DC Busega ‘anyunyiza’ simulizi ya wanavyokwea kupitia ‘hapa kazi’

29Nov 2019
Anthony Gervas
Mwanza
Nipashe
DC Busega ‘anyunyiza’ simulizi ya wanavyokwea kupitia ‘hapa kazi’
  • Aibua ombi ‘utumbuaji’ ufike chini yao

BUSEGA ni miongoni mwa wilaya tano zinazounda Mkoa wa Simiyu. Zingine ni Bariadi, Meatu, Maswa na Itirima. Kabla, ilikuwa jimbo la uchaguzi la Busega Vijijini, katika Wilaya ya Magu, Mkoa wa Mwanza.

Mkuu wa Wilaya Busega, Tano Mwera.

Wilaya hiyo ilianzishwa mwaka 2012,katika kipindi ilipoanzishwa mikoa mipya mbalimbali nchini. Katika uhai wake mpya, sasa inajigamba kuwa katika serikali ya awamu ya tano ya Rais, Dk. John Magufuli, ikipiga hatua kutekeleza miradi mingi ya maendeleo ya wananchi kwa mafanikio.

Kihistoria, ni wilaya pekee kutoka mkoa Mwanza, kuunda Simiyu, zilizobaki zinatoka mkoa Shinyanga.

Hadi sasa Busega, kwa mujibu wa Sensa ya Mwaka 2012, ina wakazi 203,597 ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 2,129, asilimia 28 ikiwa ni maji sehemu kubwa ni Ziwa Victoria na inapakana na Mkoa wa Mwanza, ikiwamo kisiwa Ukerewe na wilaya Serengeti, mkoa Mara.

ORODHA MAENDELEO

Shughuli kuuza kiuchumi kwa wananchi hao ni kilimo, ufugaji, uvuvi pamoja na biashara, huku Mkuu wa Wilaya, Tano Mwera, anasema kuna ushuhuda wa kasi ya maendeleo na uchumi kutokana na kasi ya miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi, kwenye maeneo kama afya, elimu, kilimo, maji na uboreshaji miundombinu ya barabara.

Mkuu wa Wilaya ya Busega Mwera, alipozungumza na Nipashe ofisini kwake wiki hii, anataja miradi ya ufugaji samaki aina ya sato kupitia mabwawa maalumu, kwa ajili ya kuongeza tija katika wilaya.

“Wakati mimi nikiteuliwa na kuwa Mkuu wa Wilaya ya Busega mwaka 2016, maendeleo ya wananchi yalikuwa chini sana kuliko sasa hivi,” anafafanua na kuendelea: “Masuala ya uwajibikaji yanatekelezwa katika sekta zote za umma, wananchi wanahudumiwa bila kuzungushwa.”

Mwera anasema, katika utekelezaji sera za maendeleo ya wananchi, huduma bora sasa zinatolewa katika sekta mbalimbali ikiwamo afya, elimu, kilimo, maji, ujenzi wa miundombinu ya barabara.

Mkuu wa Wilaya anaanza na sekta ya afya, kwamba kuna miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa na kwa sasa kuna ujenzi wa hospitali ya wilaya iliyofikia hatua za mwisho kukamilika, ikigharimu kiasi cha Sh.bilioni 1.5.

Anasema, wanachokisubiri sasa ni kuongezewa fedha na serikali kuu, kiasi cha Sh.milioni 500 kinachohitajika kwa ajili ya kukamilishia vifaa vya kutoa huduma na kwamba, hospitali hiyo inatarajiwa kuanza kutoa huduma rasmi mwaka ujao.

Pia anaunganisha hoja hiyo na kuboresha vituo vya afya viwili vya Igalukilo na Nassa, vinavyotoa huduma za upasuaji wagonjwa, huku kukikarabatiwa Kituo cha Afya Lukungu ambacho baadaye kitaanza kutoa huduma za upasuaji na kuna Kituo cha Afya Kiloleli anachosema kinaboreshwa.

Mwera anasema, walipata ufadhili kutoka wa Mradi wa Lipa kwa Ufanisi (BRF), kwa ajili ya kusaidia ukarabati wa zahanati na vituo vya afya, ambavyo kila moja kilipewa fedha Sh. milioni 10.

Anaoanisha hilo na bajeti yao ya upatikanaji dawa katika zahanati na vituo vya afya kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD), anayoitetea kwamba inaridhisha na haina malalamiko, kama ilivyowahi kuwapo awali.

Katika kufanikisha hilo, mkuu wa wilaya anawahamasisha wananchi kujiunga na Bima ya Afya iliyoboreshwa (CHF), ili kinamama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano, wapate huduma ya matibabu bure.

“Dawa muhimu zote zinapatikana kwa wagonjwa,sisi wilaya yetu hatuna shaka na hilo,” anasema.

