Kukomesha ujangili kwanusuru mazingira ndani ya hifadhi Rufiji

18Apr 2019
Beatrice Shayo
Rufiji
Nipashe
Kukomesha ujangili kwanusuru mazingira ndani ya hifadhi Rufiji
  • Wahalifu waweka silaha zao chini
  • Wanyama zaidi, majeruhi wafidiwa

ELIMU ya kirafiki ilivyowateka majangili kuwasilisha silaha zao na kuachana na vitendohivyo, baadhi yao kuwasaidia katika mapambano.

Mandhari ya Kijiji cha Mloka, Rufiji. PICHA: MTANDAO

Akizungumza na Nipashe, Mhifadhi wa Wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, Robert Kiondo, anasema elimu waliyoitoa imesaidia kwa kiasi kikubwa na sasa wanapatiwa ushirikiano.

Kiondo anasema, mwaka jana waliwaita watu waliodaiwa kujihusisha na ujangili na kuwajulisha kile wanachotuhumiwa nacho.

“Kabla ya kumchukulia mtu hatua, tuliona tutumie njia mbadala ya kuwaita. Tuliwaita zaidi ya 10 na kukaa nao tukawajulisha tuhuma zao, lakini na sisi tulikuwa tunawasilikiza na wao wanasemaje na baada ya hapo tukawapa onyo kwa njia ya mazungumzo,” anasema.

“Wengine walionyesha ushirikiano na wengine waliahidi kutojishughulisha tena na vitendo vya ujangili. Sisi kazi yetu sio kuzui tu, ila ni pamoja na kutoa elimu na kuwajulisha vitendo vya ujangili. “Sio vizuri na kama kuna ugumu wa maisha, mnaweza kufanya shughuli nyingine za kiuchumi kama kilimo, lakini sio ujangili,” anasema.

Ushuhuda Kiondo anasema, kuna mtu aliyekuwa anajihususisha na ujangili, lakini akabadilika kwa kuwasaidia kuwapa taarifa muhimu za wanaojihusisha na uhalifu huo, baada ya kumpatia elimu na kufanyia kazi huo mtandao, ili tatizo limalizike.

“Kuna wakati tulishirikiana na wahifadhi wenzetu wa Pori la Akiba la Selous, kutoa elimu ya uhifadhi kwa vijiji vinavyozunguka maeneo ya hifadhi, ambako watu waliokuwa wanajishughulisha na vitendo vya ujangili, walibadilika kupitia elimu hiyo na kutoa ushirikiano katika shughuli ya kukabiliana na ujangili.

“Walipita katika vijiji kutoa elimu na kutangaza mtu ambaye anafanya ujangili wa aina yoyote, wajisalimishe ili wapatiwe elimu na kuwa hawatachukuliwa hatua, kama watajisalimisha. Mwitikio ulikuwa mkubwa na jamii inaendelea kuwa na mwitikio chanya,” anasema.

“Tuliamua kutumia busara zaidi katika hili, tunasema mtandao wao ambao wahusika walisaidia kututajia na wengine wanaojishughulisha na ujangili. Njia hii imetusaidia kupunguza ujangili,” anasema.

Aidha, anasema kutokana na jitihada zilizofanywa katika kudhibiti ujangili, tatizo hilo limepungua kwa kiasi kikubwa. Kwa mujibu wa Kiondo, kupungua ujangili wanaupima kwa mengi, ikiwamo ongezeko la matukio ya wanyama waharibifu na hatari, pamoja na kupungua kukamatwa kwa watuhumiwa wa ujangili.

“Sisi tunapima kwa ongezeko la wanyama, halafu tunapima tena kwenye matukio ya wanyama, kwa mfano kipindi cha nyuma ujangili ulikuwa umezidi, wanyama wengi walikuwa wametoweka, lakini sasa hivi wanaonekana kwa wingi na katika makundi makubwa.”

Kiondo anasema, hivi sasa ujangili umepungua na serikali imekuwa makini kutatua changamoto ya ujangili, kwa kushughulikia mtandao wa wafanyabiashara wakubwa wa nyara za serikali, hivyo utaona kuna viashiria vya ongezeko la wanyamapori.

Anasema, kipindi cha nyuma watu walikuwa hawatoi taarifa za wanyama, mfano hai tembo au viboko wanaoingia katika maeneo na wapo wanaofanya ujangili huko waliko.

