Ikungi katika maajabu makuu maboresho mradi elimu shuleni

04Jul 2020
Elisante John
Singida
Nipashe
Ikungi katika maajabu makuu maboresho mradi elimu shuleni
  • Darasa 7 wateleza kuiona sekondari

MPANGO wa kuinua ubora wa elimu nchini au Equip -Tanzania, ni mradi unaofadhiliwa na serikali ya Uingereza kupitia shirika lake la misaada (DFID-UKAID), kwa gharama ya zaidi ya Sh. bilioni 100.

Mratibu wa asasi ya Equip Tanzania wilayani Ikungi, Mwalimu Imani Maketa, akifafanua jambo ofisini kwake.

Ni mpango unaowezesha shule za msingi kuunda chombo cha ushirikiano kinachojulikana ‘Umoja wa Walimu na Wazazi’ (UWW), lengo ni kuimarisha uhusiano baina yao, ili kuinua taaluma na kumfanya mwanafunzi aelewe vyema anayofundishwa.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida, mpango unatajwa kutoa mchango mkubwa kitaaluma na inaongeza kasi kila mwaka, kutokana na shule kufanya vyema kwenye mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.

Ni hali inayowezesha shule za sekondari kufanya vizuri, kutokana na wengi wanaojiunga, kuandaliwa vyema.

Ofisa Elimu Msingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Gidion Kitoboli, akiwa kwenye shughuli zake. PICHA ZOTE: ELISANTE JOHN. 

 

Mratibu wa Equip-T, ambaye pia ni Ofisa Elimu Vifaa na Takwimu, wilaya Ikungi, Imani Maketa, anasema maeneo mengi yamefanyiwa kazi tangu mpango ulipoanza mwaka 2018 na kuwezesha elimu kukua wilayani.

Anataja baadhi ya maeneo, ni ufundishaji kwa walimu, uliowabadili wanafunzi wa darasa la pili na tatu kuelewa vyema utangulizi wa ‘KKK’; kusoma, kuandika na kuhesabu.

Maketa anasema, kabla mpango kuanza, ilikuwa kawaida mwanafunzi wa darasa la pili hadi tatu kushindwa kusoma.

Eneo lingine ni ufanisi wa waratibu elimu kata, maofisa elimu wilaya, wajumbe kamati za shule, wazazi na jamii wanaohudumia shule husika na wanafunzi na kuwandaa vyema wanaotarajiwa kuanza shule.

Pia, kuna wajumbe wa kamati za shule waliopatiwa mafunzo kuongeza ufanisi kazini, ili kuwa na mkakati wa pamoja wa wazazi na jamii husika, washiriki katika maendeleo ya shule na imeleta tija kwenye mradi.

 

DED

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi, anamshukuru Rais Dk. John Magufuli, kwa mapinduzi makubwa kwenye sekta ya elimu, hata thamani ya sekta hiyo inaonekana.

Anasema kupitia ‘Equip-T’ Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi imenufaika na zaidi ya Sh. bilioni 1.4 tangu programu ilipoanza kutekelezwa wilayani, Septemba 2018.

Kijazi anataja yaliyotekelezwa sasa ni ujenzi wa shule shikizi nne, ukarabati vyumba vya madarasa ya shule za msingi, mafunzo ya wawezeshaji vituo vya utayari, semina ya mafunzo ya jinsia na mafunzo ya ukusanyaji taarifa kwenye mfumo (SIS).

Wanafunzi wa shule ya sekondari, wilayani Ikungi. PICHA: MTANDAO

 

Anatumia fursa kuwahimiza wanafunzi kuhudhuria shule bila kukosa, akisema wamewezeshwa kujengwa vyumba vinane vya madarasa na samani zake, ofisi nne za walimu na matundu 24 ya vyoo.

Pia, kuna maboma sita ya vyumba vya madarasa yamekarabatiwa na kumenunuliwa samani katika shule tatu.

 

OFISA ELIMU

Ofisa Elimu wa Shule za Msingi Wilaya ya Ikungi, Gideon Kitoboli, anasema licha ya kuwajengea uwezo wa uongozi maofisa elimu kata na walimu wakuu, Equip-T  tangu ianze, imeshanufaisha zaidi ya walimu 650 kuwapa mafunzo, ili kuboresha utendaji darasani.

