Kutoka ‘wadunga mimba’ sasa walinzi wa mabinti, kufuatilia unyanyasaji

09Nov 2019
Gaudensia Mngumi
Mafia
Nipashe
Kutoka ‘wadunga mimba’ sasa walinzi wa mabinti, kufuatilia unyanyasaji

KUNA msemo kuwa mchawi mpe mwana alee. Hilo ndilo linalofanyika kisiwani Mafia katika Mkoa wa Pwani kwa sasa. Analea mwana kwa sababu watuhumiwa namba moja wa kuwapa wanafunzi mimba ambao ni madereva wa bodaboda, wamebadilika na ndiyo walinzi na watetezi wa mabinti iwe shuleni au mitaani.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Kilindoni, Stephen Mlobi, akizungumza na kusikiliza wanafunzi kuhusu masuala mbalimbali shuleni hapo.

‘Wachawi’ hawa ni walinzi wa wasichana na mabalozi wa wakupinga vita mimba za utotoni, ukatili kijinsia na kuwanyanyasa watoto kingono.

Hivi karibuni Nipashe ilifika Mafia na kukutana na mwamko mpya wa bodaboda ambao ni chachu na chanzo cha mabadiliko na walinzi na watetezi wa watoto na wapinzani wakubwa wa ndoa za udogoni kisiwani humo.

Kwa mujibu wa Selemani Haji, Mtendaji wa Kijiji cha Muburani moja kati ya vijiji 23 vya Mafia, ambacho kina sekondari ya Micheni (shule ya kata), kila mara wanafunzi wa shule hiyo walipopata mimba waliwataja madereva wa pikipiki.

“Kila kesi inayofikishwa ofisi ya kijiji, mwanafunzi anamtaja bodaboda. Walihusika kwa vile wana pesa za papo kwa papo, usafiri wa haraka wa kumfikisha binti shule na kumpeleka sehemu yoyote.” Anasema Haji.

Anaeleza kuwa madereva hawa walionekana na wanafunzi wakiwa hata nyumbani kwao na pia kwenye pikipiki zao na kwa ujumla walikuwa watuhumiwa wakuu kila kesi ilipoibuliwa.

Anaeleza kuwa mabinti walikuwa wahanga kwani wengi hawana usafiri wanatembea zaidi ya kilometa tano kwenda shuleni na kurudi nyumbani.

Aidha, msaada wa karibu kwao ni bodaboda ambazo kwa wanafunzi wengi hawana fedha za kulipia usafiri wala baiskeli, hivyo hutegemea huruma ya lifti ya pikipiki, mwisho wa msaada huo ni hadaa za mapenzi zinazoishia na mabinti kupata mimba.

MBINU ZILIZOTUMIWA

Katika ziara ya wanahabari wilayani Mafia iliyoandawaliwa na Shirika la Action Aid Tanzania (AATZ), kutembelea miradi na wanajamii wanaohudumiwa na shirika hilo, Nipashe ilifika katika Shule za Msingi Balemi na Kilindoni na katika kuzungumzia hadaa na ubakaji unaofanywa kwa wanafunzi, wanataja madereva wa pikipiki na mbinu wanazotumia.

Wanataja mbinu kama madereva kuwapa lifi wanafunzi, kuwanunulia mabinti simu, kuwawekea fedha za matumizi kwenye simu na pia kuwatumia ‘mshiko’ na kuwarubuni kupitia mawasiliano hayo.

Wanadaiwa kuhusika na kuwapeleka mabinti kwenye nyumbani zao, wengine walitumika kuwafikisha kwenye nyumba za wageni au mafichoni ambako wananyanyaswa kingono aidha, wanawapeleka wavulana maporini na kuwalawiti.

Vilevile, wanafunzi hawa wanaeleza kuwa mbinu nyingine zinazotumiwa na madereva hao ni kuwapa watoto wa kiume fedha pengine Sh.10,000 kwa ajili ya kusaidia kuwapata dada zao au kuchonga mchongo wa kuwaletea wasichana wanaowataka.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Kilindoni, Stephen Mlobi, anataja njia nyingine iliyotumiwa na madereva hao na watu wengine wanaowawiti watoto kuwa ni kuwaonyesha picha za ngono kwenye ‘simu janja’ (smartphones) na kuwashawishi kufanya ngono kinyume cha maumbile.