“Kwa sasa hivi tembo wakiingia katika mashamba ya watu, wanatupatia taarifa na kwenda kutoa msaada. Hii inaonyesha biashara ya ujangili hasa kwa tembo imepungua sana.” Changamoto mashambani “Pia, katika matukio ya mashamba na wanyama, yameongezeka na wanaonekana katika makazi ya watu,” anaeleza Kiondo.

Anasema, changamoto iliyopo ni matukio ya wanyama hatari kuuawa na mali zao kuharibiwa na wanyamapori, yakiwamo mashamba. “Wiki iliyopita, kuna mtu kauawa na mamba na mwingine kajeruhiwa na kiboko.

Yapo matukio mengine yametokea katika kipindi cha nyuma,” anasema. Kiondo anataja lingine ni wananchi kutoelewa kuhusu uhifadhi na hawatoi ushirikiano, wakiwaona wanyama hawana faida kwao, wakiwaacha kwa mtazamo ni mali ya serikali pekee.

Aidha, anasema kwa sasa wanafanya kazi kwa kutumia intelijensia na taarifa za simu, pia kuna Askari wa Wanyamapori wa Vijiji (VGS), wanafanya nao kazi kudhibiti ujangili na kukabili wanyama waharibifu na hatari kwa maisha ya wanadamu ndani ya vijiji mbalimbali.

Anarejea, huko nyuma kulikuwapo matukio na wananchi waliokuwa wasiri kutetea ujangili na unapofika, ambao hawakuwa tayari kutoa taarifa yoyote.

Kiondo anasema, kuna mashirika yaliyosaidia kutoa elimu ya uhifadhi na kuna fedha asilimia 25 ya uwindaji wa kitalii, zinazotolewa na Pori la Akiba la Selous kwa halmashauri, ili ziende katika vijiji kusaidia miradi ya maendeleo.

Anasema Selous na mashirika mbalimbali zimejaribu kuwawezesha wananchi kujua umuhimu wa rasilimali za wanyamapori.

Anasema, kwa sasa pori la Selous linasaidia katika uhifadhi na limekuwa likitoa elimu kwa jamii na vijiji vyote vinavyoizunguka hifadhi hiyo na kila mwaka, kuna fedha zinazotolewa kwa vijiji hivyo wilayani Rufiji. “Zamani unaweza kukuta mnyama kauliwa au kujeruhiwa, lakini jamii kwa sasa ina mwamko katika kutoa ushirikiano katika masuala ya hifadhi.

“Tunaamini kadri siku zinavyokwenda na elimu inayotolewa itasaidia kutoa ushirikiano wa kutosha, ili kufikia malengo ya serikali kupambana na ujangili,” anasema.

Kondo anasema, katika nafasi yao ya uhifadhi wanaendelea na ujirani mwema na jamii, kwa sababu rasilimali hizo zinahusu pia kizazi kijacho, nao waje wazikute salama.

Malipo kifuta machozi Kiondo anasema, serikali inalipa kifuta jasho au machozi kwa waathiriwa wa matukio ya wanyamapori, ambayo jumla ya watu 15 waliojeruhiliwa na wengine kuuawa na wanyamapori katika Halmashauri ya Wilaya Rufiji, walilipwa shilingi milioni 11.6.

Ni fidia hiyo ya matukio yaliyotokea kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka jana. “Sio kwamba inaondoa lile tatizo, lakini angalau inasaidia kufuta machozi.

Hivyo wiki mbili zilizopita, serikali ya Rais John Magufuli, imewawezesha kutoa kifuta machozi kwa ndugu wa mtu aliyeuawa na mnyama,” anasema Kiondo.

“Ndugu amepewa shilingi milioni moja na yule aliyejeruhiwa amepatiwa shilingi 200,000 kama kifuta machozi (ubani),” anadokeza mchanganuo unaowafikia waathirika, kila mmoja, akisema lengo ni kuwahamasisha wananchi watambue uthamini wa serikalini yao.

“Ninamshukuru Rais Magufuli, kwa kuwa jambo hili ni nzuri na hata sisi wahifadhi inakuwa ni rahisi wananchi kutuelewa, hasa lengo la serikali ni nini. “Maana kama huwapi kifuta machozi, wanaona wanyama ndio wanaopendwa kuliko watu, kumbe serikali inajali wananchi wake pamoja na wanyamapori,” anafafanua.

