Kivutio ‘kinachowafolenisha’ watalii kutembelea Hifadhi ya Maghamba

11Jan 2019
Elizaberth Zaya
Lushoto
Nipashe
Kivutio ‘kinachowafolenisha’ watalii kutembelea Hifadhi ya Maghamba
  • Yavunja mwiko watalii wenyeji kuwa adimu

WIKI kadhaa zilizopita, makala yenye simulizi ya kina kuhusiana na Hifadhi ya Maghamba, iliyoko milimani Lushoto, mkoa wa Tanga. Endelea kupata simulizi hiyo, ikifafanua kivutio cha kipekee, Jiwe la Mungu, ambalo limekuwa mtaji mkuu unaowavuta wengi, watalii wa ndani na nje ya nchi. Simulizi kamili

Mandhari ya juu Jiwe la Mungu, ambako mtalii anaweza kushuhudia vijiji jirani kama Mkumbara na Goha, katika vijiji jirani vya wilaya ya Korogwe, huku kwa upande mwingine, Mto Mangha unaonekana vyema. PICHA ELIZABETH ZAYA.

NI umbali wa kilomita 20 kutoka Lushoto mjini, kunakopatikana Jiwe la Mungu’ kivutio hicho chenye unyayo wa binadamu, ambao unaoelezwa kuwasababisha watalii wengi kuona kwamba ni ‘maajabu ya Mungu.’

Huo ni upekee unaoifanya Hifadhi ya Maghamba, kuvutia watalii wengi kutoka ndani na nje ya nchi, wanaomiminika mahali hapo kupata ushuhuda, lakini ikiwa na vivutio vingine vingi vya asili.

Wapo watalii wanaotenga muda au kipindi maalumu cha kwenda katika eneo hilo la Jiwe la Mungu kufanya ibada zao, wakiamini kwamba unyayo huo ulitokana na Mungu na binadamu kufika katika eneo hilo ni baraka na neema.

Ni kawaida watalii wengi wanatenga muda katikati na mwisho wa mwaka, kwa ajili ya kuhakikisha wanafika katika eneo hilo, kufanya ibada au shughuli zingine za kiimani.

Mwandishi wa Nipashe, hivi karibuni alishuhudia utaratibu uliopo ni kwamba watalii wanapofika hifadhini, wanalipa gharama ya kuangalia vivutio kwa mtindo wa ‘kifurushi,’ ambacho kinaelezwa kinampa fursa mtalii kuangalia vivutio tofauti mahali hapo.

Inaelezwa kwamba, sehemu kubwa ya watalii licha ya kulipia vifurushi vingi, kivutio na shinikizo lao ni kupelekwa moja kwa moja katika eneo la Jiwe la Mungu.

OFISA UTALII

Ofisa Utalii wa Hifadhi ya Maghamba, Samji Mlamba anasema Jiwe la Mungu ni kivutio chenye alama inayofanana na nyayo za binadamu iliyopo kwenye mwamba ambao watu wengi wanaamini, asili yake ni nyayo za mwanadamu wa kale.

Anasema mbali na hilo, lakini watu wengi kulingana uelewa na imani zao, wamekuwa wakitafsiri kivutio hicho katika namna mbalimbali, wakiegemea misukumo kama vile imani, dini na kabila zao.

Mlamba anakiri Jiwe la Mungu, kwamba linawabeba watalii wengi zaidi, kuliko vivutio vingine ndani ya hifadhi hiyo ya Maghamba na idadi hiyo imekuwa ikiongezeka kila mwaka, kutokana na namna inavyozidi kutangazwa.

Matangazo hayo ni taarifa katika mifumo rasmi za kitalii na kiserikali kama vile ubalozi, hali kadhalika watalii wanavyopeana taarifa na wenzao kuhusu mazuri hayo ya kitalii.