HUDUMA MAJI

Mkuu wa Wilaya anasema utekelezaji wa miradi ya maji katika Kata ya Kiloleli, umekamilika na utagharimu kiasi cha Sh.bilioni 1.6 mradi wa Kata ya Nyashimo katika makao makuu ya wilaya hiyo nao unaendelea kutekelezwa kwa gharama ya Sh. bilioni 1.8.

“Upo mradi mkubwa zaidi wa maji unaojengwa katika kata ya Lamadi, ambao utahudumia kata nzima na vijiji vingine vya jirani, utakaogharimu kiasi cha Sh. bilioni 12 unaofanyiwa majaribio sasa.

Unakisiwa kuhudumia zaidi ya kaya 33,000 ifikapo mwaka 2030, kadri watu wanavyozidi kuongezeka,” anasema Mkuu wa Wilaya Mwera.

ELIMU IMEKAAJE?

Katika elimu, Mwera anaanza na taarifa ya kiwango cha ufaulu kilichoongezeka mwaka jana, kufika zaidi ya asilimia 70 na mwaka huu 2019 imekwea zaidi hadi asilimia 90 ya wanafuzi wote wa shule za msingi, kukiwapo wanafunzi wanne walioingia katika kundi la ‘kumi bora’ za wanafunzi kujiunga sekondari kutoka shule za msingi.

Anasema kupanda kiwango cha ufaulu huo, umeleta chachu kwa watoto kuandikishwa shule za msingi, kutokana na sera iliyopo ya’ elimu bure’ ambayo katika sura ya pili, inachangia ongezeko kubwa la wanafunzi shuleni na kuangukia shida ya upungufu wa vyumba vya madarasa.

Mkuu wa Wilaya anasema, malengo yao katika wilaya mwaka uliopo wa fedha ni kujenga zaidi shule za sekondari kila kata, kutoka moja hadi shule tatu, ili kuondoa changamoto za wanafunzi wanaofaulu darasa la saba kuingia sekondari wasikose nafasi, katika wilaya hiyo yenye kata 15.

Mkuu huyo wa Wilaya, anasema mwaka juzi walijenga shule za sekondari tatu, anazozitaja kuwa: John Mtaka, Dk. Chegeni na Masanza Kona na mwaka jana zilijengwa sekondari mpya mbili ambazo ni Nyamikoma na Gininiga.

MIRADI BARABA

RA Anaeleza kuwa, barabara ndani ya wilaya hiyo zimejengwa na kuunganisha kata moja na nyingine, chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura).

“Makandarasi waliokuwa ‘makanjanja’ katika halmashauri za wilaya sasa hawapo tena, baada ya serikali kubadilisha mfumo wa usimamizi wa barabara hizo na kuwapa Tarura. Ndiyo maana, barabara zinajengwa kwa kiwango kinachotakiwa na haraka.

“Mikataba ya ujenzi inasimamiwa na mkoa na kupewa tenda makandarasi wenye sifa. Sio mtu anabeba begi tu na makaratasi anapewa tenda ya kujenga barabara, hana hata vifaa vya ujenzi. Hivi sasa mpaka awe na vigezo,” anasema Mwera.

Anafafanua kwamba kabla ya Tarura kupewa usimamizi, kuna wanasiasa na watendaji waliochukua tenda za ujenzi kwa maslahi yao binafsi, jambo lililoleta mvutano na changamoto nyingi katika kuwafikishia huduma muhimu wananchi wake.

Mkuu wa Wilaya anasema, pia sasa wanaendelea kupambana na uvuvi haramu wa kutumia zana zilizozuiliwa na serikali kutumika kuvulia samaki wadogo, hivyo wanawachukulia hatua za kisheria.

Mkuu huyo wa wilaya, anajigamba kuwa miradi yote inasimamiwa vyema sasa pasipo ubadhirifu na anatumia uthibitisho wa mwenge wa uhuru ulipozuru hapo mwaka huu, wakimbizaji walikagua miradi hiyo na hapakuwapo miradi chini ya viwango na kukataliwa.

Mwera anahitimisha kwa kumpongeza Rais Dk, Magufuli na kutoa rai ya kuwapo watendaji wa ngazi za chini yao wakuu wa wilaya, akiwatuhumu wanakwamisha shughuli zingine za maendeleo.

Anafafanua, bila ya kutaja vyeo vya wanaotuhumiwa, akisema: “...watendaji wanaotukwamisha sisi wa juu na kusababisha sisi tunafanya kazi kwa ‘presha’ kubwa, nao tunaomba wawajibishwe kwa haraka, kama ilivyo kwetu”

•Mwandishi wa makala hii anapatikana Kanda Ziwa, kwa barua pepe; [email protected], Simu (+255) 0682 86 92 44.

Habari Kubwa