Anasema, kuanzia mwaka 2005 hadi 2008, zaidi ya watu 48 walidhuriwa na wanyamapori, yakiwamo matukio ya vifo wilayani Rufiji.

“Wilaya inafanya jitihada mbalimbali kudhibiti matukio haya kwa kutoa elimu kwa wananchi, pamoja na kudhibiti matukio ya wanyama wakali kabla yakuleta madhara,” anasema.

Kiondo anafafanua, ili mwananchi apatiwe kifuta machozi, taarifa zinapaswa kutolewe kupitia watendaji wa vijiji husika na baadaye kupelekwa wilayani, ambako fomu maalumu ya kifuta machozi inajazwa na kuwasilishwa wizarani kwa hatua zaidi. Anasema, wananchi wanapaswa kutoa taarifa kwa wakati, pindi wanapopatwa matukio hayo, kwa kushirikiana na watendaji wa vijiji, ili wapate vifuta jasho hivyo mapema.

Kiondo anasema wapo ambao hukutana na madhara, ikiwamo kushambuliwa na wanyama wakali kama simba, tembo na chui, huku wananchi wengine wakiweka hisia tofauti dhidi ya wahifadhi.

“Wapo ambao huingia kwenye maeneo ya hifadhi kama mnavyoelewa, baadhi ya wanyamapori ni wakali. Kwa mfano chui wanaweza kujificha usijue. Sasa unavyopita wakakushambulia hadi kupoteza maisha,” anasema.

Pia, anashauri: “Ni vizuri wana nchi wakazingatia sheria kwenye maeneo ya hifadhi kwa kutoingia ovyo kwenye hifadhi za wanyamapori.” Malalamiko ya tembo Kwa upande wake, Asia Selemani, mkazi wa kijiji cha Mloka, katika Tarafa ya Mkongo wilayani Rufiji, anasema wamekuwa wakisumbuliwa na tembo wanaoharibu mazao yao.

Anasema, kwa sasa tembo ni wengi na wanapokuwa wanavamia mazao yao, wanashindwa kuwafukuza kwa sababu hawana uelewa na wanaogopa kuhatarisha usalama wa uhai wao.

“Tungepatiwa askari wa wanyamapori hapa kijijini, ili watusaidie katika kuwaondoa hao tembo wanapovamia mazao yetu. “Kwa mfano lenye mpunga hatoki huwa tunajaribu kuwafukuza hawataki kuondoka, hivyo tungepatiwa hao wataalamu wangetusaidia,” anasema Selemani.

Mwenyekiti Kijiji Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mloka, Ahmed Mloya, anasema kijiji hicho kipo jirani na Pori la Akiba la Selous na kwa sasa imekuwa changamoto kwao wanyama kuingia shambani, wakiwamo tembo.

Mwenyekiti huyo anasema, ni hali inayotokana na ongezeko la wanyama hifadhini na chanzo kikubwa ni matokeo ya jitihada za serikali kupambana na ujangili.

Mloya anasema, wananchi waliodaiwa kuhusika na ujangili, sasa wameacha na kuwasilisha silaha zao serikalini, hivyo sasa wanaelewa umuhimu wa kuhifadhi wanyamapori.

“Kijiji chetu kilipatiwa ufadhili wa kusomesha vijana skauti. Hawa wanatusaidia katika kupambana na ujangili na wanapoona kuna jambo ambalo sio zuri, wanatupatia taarifa na kulifanyia kazi,” anasema.

“Kutunza mazingiza na kuhifadhi hii ni ajenda ambayo tunaifanya katika mikutano yetu kama unavyoona, Mloka pasipo utalii, basi hakuna Mloka. Hatuna kiwanda wala ardhi nzuri ya kilimo.

Huwa tunalima kwa ajili ya kupata chakula,” anasema. Mloya anausifu umeleta maendeleo makubwa na ndio maana wameamua kukabiliana na ujangili, akianisha mbinu zao:

“Wale ambao walikuwa wanamiliki silaha kinyume cha utaratibu, tumewajulisha mamlaka husika na kuja kuzichukua.”

Habari Kubwa