“Kwa kweli tunajivunia na kumshukuru Mungu kwa maajabu yake. Tuna vivutio vingi katika hifadhi yetu, lakini watalii wengi wanapokuja, pamoja na kutembelea vivutio vingine, lakini unaweza kukuta mwingine anakuambia kwamba jambo la kwanza anaomba kwamba asiachwe kupelekwa katika kivutio hicho cha Jiwe la Mungu,” anaeleza Mlamba.

“Huwezi kumkatalia, inakubidi umpeleke japo anapomaliza, huwa tunashauri kupelekwa kwenye vivutio vingine, Ofisa Habari huyo, anasimulia Mlamba na kuongeza:

“Hii ni njia mojawapo ambayo imesaidia kutuongezea. Pia, idadi kubwa ya watalii, kwa mfano inapotokea tunapata watalii 200, unaweza kukuta kati ya hao hakuna hata mmoja ambaye hataki kufika kwenye Jiwe la Mungu na wengine huwa wanapendelea waanze kwenda huko kwanza, kabla ya kufika katika vivutio vingine na sisi huwa tunajisikia furaha kwa hilo kwa sababu vyote ni vivutio vyetu na lengo ni kuona watalii wanakuja kwa wingi na wanavifurahia.”

Mlamba anasema, kazi yao ni kuhakikisha wanatangaza vivutio vyote na kuwaonyesha watalii vivutio vyote wanavyopendelea kuviona.

Anaongeza: “Huwa tunashuhudia watu wa makabila mbalimbali wanapofika katika Jiwe la Mungu, wanafanya ibada na siyo Watanzania tu, hata watalii wa kutoka mataifa mengine.”

Anataja faida nyingine ya watalii, ni kwamba Jiwe la Mungu liko katika eneo la mwinuko, ambako mtalii anaposimama, anaona kwa urahisi sehemu nyinginezo za Hifadhi ya Maghamba, inayompatia picha halisi ya mandhari yake.

”Ukisimama katika eneo lililopo Jiwe la Mungu, ni kama umepanda kwenye ghorofa, yaani maeneo mengine unayaona kwa bondeni kwa mbali sana, unaona hata mashamba ya mkonge na vitu vingine.

“ Kwa hiyo ni ‘view’ (mwonekano) mzuri sana, ambayo inapendwa na watalii wengi na naona wanapenda kupata ‘peace of mind’ (amani mawazoni). Watu wenye lugha zao huwa wanasema hivyo,” anatamka Mlamba.

Anatumia kauli kwamba kivutio hicho ndicho kimefanikiwa ‘kuwakamata’ watalii wengi wa ndani, kuliko wageni, jambo ambalo limekuwa likiwashangaza.

“Unajua kama binadamu pamoja na kushukuru Mungu kwamba tunapata watalii wengi, lakini kwa namna moja ama nyingine tunashangazwa na kivutio hiki.

“Unajua katika maeneo mengine, huwa tunapiga kelele kuwataka Watanzania kuwa na mwamko katika kufanya utalii wa ndani, lakini katika kivutio hiki wametutia moyo sana, yaani huwa wanakuja kwa wingi mpaka tunashangaa,” anasema.

Mlamba anataja vipindi ambavyo watalii wengi hasa wa ndani humiminika kutembelea Jiwe la Mungu, ni vipindi mwisho wa mwaka na katikati ya mwaka.

Kwa sababu zipi? Mlamba anajibu: “Tunaamini hii husababishwa na idadi ya watalii wengi hasa wa ndani, kupata mapumziko katika vipindi vya mwisho wa mwaka.

Watalii wa ‘rangi nyeupe’ (wageni kutoka Ulaya, Asia, Uarabuni, pia Marekani Kusini na Kaskazini) wengi wao msimu wao ni mwezi wa sita na saba, wanapokuja huwa wanapenda kuangalia pia haya mabaki ya majengo ya Wajerumani. ambayo pia yapo katika eneo la Jiwe la Mungu.”