Pia, anasema kuna jumla ya wawezeshaji 62 waliopata mafunzo ya kufundisha kwenye vituo vya utayari, vinavyowandaa wanafunzi kuingia darasa la kwanza, wamepatiwa mafunzo kuendesha shule hizo.

Wahamasishaji jamii, wawili kila shule walipatiwa mafunzo kusimamia wanafunzi 1,200 waliotoka mbali na makazi, wamenufaika kupata nafasi  ya  kusoma kwenye shule shikizi nne, jirani na makazi yao.

“Kwa kweli naweza kusema mpango huu ni mzuri sana, umenufaisha watoto 3,528 waliokuwa hawawezi kwenda shule za awali kutokana na umbali, lakini waliandaliwa vituo 74 vya utayari vilivyopo maeneo mbalimbali ya wilaya yetu, na kusoma vizuri tu,” anafafanua Kitoboli.

Kitoboli anasema, kuna wanafunzi 270 waliokuwa wanabanana darasa moja, sasa wako huru, baada ya kukamilika vyumba vya madarasa katika maeneo yao.

Anataja pingamizi walio nayo ni ubovu wa miundombinu kwa baadhi ya maeneo, hali inayosababisha kusuasua mipango na mikakati ya elimu kutokamilika kwa wakati.

Ofisa Elimu huyo, anataja kukosekana usafiri wa uhakika katika Idara ya Elimu, inakwamisha ufuatiliaji shughuli za maendeleo na utekelezaji malengo maalumu waliojiwekea katika kuzifikia shule.

 

MSONGAMANO DARASANI

Kuhusu mafanikio, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Darajani, iliyopo kijiji cha Mkiwa, mpakani mwa Ikungi na Manyoni, Loth Ntandu, anasema shule yake imepunguza msongamano darasani na utoro, baada ya kugawanywa kutoka shule mama ya Mkiwa.

Anasema, wanafunzi hao wanafikia zaidi ya 360, wakwenda shule na kurudi nyumbani umbali wa kilomita 10, lakini baada ya jamii kuanzisha shule shikizi na Equip-T kujenga vyumba vya madarasa, itasajiliwa rasmi.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kiupuiko, Mariam Makerah, anasema mpango wa Equip-T, umewainua, kutokana na kuimarika chombo ‘Umoja wa Wazazi na Walimu” (UWW).

Anasema UWW ilianzishwa kupitia mradi wa EQUIP-T mwaka 2018, na umekuwa msaada katika kuimarisha taaluma shuleni hapo.

Mwalimu Mariam, anatoa mfano, kipindi serikali ilipofunga vyuo na shule nchini kutokana na tishio la ugonjwa wa corona, wazazi walilazimika kufanya kazi za shamba kupalilia alizeti na viazi vitamu kwenye shule yao, badala ya watoto.

Anasema, ni hali iliyotokana na umoja huo kubaini hatari mazao yao kuharibika katika kipindi watoto hawakuwepo, jambo walilolifurahia chini ya kivuli cha kinachoitwa “Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania.”

Emmanuel Msuta, anasema wanafanya kazi hiyo kwenye shamba la alizeti na viazi vitamu, huku wakiwa na tahadhari kubwa kutokana na ugonjwa wa corona,  ikiwemo kuachiana nafasi ya kutosha kukwepa maambukizi.

Kwa mujibu wa mratibu wa Equip Tanzania, Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Imani Maketa, mradi ulianza mwaka 2018 katika wilaya hiyo yenye shule za msingi 108 na sasa imefanikiwa  kuimarisha sekta ya elimu ya msingi.

Ikungi ni wilaya iliyoanzishwa mwaka 2013 kutoka wilaya ya Singida, imefaulisha darasa la saba na kupanda kutoka nafasi ya  tano mwaka 2017 na asilimia 66.38 kati ya halmashauri saba za mkoa wa Singida, hadi kushika nafasi ya nne mwaka jana (2019) sawa na asilimia 78.34.

 

Habari Kubwa