Anasema kwa kutumia simu na hata televisheni nyumbani, kuwapa fedha na zawadi watoto hawa wa kiume wanakubali kuonyeshwa picha hizo na kutumbukia kwenye unyanyasaji huo.

MWANZO MABADILIKO

Mratibu wa Action Aid, Wilaya ya Mafia, Samwel Mesiaki, anaelezea jinsi AATZ ilivyoleta hamasa kuwabadilisha bodaboda kutoka kwenye kutuhumiwa kunyanyasa watoto na kuwaingiza kwenye ubalozi, ulinzi wa wasichana na machampioni wa kupinga ukatili wa kijinsia na kingono dhidi ya watoto.

Anasema pengine ni AATZ Mafia ndiyo wa kwanza kuwatumia madereva hawa kuwa chachu ya mabadiliko.

Na kwamba ili kupanga mikakati ya kukabiliana na unyanyasaji wa watoto kingono, waliwaunganisha na kuwahamasisha madereva hawa kuwa mabalozi jambo ambalo limefanikiwa.

Mesiaki anaielezea Mafia kuwa kuna ukatili wa kijinisia na kingono dhidi ya watoto na pia suala la muhali au jamii kuoneana aibu au haya na kumwona mtuhumiwa wa ukatili huo kuwa ni jamaa na ndugu wa karibu asiyeweza kuchukuliwa hatua, ni suala linalorudisha nyuma kukomesha vitendo hivyo.

Hata hivyo, anaeleza kuwa madereva hawa wameleta mabadiliko. Idadi ya mimba utotoni zimepungua, wasichana wanaomaliza darasa la saba ni wengi zaidi na utoro unapungua na unaelekea kwisha ni moja ya mafanikio, AAT inayojivunia.

Mabalozi 155 wamesajili na wanafanyakazi na AATZ Mafia, lakini jitihada zinafanyika kuongeza idadi ili kuwa na walinzi wengi na watetezi wa watoto, anaongeza Mesiaki.

MTANDAO WA ULINZI

Kuunda mtandao huo ni moja ya mikakati. Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Pikipiki Mafia (Chawapima) Omary Khai, anapozungumzia juhudi hizo anasema kuna wanachama takriban 730 kisiwani kote ambao ni mabalozi wa kupinga unyanyasaji watoto.

Aidha, ili kukomesha ukatili huo wameunda vikundi au vijiwe 42 vipo kila mahali Mafia na wamekubaliana kuwalinda, lakini pia kuwafichua wote wanaowanyanyasa watoto kingono, anasema Khai.

“Tunafuatiliana kwenye vijiwe tukikukamata tunatoa ripoti polisi. Tunao mtandao ambao tunadhibiti uhalifu kuanzia kunyanyasa watoto, biashara haramu za dawa za kulevya na bangi,”anasema Khai.

Mwanachama wa Chawapima, Daniel Peter, anaelezea zaidi namna ya kutimiza wajibu huo kwa kuwalinda watoto kupitia mtandao maalumu uliounganishwa na jeshi la polisi ambao kila wanapoona kuna dalili za udhalilishaji binti au watoto wanafuatilia kuwaarifu polisi.

“Tumekubali kuwalinda watoto wetu. Tunajua asipokuwa mwanao ni wa ndugu yako. Ni raia wa taifa hili. Sisi ni mabalozi tuliojitambua.”

Aidha, Peter anasema pikipiki ndiyo usafiri mkubwa Mafia na kwingineko nchini, ndizo zinazotoa huduma kwa asilimia 95 na kwamba wao ni kila kitu kwenye kusafirisha.

Ni kwasababu wapo kila kona, wametapakaa nchi nzima, wanapenya pale magari yasipofika na ni miongoni mwa wachache wenye kipato ndani ya jamii, hivyo ndiyo wahusika wakuu wa ulinzi wa mtoto.

“Baada ya kuhamasishwa na AATZ sasa tunalinda watoto, kupunguza unyanyasaji, mimba za udogoni na tumekubali kwa hiari yetu.

“Tunaona tuwajibike kwa kuwa wasichana kupewa mimba ni kuongeza umaskini kwa vizazi vya sasa ni vijavyo. Binti atakosa elimu na kiuchumi hataweza kujikimu. Atazidi kuwa maskini atapata watoto wake na uzao wake wataendelea kuwa maskini.”anasema dereva Ali Bakari.

Anasema hilo tunalifanya lakini pia tunakuwa mabalozi wa kuieleza na kuikumbusha jamii yetu kuwa ni lazima tujitambue na kuachana na mazoea hayo yasiyokuwa na tija.

