Ijue siri ya Kagera kung’ara unyonyeshaji vichanga

15Oct 2020
Jaliwason Jasson
Bukoba
Nipashe
Ijue siri ya Kagera kung’ara unyonyeshaji vichanga

JAMII inapaswa kutafakari hiari ya unyonyeshaji watoto bila lishe mbadala ndani ya miezi sita. Hata hivyo inaelezwa hilo limeshindikana kutekelezwa vyema.

Mkoa wa Kagera una rekodi inayokinzana na hilo, kwani unang’ara katika unyonyeshaji watoto, kuanzia wanapozaliwa hadi umri miezi sita ya awali.

WATAALAMU LISHE

Takwimu za mwaka 2018 zinataja asilimia 96 ya watoto wanaonyonya ndani ya saa moja ni asilimia 97 na wananyonya kwa miezi  sita ni asilimia 86, huku walionyonya kwa miaka miwili ni asilimia 44.

Mtaalamu lishe anayejitambulisha kwa jina Hamis, anasema mbinu wanayoitumia ni utoaji elimu kupitia vyombo vya habari vya kijamii na kitaifa, kuifunza umma ubadilike, ili mkoa upige hatua katika unyonyeshaji.

Kiongozi huyo anataja mbinu nyingine, wahudumu wa afya ngazi ya jamii hupeleka elimu kwa walengwa  kinamama wanaonyonyesha na wajawazito na kuhakikisha vituo vya afya vinavyotoa huduma  vina wataalamu wanaosaidia elimu ya unyonyeshaji kwa kipindi hicho wajawazito wanapohudhuria kliniki.

Aidha, Hamis anasema kuna mikataba kati yao na maofisa watendaji kata, vijiji na mitaa wanaokuhakikisha kila mama uhudhuria kliniki, anapata elimu ya unyonyeshaji na namna ya kuandaa chakula lishe.

Kimsingi, ni mkakati wa mabadiliko chanya unaochangia mkoa kufanya vizuri kwa watoto wenye umri chini ya miezi sita na waliovuka.

“Tunaangalia kijiji ambacho kina hali mbaya na tunawapa vipimo na kuwapa elimu wazazi na watoto,” anaeleza Hamis, akisema wanafuatilia kila baada ya muda uliotengwa kama vile miezi sita na mwaka, kuona namna ya kuwasaidia wahusika. Mtaalamu huyo anasema unyonyeshaji ni suala la kisaikolojia na linatakiwa kuwekewa mazingira rafiki kwa mama ili kuepuka dai ‘maziwa hayatoki.’

MAZIWA YALIVYO

“Mtoto anapokuwa ananyonya ile sehemu ya titi nyeusi iwe ndani kwenye mdomo wa mtoto na mtoto  asishike  lile titi na tumbo la mama na la mtoto vigusane, ili apate lile joto la mama …mtoto akamate vizuri titi.”

Anafafanua kuwa, mtoto anapoikamata vizuri titi, kuna sauti itasikika, lakini asipokamata anaangukia kulia na ndio anaanza kumng’ata mama yake.

Hamis anasema maziwa ya mama yamegawanyika katika sehemu kuu mbili; maji na maziwa na mama anaponyonyesha anatakiwa amuweke mtoto kwenye titi moja mpaka ashibe, kwani kumbadilisha titi kunamfanya anyonye maji na siyo maziwa.

Anasema, mtoto anatakiwa anyonye kwa dakika 20 hadi dakika 30, huku mama asiwe anafanya suala jingine na mtoto anapomng’ata mama, ni ishara hapati maziwa vizuri na anatakiwa anyonye kadri anavyohitaji, asipangiwe usiku muda wa kunyonyesha. Mtaalamu huyo anapinga unyonyeshaji wa mazoea.

Mtoto anaponya anatakiwa ama kuimbiwa au kucheza ili kumpa furaha na kuufanya ubongo uchangamke kwa ajili ya kufanya utambuzi wa vitu mbalimbali.

Anashauri mama wanaonyonyesha kula makundi kadhaa ya vyakula akivitaja vyakula vya nafaka kama mahindi, mchele, mtama na ndizi mbichi; kundi jingine ni protini kama vile maharage, soya, maziwa, samaki na nyama. Makundi mengine ni mboga, matunda kama ndizi mbivu, maembe, papai, parachichi, pasheni; pia mwisho ni sukari mafuta na asali.  

WAZAZI WANYONYESHAJI

Nyangoma Busenene mkazi wa Kashai, anasema suala la kumnyonyesha mtoto ni baraka kwao na linakuza kiumbe, akitaja utamaduni wao unatilia maanani vyakula vinavyhoshauriwa kitaalamu na wazazi.

Busenene anasema vyakula hivyo ni vya kawaida na vinapatikana kwa gharama katika mazingira yao, akitaja mfano wa jamii ya nyanya chungu.

Mkazi wa Katoma, Asha Mussa, anasema kinachowasaidia katika unyonyeshaji bora ni kufuata ushauri wa wataalamu wa afya na lishe kliniki na mafunzo ya wazazi wao.

Kwa mujibu wa  Asha, elimu hiyo ni ya kurithishana vizazi, hivyo anayekiuka kwa makusudi haivumiliwi kijamii kwa ajili ya ustawi wa mtoto.

