuzi wake, Dk. Sichalwe anasema ugonjwa wa corona unaathiri watu wote katika kila eneo."Ugonjwa huu unaenezwa kwa njia ya hewa hivyo mtu yeyote anaweza kuupata. Ili kuwalinda watumishi wa afya, serikali imehakikisha vifaa vya kujikinga na maambukizi vinapatikana katika maeneo ya kutolea huduma na watumishi wanavitumia.

"Pia mafunzo kwa watumishi yanatolewa ya namna ya kuhudumia wagonjwa huku wakizingatia afua zote za kinga. Kwa kuzingatia haya, serikali imeweza kuwalinda watumishi wake."Dk. Sichalwe pia anasema fursa ya kuchanja ambayo watumishi wamepewa kipaumbele, ni njia mojawapo ya kuhakikisha wanakingwa dhidi ya corona.

KUHUSU CORONA

Virusi vipya vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Uviko-19, viligunduliwa Novemba 2019 huko Wuhan, China na kwa Bara la Afrika mgonjwa wa kwanza raia wa kigeni aligundulika Misri.

Machi 16 mwaka jana, Tanzania ilithibitisha mgonjwa wa kwanza wa corona jijini Arusha ambaye aliwasili kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akitokea Ubelgiji.Msafiri huyo raia wa Tanzania aliondoka nchini Machi 3 mwaka jana na kati ya Machi 5 na 13, alitembelea nchi za Sweden na Denmark na kurudi tena Ubelgiji.

Siku iliyofuata, yaani Machi 17 mwaka jana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alitangaza kufunga shule zote za awali, msingi na sekondari hadi kidato cha sita na baadaye vyuo vikuu kwa muda wa siku 30.Kwa mujibu wa WHO, idadi ya wagonjwa wa corona duniani hadi wiki iliyopita, ni watu milioni 2.58 (takwimu halisi 2,258,909) na vifo vilifikia watu 154,388 huku Marekani, Italia, Hispania na Uingereza zilitajwa kuongoza kwa idadi ya wagonjwa na vifo.

Katika taarifa yake wiki iliyopita, Waziri Afya, Dk. Dorothy Gwajima, alibainisha kuwa idadi ya waliopata maambukizi ya virusi vya corona nchini ilifikia watu 25,957 huku vifo vikiwa 723.