Dereva Maulidi Mpogo, anasema bodaboda ni wepesi na popote pale wanafika ni jukumu la taifa sasa kuwahamasisha na kuwatumia kukomesha uhalifu wa aina mbalimbali ukiwamo ukatili dhidi ya watoto.

WANATOA USHAURI

Kwa serikali, Mwenyekiti wa Chawapima, Omary Khai, anashauri iwashirikishe madereva hao kikamilifu kwenye masuala ya usalama, ulinzi wa watoto na taifa pia.

Anaiomba iwawezesha kufika mikoa mbalimbali kufikisha ujumbe wa kutumiwa kuleta mabadiliko na kusaidiwa kuwa na chombo cha umoja wa wasafirishaji hao ambao ni muhimu nchini.

Kwa madereva wa boda wanakumbushwa kuwa waadilifu na kufuata sheria lakini pia kuwa na hofu ya Mungu kwa kusali na kushiriki ibada.

Aidha, madereva hao wanashauriwa kutumia ujumbe wa kuhamasisha mabadiliko mfano baadhi ya maneno wanayoyaandika kwenye pikipiki yawe na ujumbe kuwa sisi ni walinzi wa watoto , au ni wanabadiliko tunaopinga ndoa na mimba za utotoni au tuwalinde watoto na kuwasaidia kutimiza ndoto na kujenga maisha yao.

KUKABILI CHANGAMOTO

Kutokana na kuwa na mwenendo mbaya madereva hawa wa Mafia wanakiri kuwa jamii inawaona wengine kote nchini kuwa ni kundi la wahuni na wahalifu, wezi na wanaowahadaa na kuwarubuni watoto wa kike.

“Bodaboda tuna sifa mbaya wakati mwingine wazazi wanakataa posa tukitaka kuoa watoto wao. Wanatuita wahuni. Yote haya yamesababisha kupuuzwa na kudharauliwa kutokana na kukosa uadilifu.

Lakini sasa tumejitambua kuwa tuna nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko nchini.” Madereva hawa wanasema walifanyakazi bila kujitambua walijitumbukiza kwenye usafirishaji bila kuwa na elimu ya kujithamini na kujipanga kutumikia taifa ndiyo maana wakaonekana kuwa wasio na maadili.

Hata sasa katika sehemu nyingi sifa si nzuri, hawafanyikazi kwa kujiamini kutokana na kutokujitambua huku jamii ikiwachukulia kuwa ni wahuni, anabainisha Daniel Peter.

TAMKO LAO

Katika mkutano na wanahabari , maofisa wa AATZ na wanajamii kujadiliana mafanikio ya kulinda na kuwa mabalozi wa kuwatetea watoto wa kike, bodaboda wanatoa tamko la kuunga mkono hukumu ya Mahakama ya Rufani ya kukataza ndoa kwenye umri mdogo.

Kwa niaba ya wote Mwenyekiti wa Chawapima, Khai anazungumza:“Tunapenda kuwaambia wenzetu kubeba watoto kwa nia ya kuwashawishi na kuwarubuni kingono watoto wa chini ya miaka 18 na wanafunzi tulichukulie jambo hilo kuwa ni hatia. Tena ni jinai kwani ni kuwapoteza watoto ambao ndilo taifa la kesho.

Lakini pia ni kukwamisha ndoto na maendeleo yao.” Anataka waendesha pikipiki kuwa na hofu ya Mungu na kwenda kwenye ibada za madhehebu yao kama njia ya kuleta mabadiliko ya kiroho.

Anawahimiza wazazi kuzingatia jukumu la kuwalea watoto kimaadili na kujali hatma zao muda wote kwani wengi wamejisahau ndiyo maana watoto wanatumbukia kwenye ngono, mimba za udogoni na uhalifu.

Ali Bakari anawaasa madereva popote walipo kuwaogopa watoto wa chini ya miaka 18 na wanafunzi kama nyara za serikali.

Aidha, anawakumbusha wanaume kujifunza na kuijua adhabu inayotolewa na Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ya kifungo cha miaka 30 jela kwa anayebaka mtoto wa chini ya miaka 18 au mwanafunzi wa na pia kifungo cha maisha kwa wanaowanajisi watoto wadogo kwani adhabu zipo na wengi wanaweza kuishia jela.

 

 

Habari Kubwa