Mkazi wa Kastamu, Juster Rweyemamu, anaona chanzo cha mafanikio unyonyeshaji wa miezi sita mfululizo inatokana na mkoa huo kuwa na uhakika wa chakula. Juster, anataja ukaribu na Ziwa Victoria kunawapa lishe, pia mifugo ya kutosha nayo inawasaidia uhakika wa lishe hata kumudu unyoyeshaji.

Mkazi wa Kyakailabwa, Martha Bwenge, mwenye umri miaka 79, anakumbusha unyonyesha hauhitaji uzembe, kwani ndiko kwenye msisitizo wa wataalamu wa lishe na afya.

Bibi huyo anaungana na siri ya mafanikio ya mkoa wa Kagera, ni mila na desturi zikiwamo babu na bibi kuwaridhia watoto kukaa, hata katika hatua ya kuacha ziwa, mtoto anapokabidhiwa asubuhi mapema.

“Babu yake huwa anauliza kama mama yake  mjamzito hapo ndio anaweza kukubali mtoto aachishwe na umri uwe unaruhusu, lakini kama umri wake ni mdogo na mama hana matatizo ya kiafya anaambiwa asimwachishe,” anasema Bwenge.

Aidha, anasema sheria ndogo za ukoo wanazojiwekea zimesaidia kuepuka ukiukaji maadili, hata kushindwa kuwanyonyesha watoto kwa kipindi cha miezi sita bila kumpa chochote.

George Mulokozi anachangia kinachosaidia ni kutii kanuni afya, kujua na kuheshimu wajibu wa kumtunza mtoto, baba na mama wakisimamia kikamilifu unyonyeshaji wa miezi sita ya awali, pia kwa mtoto siku ya kwanza. Frank Byamungu, anahusisha uzembe katika unyonyeshaji unaweza kuwagharimu wazazi wote wawili.  

MIKAKATI GANI?

Nipashe ilidokezwa, Kamati ya Lishe Mkoa Kagera, hufanya vikao kila baadaye ya robo mwaka, chini ya uenyekiti wa Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), wakiwa na mkakati wa bajeti kumtengea Sh. 1,000 kwa kila mtoto.

Pia, wanashirikiana na wadau kufanya urutubishaji wa vyakula vya lishe hasa unga wa lishe ambao utakuwa na mchanganyiko wa makundi yote vyakula.

Mratibu wa Huduma ya Mzazi na Mtoto Mkoa wa Kagera Neema Kyamba, anasema elimu ya unyonyeshaji kwa miezi sita ya kwanza, huwa wanawapatia wanawake wakiwa wajawazito na baada ya kujifungua ndani ya saa moja wanatakiwa kunyonyesha.

Aidha, anahimiza mama kumnyonyesha maziwa yake pekee, yakibeba mlo kamili na mtoto akiwa anaponyonya vizuri, hakuna haja kumpa kingine maana hakiongezwi chochote. Mratibu huyo anataja athari za kumnyima kunyonya ni kupata majipu, usaha na homa.

Anafafanua: “Na mama usipomnyonyesha mtoto unapata ujauzito kwa kuwa kunyonyesha ni njia ya asili ya uzazi wa mpango.

“Kunyonyesha kunajenga ukaribu na upendo unakuwapo mfano unapolala naye unasikia moyo wa mtoto unadunda,” anasema. Vilevile anasema, mtoto anaponyonya vizuri, unamfanya mama yake anaoisikia tumbo linauma kutokana na kurudi kizazi, lakini inaweza ikatulizwa na nyonyo.

WADAU 

Mratibu wa Shirika la Kikukwe Community Development Initiatives (KCDI), Christine Nyangoma, anaungana na wataalamu akiwa na hoja ya kitaalamu  wazazi wenye umri miaka 25 hadi 35 wananyonyesha katika namna isiyo sahihi wakiona ni ya kisasa, akiibatiza jina ‘kidotcom.’

Anatoa mfano wa mzazi anayenyonyesha, huku akipiga simu, jambo ambalo si sahihi. Nyangoma, anayefanya kazi wilayani Misenyi, Tarafa ya Kiziba, anachangia kilichoinua mkoa wa Kagera, kung’ara katika unyonyeshaji watoto wachanga katika miezi sita ya awali ni ukiitwa ‘Mradi wa Mtoto Mwerevu’ ulioanzia Misenyi mwaka 2015, sasa huko ngazi ya mkoa.

Anasema mnamo Oktoba 2017 walikuwa na walengwa watoto 10,000 katika siku 1000 walizojitengea, yaaani miaka miwili na miezi tisa, wakofikia mafanikio asilimia 86.2 mwaka 2018 na kitaifa asilimia 58.1.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria duniani asilimia 40 ya watoto wachanga chini ya umri wa miezi sita ndio wanaonyonyeshwa pekee, sababu zinazotolewa juu ya kasoro hiyo ni kazi, magonjwa na utamaduni.

Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), katika ripoti ya utafiti, watoto  na vijana wadogo walionyonyeshwa  wakiwa wachanga wana uwezekano mdogo wa kupungua uzito mwilini kupindukia.

Habari Kubwa